Sayansi na Teknolojia 28
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya matukio muhimu ya sayansi na teknolojia duniani nchini Iran na maeneo mengine duniani hivi karibuni.
Tanzania imezindua maabara ya kwanza ya utafiti wa kemia ya mionzi (Radiochemistry) kwenye Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) mjini Arusha, kaskazini mwa nchi.
Akizungumza mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2019 kwenye uzinduzi wa maabara hiyo ya kisasa iliyogharimu dola za Kimarekani milioni 4.3, Waziri Mkuu wa Tanzanzia Kassimu Majaliwa alisema, nchi yake iko kwenye mstari wa mbele katika kuimarisha udhibiti wa uchimbaji, uchakataji na usafirishaji wa madini ya mionzi, na kuzinduliwa kwa maabara hiyo ni hatua nyingine ya juhudi hizo.
Majaliwa aliishauri TAEC kujenga vinu vya nyuklia, ili kuitayarisha Tanzania kutumia akiba yake kubwa ya madini ya Uranium katika kuzalisha nishati.
Serikali ya Tanzania kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imetangaza kufanikiwa kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya teknolojia ya nyuklia nchini humo. Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekenolojia wa nchi hiyo William Ole Nasha wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Waratibu wa Miradi ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia kutoka nchi 46 wanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) uliofanyika mjini Arusha kuanzia Machi 11 hadi 15 mwaka huu wa 2019.
Akihutubu katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kiufundi ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA barani Afrika, Profesa Shaukat Abdulrazak amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia ya nyukilia kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, kilimo, mifugo, maji, viwanda na ujenzi.
Mwishoni mwa mwaka jana nchi jirani ya Kenya iliomba msaada wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuisaidia kuimarisha matibabu ya saratani katika hospitali mbili kubwa nchini humo na pia kueneza huduma hizo za matibabu katika miji mingine mitatu. Waziri wa Nishati wa Kenya alihutubia kikao cha mawaziri cha IAEA mjini Vienna Austria na kufichua kuwa, nchi hiyo ya Afrika Mashariki iko mbioni kujenga kiwanda cha kuzalisha nishati ya nyuklia kwa ajili ya kuimarisha huduma za matibabu.
Kuanzia Mei 28 2019, mjini wa Geneva, Uswisi kulifanyika mkutano wa siku nne ambao ulilenga kusaka mbinu na mikakati ya kuhakikisha kuwa Akili Bandia kwa Kiingereza Artificial Intelligence au AI inakuwa na manufaa kwa kila mkazi wa dunia hii. Akili Bandia au AI ni akili ya mashine ambayo ina uwezo wa kufanya kazi za kibinadamu.
Mkutano huo uliandaliwa na Shirika la Mawasiliano Duniani, ITU kwa ubia na taasisi 37 za Umoja wa Mataifa. Kikao hicho kililenga kutumia ushawishi wa Umoja wa Mataifa katika kuleta pamoja wadau mbalimbali wa ubunifu na utumiaji wa akili bandia. Miongoni mwa washiriki kulikuwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa, kampuni zinazoongoza kwenye akili bandia na mashirika ya kiraia pamoja na wasomi na wanasayansi kutoka vyuo vikuu zaidi ya 50. Washiriki walijadili njia za kupata miradi ya AI yenye faida kwa jamii lakini pia akili bandia ambayo ni salama, jumuishi kwenye maendeleo na yenye kuweza kutumiwa na wengi iwe ni kwenye sekta ya afya, elimu, ustawi wa kijamii au utafiti.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa ITU, Houlin Zhao alisema kuwa, asilimia 50 ya hataza (Patent Rights) zote za akili bandia zimesajiliwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, na wakati huo huo suala la akili bandia linaibua hoja ya faragha, uaminifu, ubinadamu na usawa. Hali kadhalika amesema AI inaleta changamoto kubwa kwenye ajira, silaha zinazojifyatua zenyewe kiasi kwamba kampuni zenyewe za teknolojia zimeibuka na mbinu za kuhakikisha teknolojia ya akili bandia inakuwa wajibifu.”
Zhao alisema ni dhahiri shairi kuwa hakuna taifa, jamii au kampuni moja inayoweza kukabili hizo changamoto peke yake.
Alisema “mwelekeo wa kuleta mabadiliko thabiti na akili bandia yenye maslahi kwa wote na salama inahitaji ushirikiano wa kipekee baina ya serikali, wanazuoni na kampuni bila kusahau mashirika ya kiraia.”
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Iran Jabbar Ali Zakeri ametangaza kuwa, chuo hicho kitakamilisha ujenzi wa satalaiti iliyopewa jina la Zafar mwezi Septemba mwaka huu wa 2019. Amesema Satalaiti hiyo ya Zafar itakabidhiwa Shirika la Anga za Mbali la Iran (SPA) na kurushwa katika anga za mbali mwezi huo huo.
Amesema kimsingi ujenzi wa satalaiti hiyo umeshakamilika na kile kinachofanyika sasa ni majaribio mbali mbali ya kiufundi. Ameongeza kuwa watafiti katika Kituo cha Utafiti wa Satalaiti cha Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Iran hivi sasa wanajishughulisha na miradi kadhaa ya satalaiti. Ameongeza kuwa, satalaiti ya Zafar ina uzani wa kilo 90 na ina kamera zinazoweza kupiga picha za rangi na pia ina uwezo wa kuchunguza hifadhi za mafuta ya petroli, migodi, misitu na maafa ya kimaumbile.
Iran ilirusha katika anga za mbali satalaiti yake ya kwanza inayojulikana kwa jina la Omid (yaani Tumaini) mwaka 2009. Iran pia imetangaza kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo itatuma mwanaadamu katika anga za mbali. Tayari mazoezi yameshafanyika kuhusiana na lengo hilo kwa kutumwa nyani hai katika anga za mbali ambaye alirejea ardhini akiwa salama. Mafanikio haya ya Iran yanajiri pamoja na kuwepo vikwazo vya kila upande vya nchi za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kislamu.
Na hivi karibuni Rwanda ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa kuchochea mageuzi ya teknolojia ya kidijitali barani Afrika ambao kwa Kiingereza unajulikana kama “Smart Africa Initiative”. Mkutano huo ulihudhuriwa na mwenyeji Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Rais Boubakar Keita wa Mali pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu wa Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiteknolojia ya bara la Afrika. Rais huyo wa Rwanda ndiye mwenyekiti wa sasa wa mpango huo unaolenga kubuni soko moja la kidijitali katika bara hilo kufanikisha biashara na uwekezaji.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika kuanzia Mei 14-17 mwaka huu wa 2019, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alitoa wito kwa nchi za Afrika kuupa kipaumbele ushirikishi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) katika mipango yao ya maendeleo kwani fani hiyo ina uwezo mkubwa wa kuimarisha uchumi wa mataifa hayo.
Rais Kenyatta pia alisema kuwa Kenya iko mstari wa mbele katika kuendeleza matumizi ya teknolojia katika uimarishaji uchumi wa Afrika akitoa mfano wa uvumbuzi wa njia ya kutuma na kupokea pesa kwa simu ya mkono, maarufu kama MPESA. Alisema uvumbuzi huu ni dhihirisho la nafasi chungu nzima zilizoko katika bara hili za kutumia ICT kufanikisha shughuli za kuichumi.