Jun 25, 2019 14:59 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo popote pale mlipo wakati huu. Ninakukaribisheni tena kusikiliza kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) kinachokujieni, siku na saa kama hii, kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hii ikiwa ni sehemu ya 26.

Katika kipindi kilichopita tuliendelea kuzungumzia nafasi chanya ya wanawake, na leo pia tutaendelea kubainisha suala hilo. Ndugu wasikilizaji Imam Khomeini (MA) aliitaja ndoa kuwa uwanja wa kuzuia upotovu katika jamii ya mwanadamu na sababu ya kupatikana jamii salama. Pia aliitaja ndoa kuwa inayokinga matamanio na ghariza na kuyafanya maisha kwenda sawa na mafundisho ya Mitume wa Mwenyezi Mungu na hivyo kupatikana saada ya dunia na mafanikio ya Akhera kwa kusema: “Lengo la ndoa ni kuzuia upotovu katika jamii. Kwa kuyawekea mipaka matamanio jumla, Mitume wa Mwenyezi Mungu walitangaza idara hiyo (yaani ndoa) kuwa eneo la kuzuia ufisadi na machafu. Sio msingi wa matamanio kwa sababu hilo ni jambo la kimaumbile linalopaswa kuchukua mkondo wake wa kawaida, lakini linapasa kuwekewa mipaka. Iwapo malezi na mafunzo yaliyofundishwa na Mitume yatatekelezwa ipaswavyo, ni wazi kuwa dunia ya mwanadamu itarekebika na kupatikana mfumo mmoja na hivyo ukiukaji huu, ukatili na tofauti mbalimbali za kimatabaka hazitakuwepo na wakati huohuo kudhaminiwa maisha mazuri na ya kudumu milele. Fanyeni juhudi za kutoa mafunzo na kuwalea wanadamu ili wapate kutoka katika mipaka ya unyama na kustawi kibinadamu na kiutu.” Hotuba yake mbele ya wanawake tarehe 16/4/1358.

Ndoa katika Uislamu

Baada ya hayo sasa tuelekeze dira ya kipindi chetu hiki katika mtazamo wa Imam kuwahusu vijana. Ndugu wasikilizaji kama mnavyojua, ujana ni kipindi nyeti katika maisha ya wanadamu na sifa za kipekee za kipindi hiki ni kama vile kuwa na hisia, nguvu nyingi, upendo, ushujaa, kufanya juhudi, kupigania matukufu, kutafuta uadilifu, kupigania kujitosheleza, kujitolea na mambo mengi kama hayo. Kadhalika katika kipindi hiki moyo wa mwanadamu na kutokana na usafi wake na kutochafuliwa na vikwazo vya maisha, huwa na msukumo wa kutaka kufahamu zaidi ukweli wa mambo na matukufu ya kibinaadamu na ukamilifu wa kimaadili. Kipindi hiki ni kipindi bora zaidi kwa ajili ya mwanadamu kupangilia mambo yake ili kufikia maendeleo binafsi na ya kijamii. Hii ni kwa kuwa akili ya mwanadamu ina utayarifu kamili kwa ajili ya kupokea maandalizi na vipawa alivyopewa na Mwenyezi Mungu katika njia ya mabadiliko yake. Wale ambao wataweza kutumia vyema vipawa walivyopewa na Mwenyezi Mungu, basi hufikia mustakbali mwema na mafanikio. Ukuwaji wa jamii ya Iran ni wenye nafasi muhimu hususan kwa jamii ya vijana na ni kwa ajili hiyo ndio maana Imam Khomeini (MA) akaupatia uzingatiaji maalumu katika njia ya kuelekea mabadiliko ya kisiasa na kijamii na kukuza vipawa vya vijana. Aliwapa vijana nafasi ya aina yake katika ustawi na maendeleo ya nchi. Kwa kuzingatia umuhimu wa vijana, Imam Khomeini alitoa maelekezo mengi katika uwanja huo.

********

Katika kipindi cha mwamko wa mapinduzi ya wananchi nchini Iran, Imam Khomeini alikuwa pamoja na vijana katika hali ambayo katika ulingo wa kiumri, kulikuwa na tofauti kubwa kati yake na vijana hao. Katika uwanja huo, Imam alikuwa akiwapa vijana heshima na utukufu ambapo pia alikuwa akiwapatia kazi muhimu na nyeti. Katika kipindi cha uongozi wa Imam, vijana wengi waliweza kushikilia kazi na nyadhifa muhimu za serikali na hilo halingefikiwa  kama isingelikuwa imani ya hali ya juu ya Imam Khomeini (MA) kwa vijana na kuamiani uwezo na irada yao kuhusiana na uongozi wao bora katika jamii. Vita vya miaka minane vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na utawala wa Baathi wa Iraq dhdi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, viliwahusisha vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 25 ambapo kutokana na imani ya Imam kwa vijana hao na pia nafasi muhimu na ya kihistoria waliyokuwa nayo, waliweza kupata uzoefu na tajriba kubwa kwa ajili ya kuitumikia nchi yao. Katika kipindi cha mwamko wa Mapinduzi ya Kiislamu pia Imam Khomeini na kwa kutegemea uwezo, irada na imani ya vijana aliweza kuwakusanya mamilioni ya watu kuelekea kwenye medani ya harakati ya Mapinduzi na hivyo kufanikiwa kuung’oa utawala wa kitwaghuti wa Shah. Kwa hakika nafasi muhimu ya vijana ilikuwa yenye kuheshimiwa sana na Imam. Kadhalika katika kipindi cha mwamko wa Kiislamu mwasisi huyo wa Mapinduzi ya Kiislamu alipata kukutana mara nyingi na vijana na kuzungumza nao mambo muhimu, suala ambalo lilikuwa na taathira kubwa kati ya pande mbili. Weledi wengi wa masuala ya kisiasa wanaamini kwamba, shakhsia ya kipekee ya Imam Khomeini (MA) katika nyuga za kiakhlaqi, irfani na kidini na kadhalika azma ya mapambano na sifa yake ya kipekee ya kutetea matukufu na ushujaa wake wa kupigiwa mfano katika kufuatilia matukufu na thamani za kibinaadamu na kisiasa, ni mambo yaliyoleta muungano wenye taathira kubwa kati ya vijana na mtukufu huyo.

**********

Imam Khomeini (MA) alikitambua kipindi cha ujana kuwa kipindi bora muhimu zaidi kwa ajili ya kulea na kuitakasa nafsi na kuhusiana na suala hilo alisisitiza kwamba haifai kulipuuza na kulichelewesha hadi siku za ezeeni, hasa kwa kuwa baada ya kupita kipindi hicho haiwezekani tena kurudisha thamazi zake. Akiwahutubu vijana Imam alisema: “Kiasi chochote ambacho kijana atakuwa ameitakasa nafsi yake ujanani kitamsaidia sana katika mustakbali. Iwapo katika kipindi cha ujana (Mungu aepushie mbali) mtu hataweza kujitakasa na kujirekebisha kinafsi, huenda akakumbwa na matatizo makubwa ambayo humpata mwanadamu katika kipindi cha uzeeni….Hivyo basi kuanzia sasa jifikirini, fikirieni ujana wenu.” Hotuba ya Imam Khomeini ya tarehe 23/8/1344. Katika sehemu nyingine Imam Khomeini (MA) sambamba na kusisitizia udharura wa kuitakasa nafsi katika kipindi cha ujana na kutosubiria hadi kipindi cha uzeeni alisema: “Nyinyi ambao hivi sasa ni vijana na mnazo nguzu za ujana, zidhibitini nguvu zenu hizo wakati huu ambao miili yenu haijakumbwa na udhaifu. Iwapo hamtofikiria kujitakasa muda huu, ni vipi mtaweza kujitakasa wakati mtakapokuwa dhaifu, walegevu, msio na irada imara, maamuzi wala muqawama wa kupambana na maasi? Fahamuni kuwa kadri umri wenu unavyopita, huwa ni vigumu sana kuweza kujirekebisha.” Mwisho wa kunukuu.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 26 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.