Sura ya S’aad, aya ya 34-38 (Darsa ya 828)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 828 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 34 na 35 ambazo zinasema:
وَلَقَدْ فَتَنَّا سُلَيْمَانَ وَأَلْقَيْنَا عَلَىٰ كُرْسِيِّهِ جَسَدًا ثُمَّ أَنَابَ
Na tulimtia mtihanini Suleiman, na tukauweka mwili juu ya kiti chake, kisha akarejea kwa kutubu.
قَالَ رَبِّ اغْفِرْ لِي وَهَبْ لِي مُلْكًا لَّا يَنبَغِي لِأَحَدٍ مِّن بَعْدِي ۖ إِنَّكَ أَنتَ الْوَهَّابُ
Akasema: Mola wangu Mlezi! Nighufirie. Na unipe ufalme usio mwelekea yeyote baada yangu. Hakika Wewe ndiye Mwingi wa upaji.
Katika darsa iliyopita tulizungumzia baadhi ya fadhila na neema ambazo Allah SW alimjaalia Nabii Suleiman (as). Aya tulizosoma zinaashiria moja ya mitihani migumu aliyopewa mja huyo mteule. Tab'an kwa kuwa kilichotokea hasa katika mtihani huo hakikutajwa kwenye aya zenyewe za Qur'ani, tutalielezea suala hilo kwa kutegemea hadithi zinazokubalika zaidi. Nabii Suleiman alikuwa ana matamanio ya kupata watoto wengi, ili mmoja miongoni mwao, aliye shujaa na hodari amchague kuwa mrithi wake wa kuendeleza utawala wake baada ya kuondoka yeye. Lakini kwa vile katika kutamani kwake jambo hilo alimsahau Allah, na badala ya kutawakali na kumtegemea Mola, alitegemea matakwa na irada yake mwenyewe, Mwenyezi Mungu akamtahini kwa kumfanya kila mtoto aliyezaliwa na mmoja wa wake zake, ni mwenye kilema cha kuzaliwa, akawa mithili ya kiwiliwili kisicho na roho kilichowekwa mbele yake. Kwa kushuhudia hali hiyo, Nabii Suleiman (as) akatanabahi na kuelewa kwamba kwa sababu alighafilika na Allah, na moyo wake ukawa umetekwa na mapenzi ya mtoto, Yeye Mola amemtia majaribuni kwa kumtahini. Kwa hivyo akatubia kwa mghafala uliompata na kumrejea Allah na kuomba msamaha. Katika baadhi ya Hadithi imeelezwa kuwa Nabii Suleiman mwenyewe ndiye aliyeumwa sana akaonekana kwenye kiti chake cha enzi mithili ya kiwiliwili kisicho na uhai. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Baada ya Nabii Suleiman kuomba maghufira na msamaha kwa Allah, alimwomba Mola aujaalie utawala wake uwe na mambo makubwa na ya ajabu, ili kama ilivyo miujiza ya Mitume wengine, mambo hayo yawe hoja na ushahidi wa ukweli wa Utume wake. Hali ambayo haikushuhudiwa mfano wake katika tawala nyinginezo; na kwa njia hiyo ikautafautisha utawala wa Nabii Suleiman bin Daud (as) na watawala wengine. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mtihani na majaribu ni moja ya kaida na kanuni za kudumu za Allah, ambayo huitakasa roho na kumfanya mja awe karibu zaidi na Mola wake. Kwa hivyo wanadamu wote, hata Mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu wanatahiniwa, na hakuna mtu yeyote anayetoka nje ya kanuni hiyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, baadhi ya Mitume, mbali na jukumu la Utume na kuwaelekeza watu kwenye uongofu, walikuwa viongozi wa tawala pia; na wala hakuna mkinzano wowote baina ya mawili hayo. Vilevile aya hizi zinatufunza kwamba, tusitosheke na vichache katika kuomba, bali tuwe na hima kubwa kama ya Nabii Suleiman, kwa kumwomba Allah mambo makubwa na muhimu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 36 hadi 38 ambazo zinasema:
فَسَخَّرْنَا لَهُ الرِّيحَ تَجْرِي بِأَمْرِهِ رُخَاءً حَيْثُ أَصَابَ
Basi tukaufanya upepo umtumikie, ukenda kwa amri yake, popote alipo taka kufika.
وَالشَّيَاطِينَ كُلَّ بَنَّاءٍ وَغَوَّاصٍ
Na tukayafanya mashet'ani yamtumikie, wote wajenzi na wapiga mbizi.
وَآخَرِينَ مُقَرَّنِينَ فِي الْأَصْفَادِ
Na wengine wafungwao kwa minyororo.
Aya hizi zinaonyesha kuwa ombi na dua ya Nabii Suleiman ilipokewa na kutakabaliwa. Allah SW alimpa nyenzo, nguvu na mamlaka maalumu, ambayo haukuwahi kuyapata utawala wowote wa kabla na baada yake. Ni mambo yasiyo ya kawaida yaliyo mithili ya miujiza, yanayoonyesha nguvu za msaada wa Allah na hali ya kipekee uliyokuwa nayo utawala wake. Kutiishiwa upepo na kuwa kipando thabiti, ni moja ya at'iya ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu alimtunukia Nabii Suleiman (as). Upepo ulikuwa ukikiinua na kukibeba kiti cha enzi cha Nabii Suleiman na kumfikisha mtukufu huyo popote alipotaka kwenda. Ni mithili ya zilivyo ndege za leo zinazoruka na kupaa angani, zikatumia muda mchache kukata masafa marefu. Neema ya pili ambayo Allah SW alimpa Nabii Suleiman (as) ilikuwa ni kutiishiwa na kudhalilishiwa majini kwa ajili ya kumhudumia na kumtumikia kwa kazi mbali mbali. Kwa mujibu wa aya hizi, mashetani wa kijini walikuwa chini ya utii wa Nabii Suleiman. Kundi moja la majini lilikuwa likifanya kazi za ujenzi kama ujengaji mabwawa na madaraja; na kundi jengine likishughulika kufanya kazi za baharini. Lilikuwepo pia kundi la majini ambao waliasi na kukaidi kutekeleza amri zake, ambao aliwafunga pingu na minyororo na kuwatia gerezani kama wanavyofanyiwa wafungwa wengine. Na kwa namna hiyo, kwa rehma na fadhila zake na kwa njia ya kimiujiza, Allah SW alimwezesha Nabii Suleiman (as) kuwa na nguvu na mamlaka, ya kuzitumia nguvu zote za ulimwengu wa maumbile, na za wanadamu na majini na kuziweka chini ya usimamizi wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, jini ni kiumbe chenye akili, hisia na ujuzi wa mambo maalumu. Kwa hivyo mwanadamu anaweza kuutumia uwezo na vipawa vyake kwa ajili ya kufanyia baadhi ya kazi zake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, katika uendeshaji nchi au utekelezaji miradi na mipango muhimu, kuna udharura na ulazima wa kutumia uwezo na utaalamu wa watu wenye ujuzi na ufanisi katika utendaji. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, watu au makundi ya watu wanaosababisha maafa na madhara kwa jamii na kuvuruga nidhamu ya kijamii, inapasa wakamatwe, wawekwe kizuizini na kudhibitiwa; hatua ambayo ndiyo aliyoichukua Nabii Suleiman kuhusiana na majini waasi na wakaidi. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 828 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kuitumia kila neema aliyotuneemesha katika njia itakayotuwezesha kupata radhi zake. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/