Jul 09, 2019 02:23 UTC
  • Jumanne, tarehe 9 Julai, 2019

Leo ni Jumanne tarehe 6 Dhulqaada 1440 Hijria sawa na tarehe 9 Julai mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita Sudan Kusini ilitangazwa rasmi kuwa nchi huru inayojitawala. Nchi mpya ya Sudan Kusini iliundwa baada ya kujitenga na Sudan. Raia wa Sudan Kusini tarehe Tisa mwezi Julai mwaka 2011 walishiriki kwenye kura ya maoni kwa ajili ya kuainisha mustakbali wa eneo la kusini mwa Sudan na lile la kaskazini, kura ambayo hatimaye ilipelekea eneo la kusini mwa Sudan kujitenga na lile la kaskazini na kuundwa nchi inayojitawala ya Sudan Kusini.

Sudan Kusini

Miaka 17 iliyopita mwafaka na tarehe 9 Julai mwaka 2002 Umoja wa Afrika (AU) ulichukua nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) baada ya kuidhinishwa na wakuu wa nchi za Kiafrika. OAU iliundwa mwaka 1963 ili kusaidia juhudi za kupigania uhuru wa nchi za Kiafrika na kutatua hitilafu miongoni mwa nchi hizo. Hata hivyo siku baada ya siku kulijitokeza hisia kwamba katika mazingira ya ulimwengu wa leo kuna udharura wa kuundwa taasisi yenye nguvu za utendaji na yenye malengo mapya zaidi. Kwa msingi huo katika siku kama ya leo mwaka 2002 wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) waliunda Umoja wa Afrika (AU) katika mji wa Durban, Afrika Kusini. Taasisi kama vile bunge, kamisheni ya utendaji, benki kuu, mfuko wa fedha na mahakama zimezingatiwa katika umoja huo kwa ajili ya kuratibu mawasiliano na kusaidia ustawi wa kiuchumi wa nchi za Kiafrika.

Umoja wa Afrika

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo njama ya mapinduzi ya Nojeh iliyokuwa ikisimamiwa na Marekani nchini Iran iligunduliwa na kuzimwa. Njama hiyo ya mapinduzi iliratibiwa na Shirika la ujasusi la Marekani (CIA) likishirikiana na baadhi ya vibaraka wa jeshi la anga la utawala wa Shah kwa shabaha ya kumuua Imam Khomeini, kuangamiza utawala wa Kiislamu hapa nchini na kumrejesha madarakani  Shapur Bakhitiyar. Waratibu wa njama hiyo ya mapinduzi walikusudia kufanya mashambulizi dhidi ya makazi ya Imam Khomeini mjini Tehran na kumuua na kisha kushambulia kituo cha kuongozea ndege cha uwanja wa Mehrabad. Hata hivyo njama hiyo iligunduliwa na kusambaratishwa na waratibu wa njama hiyo walitiwa mbaroni na kuhukumiwa.

Kituo cha anga cha Shahid Nojeh, Hamedan

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita na baada ya usitishaji vita wa mwezi mmoja, vita kati ya Waarabu na utawala haramu wa Israel vilianza tena. Vita hivyo vilianza baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu mwezi Mei 1948. Vita hivyo vilisimama mwezi Juni mwaka huo kufuatia ombi la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Vita kati ya utawala wa Kizayuni na Waarabu vilipelekea kukaliwa kwa mabavu asilimia 78 ya ardhi ya Palestina na Wapalestina 750,000 kuwa wakimbizi.