Sep 19, 2019 01:27 UTC
  • Alkhamisi tarehe 19 Septemba 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 19 Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria sawa na Septemba 19 mwaka 2019.

Tarehe 19 Muharram mwaka 61 Hijria msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na familia ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein (as) na mashahidi wengine waliouawa na utawala wa Yazid bin Muawiya katika medani ya Karbala uliondoka Kufa nchini Iraq ukielekea Damascus, makao makuu ya serikali ya bani Umayyah. Msafara huo hususan Imam Zainul Abidin na Bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib (as) ulifichua na kuanika maovu ya Yazid bin Muawiyyah na kuwafanya watu wa Kufa wajute sana kwa kumuacha peke yake mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein katika mapambano ya Karbala. Watu wa mji wa Kufa walisikitika sana kutokana na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume na wasiwasi ulizuka juu ya uwezekano wa kuanza harakati ya wananchi dhidi ya utawala wa Yazid mjini humo. Kwa msingi huo mtawala wa Kufa, Ubaidullah bin Ziyad, alikhitari kutuma wajukuu hao wa Mtume wetu Muhammad (saw) huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyyah wakitanguliwa na kichwa kilichotenganishwa na mwili cha Bwana wa Vijana wa Peponi, Imam Hussein (as).

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, mafuta ya petroli ya kutumia makaa ya mawe yalizalishwa kwa mara ya kwanza katika historia ya juhudi za mwanadamu za kupata vyanzo au mada za kuzalisha nishati. Mada hiyo mpya ya kuzalisha joto na nishati ilivumbuliwa na James Young, mwanakemia wa Scotland. Young alikuwa mmiliki wa mgodi wa makaa ya mawe na alifanikiwa kutengeneza mafuta ya petroli kwa kutumia makaa hayo kupitia njia inayojulikana kitaalamu kama (distillation). 

Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, serikali ya kwanza huru iliundwa na viongozi wa mapinduzi nchini Algeria. Harakati za wananchi wa Algeria dhidi ya mkoloni Mfaransa zilianza mwanzoni wa Novemba 1954 sambamba na kushika kasi harakati za kupigani uhuru za wananchi hao. Nalo Jeshi la Ukombozi wa Algeria likaundwa kwa shabaha ya kuratibu mapambano. Tarehe 19 Septemba mwaka 1958 serikali ya muda ya Algeria ikatangaza uwepo wake. Hatimaye kushindwa jeshi la Ufaransa kusambaratisha harakati ya wananchi wa Algeria, kulipelekea Algeria ijitangazie uhuru mwaka 1962.

Bendera ya Algeria

Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, mji wa Susangerd moja kati ya miji ya magharibi mwa Iran ulikombolewa na wapiganaji wa Iran na hivyo kuondoka katika uvamizi wa vikosi vya utawala wa Kibaathi wa Iraq. Ushindi huo mkubwa ilikuwa matokeo ya ushirikiano na uratibu wa karibu baina ya vikosi vya jeshi na makundi ya wananchi.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita Kuwait na Marekani zilisaini makubaliano ya kijeshi. Makubaliano hayo yalisainiwa karibu miezi sita baada ya Iraq kuhitimisha kuikalia kwa mabavu Kuwait. Viongozi wa Kuwait walidai kwamba, lengo la makubaliano hayo, ni kuzuia kutokea tena uvamizi mwingine wa Iraq dhidi ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya kijeshi, Marekani iliruhusiwa kutumia bandari za Kuwait na kutuma wanajeshi na zana zake za kijeshi katika ardhi ya nchi hiyo na nchi mbili hizo kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi. Mwaka 1991, Kuwait ikatiliana saini makubaliano kama hayo na Uingereza na Ufaransa. Miaka iliyofuatia, Bahrain, Qatar, Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu zilisaini makubaliano ya kijeshi na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Hata hivyo kinyume na matarajio ya viongozi wa nchi hizo za Ghuba ya Uajemi, makubaliano hayo badala ya kuwaletea amani, yalipelekea kutokea ushindani wa kumiliki silaha na kushadidi ukosefu wa amani katika Mashariki ya Kati.

Na miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo, wanajeshi elfu 20 wa Marekani walifanya mashambulizi ya anga na baharini na kuikalia kwa mabavu nchi ndogo ya Haiti inayopatikana katika bahari ya Caribean huko kusini mwa Marekani. Washington ilidai kuwa imeishambulia Haiti ili imrejeshe madarakani Rais Jean Bertrand Aristide wa nchi hiyo. Mwezi Septemba mwaka 1991 Jenerali Raoul Cedras alimpindua Aristide ambaye ndio kwanza alikuwa uongozini kwa muda wa miezi minane. Baada ya mapinduzi hayo Rais Jean Bertrand Aristide alikimbia Marekani.

Jean Bertrand Aristide (kushoto)