Sep 25, 2019 01:07 UTC
  • Jumatano, tarehe 25 Septemba, 2019

Leo ni Jumatano tarehe 25 Muharram 1441 Hijria sawa na Septemba 25 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 1346 iliyopita, yaani sawa na tarehe 25 Muharram mwaka 95 Hijiria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, alifariki dunia mjini Madina akiwa na umri wa miaka 38, Imam Ali bin Hussein, maarufu kwa lakabu ya Imam Sajjad au Imam Zainul-Abidin, mtoto wa Imam Hussein (as) na mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (swa). Baada ya mapambano makubwa ya baba yake katika jangwa la Karbala, Iraq Imam Sajjad alikuwa na jukumu zito la kufikisha ujumbe wa mwendelezo wa malengo ya baba yake Imam Hussein (as). Aidha Imam Sajjad alifanya juhudi kubwa za kufundisha tamaduni za Kiislamu na kueneza mafundisho bora ya Qur'ani na suna za Mtukufu Mtume Muhammad (swa) jambo ambalo lilikuwa sababu ya kubakishwa Qur'ani na suna hizo za Mtume. Imam Zainul-Abidin alifahamika kwa uchaji-Mungu mwingi ambapo alikuwa akisujudu sana, na hivyo kupewa lakabu ya 'Sajjad' ikiwa na maana ya mtu mwenye kusujudu sana.

Siku kama ya leo miaka 122 iliyopita alizaliwa mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. Faulkner hakukamilisha masomo yake ya juu na alianza kujishughulisha na kazi mbalimbali ka ajili ya kuendesha maisha. Mwandishi huyo mashuhuri alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili raia weusi wa nchi hiyo. Riwaya za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa sasa nchini Marekani. Mwaka 1950 mwandishi huyo alitunukiwa tuzo ya fasihi ya Nobel.

William Faulkner

Katika siku kama ya leo miaka 50 iliyopita iliasisiwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Jumuiya hiyo ni ya pili kwa ukubwa baada ya Umoja wa Mataifa kwa kuwa na nchi wanachama 57 katika mabara zaidi ya manne. Jumuiya hiyo inahesabiwa kuwa sauti ya ulimwengu wa Kiislamu yenye jukumu la kulinda maslahi ya Waislamu, kueneza moyo wa amani na kuratibu masuala ya Waislamu. Jumuiya hiyo iliundwa katika mkutano wa Kihistoria uliofanyika Rabat nchini Morocco tarehe 25 Septemba mwaka 1969 kama jibu la hatua ya Wazayuni wa Israel ya kuchoma moto Msikiti wa al Aqsa hiko Baitul Muqaddas.

Na siku kama ya leo miaka 16 iliyopita aliaga dunia Edward Said, mwandishi na mwanafikra wa Kipalestina kutokana na maradhi ya saratani. Said alizaliwa mwaka 1935 katika familia ya Kikristo. Alielekea Marekani kwa ajili ya kudumisha elimu akiwa na umri wa miaka 17 na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika Chuo kikuu cha Harvard. Kitu kilichompa umashuhuri zaidi Prf. Edward Said katika upeo wa kimataifa ni jitihada zake kubwa za kuwatetea wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina bila ya kusita. Mwanafikra huyo mtajika alifikisha sauti ya kudhulumiwa wananchi wa Palestina katika masikio ya walimwengu kupita makala na vitabu vyake. Ameandika vitabu vingi na muhimu zaidi ni kile alichokipa jina la Orientalism ambacho ndani yake anaeleza jinsi wataalamu wa masuala ya Mashariki wa Wamagharibi wanavyotumiwa kama wenzo wa wakoloni kwa ajili ya kuhalalisha uporaji wa mali na maliasili za mataifa ya Mashariki mwa dunia.

Edward Said