Jumapili, tarehe 29 Septemba, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 29 Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria, mwafaka na tarehe 29 Septemba 2019 Miladia.
Siku kama ya leo, miaka 538 iliyopita alifariki dunia Muhammad Heravi, mwanahistoria wa Kiislamu huko mjini Herat, magharibi mwa Afghanistan ya leo. Heravi, alizaliwa katika familia maarufu mjini Balkh, kaskazini mwa nchi hiyo lakini aliishi umri wake mwingi katika mji wa Herat. Kutokana na elimu yake kubwa, alipewa heshima na mazingatio makubwa na Ali-Shir Nava'i, waziri msomi wa silsila ya watawala wa Mughal, ambaye alikuwa akiwaheshimu sana wasomi na wanazuoni. Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Tarikh Raudhati Swafaa kinachochunguza historia ya dunia tangu kuumbwa kwake hadi zama za msomi huyo.

Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita, alizaliwa mwanafizikia mashuhuri wa Italia Enrico Fermi katika mji wa Roma. Baada ya kukamilisha masomo ya chuo kikuu aliweza kuvumbua kanuni ya Mwendo wa Molekuli ya Gesi. Fermi alifanya uchunguzi kuhusu mabadiliko ya atomu na akafanikiwa kutengeneza betri ya atomu kwa kuipasua na kutoa nje nishati yake. Mwanafizikia huyo wa Italia alifariki dunia mwaka 1954.

Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita, alifariki dunia mwandishi wa Kifaransa Emile Zola. Zola alizaliwa mjini Paris mwaka 1840. Alipata kuandika vitabu vingi katika elimu tofauti. Kitabu chake cha kwanza kinaitwa "Mwanamke Mvaa Gunia" na kitabu chake mashuhuri kinaitwa "Nana" na "Zherminal."

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, nchi ya Bulgaria ilisalimu amri baada ya kushindwa mara kadhaa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Bulgaria ilikuwa pamoja na Ujerumani, utawala wa Othmania na Austria na Hungary na zilikuwa zikipigana dhidi ya Ufaransa, Russia, Uingereza na Italia. Baada ya Bulgaria kushindwa katika vita vya Macedonia, Desemba 15 mwaka 1918 ilitia saini Mkataba wa Salonica katika mji wenye jina hilo nchini Ugiriki ya leo.

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mehr 1360 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Hujjatul Islam Sayyid Abdul Karim Hasheminejad mwanachuoni na mwanamapambano shupavu wa Iran katika mji wa Mashhad. Sayyid Hasheminejad aliuawa shahidi baada ya kupigwa risasi na mmoja wa wanachama wa kundi la Munafikiin. Mwanachuoni huyo alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi nchini Iran dhidi ya utawala wa Shah, na aliwahi kuteswa na kuwekwa gerezani mara kadhaa.

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, makamanda 5 wa ngazi za juu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walikufa shahidi katika ajali ya ndege. Makamanda hao walikuwa wakirejea kutoka katika oparesheni za kuukomboa mji wa Abadan ulioko kusini magharibi mwa Iran. Mji huo wa Abadan ulikuwa umezingirwa na jeshi vamizi la dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein. Makanda hao ni Shahidi Fallahi, Shahidi Fakuri, Shahidi Namjuu, Shahidi Kolahduz na Shahidi Jahan-ara aliyekuwa kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mjini Khoram Shahr. Katika ujumbe wa kusifu na kushukuru mchango wa mashahidi hao baada ya tukio hilo Imam Khomein MA aliwataja kuwa mashahidi wa Uislamu.

Na siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, ulifanyika uchaguzi huru wa kwanza nchini Angola. Katika uchaguzi huo chama cha MPLA kilichokuwa kikiongoza nchi hiyo tangu mwaka 1976 kilipata ushindi na kiongozi wake Jose Edward Dos Santos akachaguliwa tena kuingoza nchi hiyo. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Angola ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno hapo mwaka 1975. Vita vya ndani nchini humo vilihitimishwa rasmi mwaka 2002 baada ya kuuawa kiongozi wa chama cha upinzani cha UNITA Jonas Savimbi aliyekuwa akiungwa mkono na Marekani.
