Oct 05, 2019 02:37 UTC
  • Jumamosi, 5 Oktoba, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 6 Mfunguo Tano Safar 1441 Hijria sawa na tarehe 5 Oktoba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 807 iliyopita, alizaliwa mwanafalsafa, mnajimu na tabibu mashuhuri wa Kiislamu Qutbuddin Mahmoud Shirazi katika mji wa Shiraz nchini Iran. Alianza kujifunza tiba akiwa bado mdogo na alianza kutibu wagonjwa katika moja ya hospitali za Shiraz baada ya kufariki dunia baba yake. Katika kipindi cha miaka kumi ya kazi ya utabibu, Qutbuddin Shirazi alitalii vitabu mbalimbali vya tabibu mwingine wa Kiislamu Bin Sina na vitabu vingine vya tiba na falfasa. Baada ya kuasisiwa kituo cha utafiti wa elimu ya nujumu katika eneo la Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran, Qutbuddin Shirazi aliishi kipindi kirefu na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi na kupata elimu ya nujumu. Katika kipindi chote cha umri wake, tabibu huyo wa Kiislamu alitembelea miji na nchi mbalimbali na kukutana na wasomi na maulamaa wa maeneo hayo. Ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Jaamiul Usul na Nihayatul Idrak. Alifariki dunia mwaka 710 Hijria. ***

Qutbuddin Mahmoud Shirazi

Katika siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, alizaliwa Louis Jean Lumiere, mwanakemia mwanaviwanda mashuhuri wa Kifaransa. Mwaka 1895 akiwa pamoja na ndugu yake aliyejulikana kwa jina la Auguste Lumiere, walifanikiwa kutengeneza kifaa ambacho kiliwasaidia kuchukua picha mbalimbali na kusajili harakati. Mwaka huo huo Lumiere alifanikiwa kuonyesha filamu yake ya kwanza au Motion Picture katika majumba ya sinema. ***

Louis Jean Lumiere

Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo  Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliondoka Iraq na kuhamia Paris, Ufaransa. Imam Khomeini aliamua kufanya hijra hiyo ya kihistoria wakati utawala wa zamani wa Iraq ulipoanza kumzuia kufanya harakati za mapambano dhidi ya utawala wa Shah. Serikali ya wakati huo ya Iraq ambayo ilikuwa ikilinda uhusiano wake na utawala wa Shah nchini Iran, ilimtaka Imam Khomeini ajiepushe na harakati zozote za kisiasa na za kimapinduzi dhidi ya utawala huo wa Shah. Hata hivyo Imam aliiambia serikali hiyo kuwa hilo lilikuwa jukumu lake la kisheria ambalo aliwajibika kulitekeleza na kusisitiza juu ya kuendelezwa mapambano kwa kutoa hotuba na kutuma kanda za kimapinduzi nchini Iran. ***

Hijra ya Imam Khomeini (MA) kuelekea Paris, Ufaransa

Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita,  Slobodan Milosevic dikteta wa zamani wa Yugoslavia na mhusika mkuu wa vita vya umwagaji damu huko Balkan, alijiuzulu baada ya miezi kadhaa ya malalamiko ya ndani na vikwazo vya kimataifa. Milosevic alikuwa rais wa Serbia tangu mwaka 1990 hadi 1997 na baadaye akawa Rais wa Jamhuri ya Yugoslavia. Katika vita vya Bosnia, na kwa uungaji mkono wa kila upande wa Waserbia, Slobodan Milosevic alishiriki pakubwa katika kutekeleza mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu wa Bosnia Herzegovina. Milosevic alikuwa kiongozi wa kwanza mtenda jinai za kivita kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa kwa ajili ya kuhukumiwa. Hata hivyo mhalifu huyo katili alifariki dunia akiwa katika korokoro za mahakama hiyo huko The Hague nchini Uholanzi kutokana na mwendo wa kinyonga wa kushughulikia kesi yake. **

Slobodan Milosevic

Na tarehe 5 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu. Siku hii ilitangazwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 8 mwezi Septemba mwaka 1994 kwa ajili ya kuenzi mchango wa walimu na nafasi yao kubwa katika jamii ya mwanadamu.

Siku ya Kimataifa ya Mwalimu