Oct 07, 2019 23:47 UTC
  • Jumanne tarehe 8 Oktoba 2019

Leo ni Jumanne tarehe 9 Safar 1441 Hijria sawa na tarehe 8 Oktoba 2019.

Katika siku kama ya leo miaka 1404 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, aliuawa shahidi Ammar bin Yassir, sahaba mkubwa wa Mtume Muhammad (saw) na msaidizi wa karibu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Ammar bin Yasir aliuawa katika vita vya Siffin vilivyojiri kati ya majeshi ya Imam Ali (as) na Muawiya bin Abi Sufian. Ammar alizaliwa miaka 57 kabla ya Hijra ya Mtukufu Mtume na wazazi wake wawili, yaani Yassir na Sumayyah, ndio waliokuwa mashahidi wa kwanza katika Uislamu. Sahaba huyu mtukufu alisimama imara dhidi ya maudhi ya makafiri na alishiriki katika vita mbalimbali pamoja na Bwana Mtume (SAW). Wakati mmoja Mtume alimwambia Ammar: "Ewe Ammar! Baada yangu kutatokea fitina, na katika hali hiyo mfuate Ali bin Abi Twalib na kundi lake, kwani Ali yuko pamoja na haki na haki iko pamoja na Ali.

Siku kama ya leo miaka 1020 iliyopita, alifariki dunia Abu Ali Maskawayh, mtaalamu, mwanahistoria na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu. Miskawayh alizaliwa mwaka 320 katika mji wa Rei ulio karibu na mji mkuu wa Iran ya sasa. Miskawayh alikuwa mwalimu katika elimu za zama zake sambamba na kufanya utafiti katika elimu ya tiba, kemia, historia na falsala. Miongoni mwa athari zilizobakia za Abu Ali Miskawayh ni pamoja na kitabu kiitwacho "Tahdhibul-Akhlaq", "Tajaaribul-Umam" na "Jaavidaane Kherad."

Tarehe 9 Safar miaka 846 iliyopita yaani tarehe tisa Safar mwaka 595 Hijria, alifariki dunia Ibn Rushd Andalusi, msomi mkubwa wa falsafa wa Kiislamu. Abul-Walid Muhammad Bin Ahmad Bin Rushd, ambaye alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa elimu ya falsafa wa Kiislamu katika karne ya 6 Hijiria, alikuwa pia mtaalamu katika elimu za fiqhi, hadithi, fasihi, mantiki na elimu nyingine za wakati huo. Ibn Rushd aliyekuwa akiishi Andalusia (Uhispania ya leo) alikuwa mtu wa karibu kwa mfalme na miongoni mwa makadhi wa eneo moja la utawala wa kifalme. mwanafalsafa huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi kikiwemo cha 'Bidaayatul-Mujtahid' 'Falsafatu Ibn Rushdi' na 'al-Kulliyaat'.

Ibn Rushd Andalusi

Katika siku kama ya leo miaka 108 iliyopita, vita vya Balkan vilianza kwa ushiriki wa Bulgaria, Serbia na Ugiriki dhidi ya Utawala wa Othmania. Ufalme wa Othmania kwa miaka kadhaa mtawalia ulikuwa umefanikiwa kuyafanya maeneo mengi ya magharibi mwa Asia, kaskazini mwa Afrika na mashariki mwa Ulaya kuwa chini ya udhibiti wake na hivyo ukawa umetanua utawala wake. Vuguvugu la kulitaka kujitenga nchi zilizokuwa chini ya utawala huo lilikuwa likipelekea kutokea vurugu mara kwa mara na vita vya Balkan ni moja ya harakati hizo.

vita vya kwanza vya Balkan

Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha rishta uliyakumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa Pakistan. Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa katika mji wa Muzaffarabad. Watu karibu 90,000 walipoteza maisha yao na wengine 3,300,000 kubaki bila makazi.