Nov 10, 2019 09:20 UTC
  • Jumapili, tarehe 10 Novemba, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 12 Rabiul-Awwal 1441 Hijiria, sawa na tarehe 10 Novemba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1494 iliyopita, yaani tarehe 12 Rabiul-Awwal mwaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Masoudi, alizaliwa Mtume Muhammad (saw). Hii ni katika hali ambayo wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha pamoja nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita, sawa tarehe 12 Rabiul Awwal mwaka wa kwanza Hijria, Mtume Muhammad (saw) aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa msikiti wa kwanza kabisa katika Uislamu katika kijiji cha Quba kilichoko pambizoni mwa Madina. Mtume (saw) aliweka jiwe la msingi la msikiti huo wa kihistoria wakati aliposimama kwa siku chache katika eneo la Quba akiwa njiani kutoka Makka kuelekea Madina. Mtukufu huyo alisimama kwa muda katika kijiji cha Quba akimsubiri Ali bin Abi Twalib na jamaa wa familia ya Mtume, kwa kuwa wakati wa hijira ya Mtume wa Allah, Imam Ali alilala kwenye kitanda cha mtukufu huyo, kwa lengo la kumsalimisha Nabii wa Allah (saw) na njama chafu za washirikina wa Makka. Baada ya hapo Imam Ali alibakia mjini hapo kwa muda wa siku tatu kwa madhumuni ya kurejesha amana za watu, zilizokuwa zimewekezwa kwa Mtume (saw). Ni baada ya hapo ndipo Amirul-Muuminina akiwa na watu wa karibu ya Mtume, akaelekea Madina. Msikiti wa Quba uliotumika kwa ajili ya kutatua matatizo ya Waislamu, licha ya kufanyiwa mabadiliko mengi, unahesabika kuwa msikiti wa kihistoria na mtukufu sana mjini Majina.

Mwonekano wa sasa wa Msikiti wa Quba

Siku kama ya leo tarehe 12 Rabiul Awwal miaka 1200 iliyopita, alifariki dunia Imam Ahmad bin Hanbal mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Baghdad, Iraq ya leo. Ahmad bin Hanbal alizaliwa mwaka 124 Hijria, katika mji wa Baghdad na kupata elimu ya kidini katika mji huo kutoka kwa maulamaa wakubwa akiwemo Imam Shafii. Imam Hanbal alifanya safari katika miji kadhaa kama vile Kufa, Basra, Makka, Madina, Sham na Yemen kwa minajili ya kukusanya hadithi za Bwana Mtume SAW. Ahmad bin Hanbal ndiye mwasisi wa madhehebu ya Kisuni ya Hanbal na mwandishi wa kitabu mashuhuri cha hadithi cha al Musnad.

Ahmad bin Hanbal

Siku kama ya leo miaka 536 iliyopita yaani tarehe 10 Novemba 1483,  alizaliwa Martin Luther mpigania mageuzi ya kidini wa Kijerumani. Luther alikuwa padri wakati akiwa kijana. Mitazamo ya Martin Luther kuhusuiana na dini ya Kikristo ilitofautiana na baadhi ya mitazamo ya Papa na viongozi wa ngazi za juu wa kanisa na kuanzia mwaka 1517, Luther alidhihirisha mapambano na upinzani wake dhidi ya dhulma na ukandamizaji wa kanisa. Martin Luther alipinga waziwazi agizo la Papa wa Kanisa Katoliki kwa kuifasiri Injili kwa lugha ya Kijerumani na akaanzisha harakati ya kiprotestanti dhidi ya kanisa hilo.

Martin Luther

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, sawa na tarehe 10 Novemba 1912, Morocco iliwekwa chini ya himaya ya wakoloni wa Ufaransa na Uhispania. Kabla ya hapo Morocco ilikuwa ikidhibitiwa na tawala kama vile Carthage, Roma, Othmania na Italia. Uislamu uliingia Morocco mwishoni mwa karne ya 7 na nchi hiyo ikapewa jina la Maghrib kutokana na ardhi yake kuwa upande wa magharibi mwa ardhi ya nchi za Kiislamu. Sambamba na kuanza ukoloni rasmi wa Ufaransa na Uhispania katika nchi hiyo, kuliibuka mapambano ya silaha ya raia wa nchi hiyo dhidi ya wakoloni hao. Na hatimaye Morocco ikafanikiwa kupata uhuru wake mwaka 1956 Miladia, baada ya kujiri vita vya muda mrefu na umwagaji damu mkubwa.

Bendera ya Morocco

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, Dakta Sayyid Hussein Fatimi Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Dakta Muhammad Musaddiq aliuawa kwa kupigwa risasi na vibaraka wa utawala wa Shah nchini Iran. Dakta Fatimi kabla ya hapo alikuwa amehukumiwa kunyongwa na mahakama moja ya kijeshi ya kimaonyesho ya utawala wa Shah huku akiwa mgonjwa sana. Baada ya mapinduzi ya Marekani na Uingereza ya tarehe 28 Mordad mwaka 1332 Hijria Shamsiya hapa nchini na baada ya kujiuzulu Dakta Musaddiq, Dakta Sayyid Hussein Fatimi alikuwa akisakwa na vibaraka wa utawala wa Shah na alikuwa akiishi kwa kujificha. Alikamatwa na kunyongwa katika siku kama ya leo.

Dakta Sayyid Hussein Fatimi katikati akiwa katika mahkama ya kijeshi enzi hizo

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, Leonid Brezhnev aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti cha Urusi ya zamani na hivyo kushika hatamu za kukiongoza chama hicho. Mwaka 1931, Brezhnev alijiunga na kuwa mwanachama wa chama hicho cha Kikomonisti. Mashambulizi ya Urusi dhidi ya Czechoslovakia na kuvamiwa kijeshi Afghanistan kulifanyika katika zama zake.

Leonid Brezhnev

Na katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita,  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 3379 lililoutambua uzayuni (Zionism) kuwa aina ya ubaguzi wa rangi. Azimio hilo lilitoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kufichua utambulisho halisi wa utawala huo. Azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliikasirisha sana Israel na waungaji mkono wa utawala huo wa kibaguzi hususan Marekani. Tofauti na mafundisho ya Kiyahudi, fikra za uzayuni ambazo zilianzishwa mwishoni mwa karne ya 19 zinawatambua wafuasi wa dini hiyo kuwa ndio kizazi bora zaidi kuliko jamii nyingine zote duniani. Kwa mujibu wa fikra hiyo, Wazayuni wa Israel wanawatambua watu wa Palestina kuwa ni kizazi duni na hakiri zaidi na kwa sababu hiyo wanawakandamiza, kuwaua na kuwafukuza katika makazi na maeneo yao ya asili.

Bendera ya utawala haramu wa Kizayuni ambao ni utawala wa kibaguzi