Jumapili, tarehe 17 Novemba, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 19 Mfungo Sita Rabiul Awwal 1441 Hijria, mwafaka na tarehe 17 Novemba 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 302 iliyopita, Jean le Rond d'Alembert mwanahisabati wa Kifaransa alizaliwa katika mji wa Paris huko Ufaransa. Baba na mama yake walimtelekeza kando ya kanisa moja mjini Paris akiwa mtoto mchanga. Aliokotwa na kulelewa na mwanamke na mwanaume mmoja waliokuwa wauza vioo. Jean le Rond d'Alembert alisoma kwa bidii na baada ya kuhitimu masomo ya kati alianza kusoma taaluma ya tiba na sheria. Hata hivyo baada ya muda aliondokea kuipenda mno taaluma ya hisabati ambapo alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo. Alipotimiza umri wa miaka 22 d'Alembert alizindua makala kuhusiana na hesabu, makala ambayo yalimpatia umashuhuri mkubwa. Ameacha athari mbalimbali ambazo zipo katika maktaba za Ufaransa. Jean le Rond d'Alembert alifariki dunia tarehe 29 Oktoba 1783 akiwa na umri wa miaka 66.
Siku kama ya leo miaka 223 iliyopita, Catherine the Great malkia mashuhuri wa Russia aliaga dunia. Alizaliwa Mei Pili 1729 na akiwa na umri wa miaka 15 aliolewa na Peter III. Hata hivyo Peter III mfalme wa wakati huo wa Russia hakuwa akimpenda mkewe huyo na alikuwa akimvunjia heshima na kumdhalilisha mbele za watu. Mwaka 1762 wakati Peter III alipokuwa ametoka nje ya mji, Catherine the Great alijitangaza kuwa malkia wa Russia. Peter III ambaye alishtushwa na kupata pigo kwa hatua hiyo alilazimika kujiuzulu pasina ya mapambano na baada ya siku chache akaaga dunia.
Siku kama ya leo miaka 161 iliyopita, Robert Owen mpigania mageuzi ya kisoshalisti wa Wales na mmoja wa waasisi wa Harakati ya Usoshalisti aliaga dunia. Alianza harakati zake tangu akiwa na umri wa miaka 18 sambamba na kujenga kiwanda cha ufumaji. Katika kiwanda chake hicho kwa mara ya kwanza alianza kuboresha hali ya afya na ustawi wa wafanyakazi barani Ulaya kwa kupunguza masaa ya kazi kutoka masaa 14 kufikia masaa 10.
Siku kama ya leo miaka 150 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 17 Novemba mwaka 1869, Mfereji wa Suez unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu ulifunguliwa. Uchimbaji wa mfereji huo ulisimamiwa na mhandisi wa Kifaransa Ferdinand de Lesseps katika kipindi cha miaka 10 huku ukiwa na urefu wa kilomita 168 na upana wa mita 120 hadi 200. Karne kadhaa kabla yake, Mfalme Daryush wa Iran na baadhi ya wafalme wa Misri walichukua hatua kadhaa za kuanzisha mfereji baina ya bahari hizo mbili, suala ambalo linaonyesha umuhimu wa Mfereji wa Suez unaopunguza kwa kiasi kikubwa masafa ya kutoka Asia kuelekea Ulaya, safari ambayo zamani ilikuwa ikifanyika kupitia Afrika Kusini.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na Libya ulianza tena. Uhusiano huo ulikuwa umekatika kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Hilo lilitokana na hatua ya Kanali Muammar Gaddafi Kiongozi wa wakati huo wa Libya ambaye alikuwa akiutambua utawala wa kifalme wa Kipahlavi hapa nchini kuwa, ulikuwa ukifungamana na ubeberu wa Marekani ambao ulikuwa ukitanguliza mbele maslahi na manufaa ya Magharibi na utawala vamizi wa Israel mbele ya maslahi ya nchi za Kiarabu na Wapalestina.

Na siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq liliasisiwa kutokana na vyama na makundi mbalimbali yaliyokuwa yakiupinga utawala wa dikteta Saddam Hussein. Lengo la kuasisiwa baraza hilo lilikuwa ni kuwaokoa wananchi wa Iraq na dhulma pamoja na ukandamizaji wa utawala wa Chama cha Baath. Kufuatia mashambulio ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq na kuangushwa utawala dhalimu wa Saddam, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq, lilihamishia harakati zake za kisiasa ndani ya ardhi ya Iraq na kuwa na nafasi muhimu katika uwanja huo.