Alkhamisi 21 Novemba 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Rabiul Awwal 1441 Hijria sawa na Novemba 21 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 1240 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Bibi Fatma Maasuma dada wa Imam Ali bin Mussa al-Ridha AS aliwasili katika mji wa Qum, Iran. Mwaka mmoja baada ya safari ya kubaidishwa kaka yake na kupelekwa uhamishoni katika mji wa Marv, Bibi Maasuma alifunga safari kwa ajili ya kwenda kuonana na kaka yake. Baada ya kuwasili Qum, aliishi katika mji huo kwa siku 17 na katika kipindi hicho alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubisha kwa Mola Muumba. Eneo alilokuwa akifanyia ibada mjukuu huyo mwema wa Mtume (saw) hadi leo linajulikana kama 'Baitul Nur, na linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (SAW). Mwishowe tarehe 10 Rabiul Thani mwaka 201 Hijiria, kabla hajakutana na kaka yake, Imam Ridha AS, Bibi Fatima Maasuma alifariki dunia akiwa katika upweke na majonzi makubwa. Hii leo haram ya BibI Fatma Maasuma AS mjini Qum ni miongoni mwa maeneo matakatifu ambapo watu kutoka katika maeneo mbalimbali ya dunia huenda kufanya ziara katika eneo hilo.
Miaka 236 iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Novemba mwaka 1783, kwa mara ya kwanza katika historia ya jitihada za mwanadamu za kupaa angani, puto lilitumwa angani. Puto hilo lilikuwa limepandwa na watu wawili mmoja akiwa mwanafizikia wa Ufaransa aliyejulikana kwa jina la Pilatre De Rozier. Tangu alipokuwa masomoni De Rozier alikuwa akifikiria kutengeneza wenzo wa kupaa angani na kwa kutengeneza puto hilo mwanafizikia huyo akawa amefanikiwa kuruka angani.
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Ayatullah Mirza Javad Agha Tehrani alimu na mwanazuoni mchaji-Mungu. Alizaliwa mjini Tehran katika familia iliyokuwa imeshikamana kikamilifu na dini. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali alielekea katika mji wa Qum Iran na baadaye Najaf Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Akiwa katika huko Ayatullah Tehrani alihudhuria darsa na masomo ya walimu mahiri wa zama hizo. Miongoni mwa sifa alizopambika nazo Ayatullah Mirza Javad Agha Tehrani ni uchaji Mungu, kuipa kwake mgongo dunia na mapenzi yake makubwa kwa Ahlul-Beit AS. Msomi huyo wa Kiislamu hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi wa vitabu.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, Butros Butros Ghali alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa sita wa Umoja wa Mataifa. Butros Ghali alizaliwa mwaka 1922 katika familia ya Kikristo katika mji mkuu wa Misri Cairo. Baada ya kumaliza masomo yake Butros Butros Ghali alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Siasa cha Cairo. Mwanadiplomasia huyo ndiye aliyemshawishi na kumshajiisha Anwar Sadat Rais wa zamani wa Misri kutia saini mkataba wa Camp David mwaka 1978 na katika kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel.
Katika siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza na kuiainisha siku hii ya tarehe 21 Novemba kuwa Siku ya Kimataifa ya Televisheni. Lengo la Umoja wa Mataifa la kuianisha siku hii lilikuwa ni kuweko mabadilishano ya vipindi vya runinga hususan vipindi vinavyotayarishwa kwa lengo la kueneza amani, ustawi wa kijamii, kiuchumi na kuimarisha masuala ya kiutamaduni ya jamii.