Jumanne, tarehe 26 Novemba, 2019
Leo ni Jumanne tarehe 28 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1441 Hijria inayosadifiana na Novemba 26 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka miaka 164 iliyopita, Adam Bernard Mickiewicz mshairi na mwandishi mkubwa wa Kipoland aliaga dunia huko Istanbul uliokuwa mji mkuu wa utawala wa Othmania. Alizaliwa mwaka 1798. Kama alivyokuwa baba yake, Mickiewicz naye alikuwa mtu aliyekuwa akipigania uhuru. Aliishi katika zama ambazo nchi yake ya Poland ilikuwa imegawanywa na madola ya Prussia, Russia na Austria na alikuwa akifanya jitihada ili nchi yake iungane tena na kuwa kitu kimoja. Ni kutokana na sababu hiyo ndiyo maana mwaka 1823 alibaidishiwa nchini Russia. Baada ya miaka 6, Adam Mickiewicz alikimbilia nchini Ufaransa na kuanza kufundisha fasihi ya lugha.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 85 Ayatullah Muhammad Gharawi Kashani, msomi mkubwa wa sheria za Kiislamu (fiqhi) na mwanamapambano mkubwa wa wa ulimwengu wa Kiislamu nchini Iran. Alizaliwa mjini Kashan, moja ya mikoa ya katikati mwa Iran katika familia ya elimu na watu wa fadhila. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi msomi huyo mkubwa alianza kusoma elimu ya dini mjini Kashan na Isfahan ambapo baada ya hapo alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kuendelea zaidi na masomo. Akiwa mjini Najaf, Ayatullah Muhammad Gharawi Kashani alipata kusoma kwa maulama wakubwa wa mji huo. Aidha alimu huyo hakutenganisha katu kati ya elimu na dini na daima aliamini kuwa ni mambo yasiyokubali kutengana. Mbali na kuwalea wanafunzi, pia alikuwa akipambana vikali na utawala wa kidikteta wa Shah.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, jeshi la kujitolea la wananchi (Basiji) liliundwa kutokana na amri ya Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuundwa jeshi la watu milioni 20 nchini Iran. Taasisi hiyo ya wananchi kutoka matabaka mbalimbali ya kijamii, kwa kuwa na wapiganaji wenye imani, moyo wa kujitolea na ari ya kuchapakazi imekuwa na nafasi muhimu katika matukio mbalimbali ya Mapinduzi ya Kiislamu hasa kipindi chote cha vita vya kujihami kutakatifu vya taifa la Iran dhidi ya uvamizi wa Iraq. Jeshi la Basiji bado linashiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii, kiutamaduni na kijeshi hapa nchini Iran.

Katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, Ustadh Mirkhani, mmoja wa waalimu hodari wa Sanaa ya hati na maandishi ya kuvutia wa Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali alijifunza Sanaa ya hati kwa walimu mahiri wa Iran katika fani hiyo. Kwa muda mfupi Mirkhani aliweza kufikia daraja ya ualimu katika Sanaa hiyo na kisha akaanza kufundisha. Ustadh Mirkhani alikuwa na kipaji maalumu katikak Sanaa ya hati huku akiwa stadi pia katika utunzi wa mashairi.