Jumapili, Disemba Mosi, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 4 Mfunguo Saba Rabiuth-Thani 1441 Hijria, inayosadifiana na tarehe Mosi Disemba 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1268 iliyopita, alizaliwa Sayyid Abdul Adhim al Hassani, mmoja wa wajukuu wa Imam Hassan al Mujtaba (a.s) huko katika mji wa Madina. Sayyid Abdul Adhim alikuwa mmoja kati ya shakhsiya walioaminiwa na Imam al Hadi (as) na alinukuu hadithi moja kwa moja kutoka kwa maimamu watukufu kama vile Ridha, Jawad na al Hadi (as). Sayyid Abdul Adhim alihamia Iran kutokana na pendekezo la Imam al Hadi (as) kwa ajili ya kuwaongoza Waislamu na akaishi katika mji wa Rei karibu na Tehran ya sasa. Sayyid Abdul Adhim aliuawa shahidi mwezi Shawwal mwaka 250 Hijria. Kaburi la mtukufu huyo liko katika eneo la Rei na ni miongoni mwa maeneo yanayotembelewa sana na Waislamu kutoka maeneo mbalimbali ya dunia.
Siku kama ya leo, miaka 928 iliyopita, alizaliwa mjini Baghdad Abubakr Muhammad Anbari, faqihi, mtaalamu wa hadithi na lugha. Anbari alipata kusoma elimu ya dini, nahwu na lugha akiwa kijana mdogo kutoka kwa baba yake. Baada ya kuhitimu masomo yake katika nyanja tofauti, alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi. Alitokea kuwa faqihi mkubwa na kutabahari katika elimu ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha ‘Manshurul-Fawaaid.’
Siku kama ya leo miaka 194 iliyopita, muungano wa kihistoria wa nchi za Ulaya uliojulikana kama Muungano Mtakatifu ulisambaratika baada ya kujiengua utawala wa Kikaisar (Tsarist) wa Russia katika muungano huo. Baada ya kuanguka kwa utawala wa Napoleon, muungano huo uliunda Congress ya Vienna, kati ya tawala za Russia, Austria na ufalme wa Pros na serikali hizo zikaafikiana kwamba nchi zilizo chini ya utawala wa muungano huo na katika uhusiano wa kimataifa zifuate misingi ya dini ya Kikristo.
Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 52 Sayyid Ali Muhammad Bin Sultan al-Ulama, maarufu kwa jina la 'Tajul-Ulama' mmojua mwa maulama wakubwa wa India. 'Tajul-Ulama alizaliwa mwaka 1262 Hijiria mjini Lucknow, kaskazini mwa India na kuanza kusoma masomo ya dini ya Kiislamu kutoka kwa baba yake na maulama wengine wa mji huo. Baadaye msomi huyo alitokea kuwa mtaalamu mkubwa katika elimu ya sheria za Kiislamu (fiqhi), theolojia na hadithi. Kadhalika alikuwa na uelewa mkubwa wa dini mbalimbali kiasi kwamba alikuwa akifanya mijadala na wananadharia wa dini tofauti. Ameacha athari mbalimbali kama vile kitabu cha 'Ahsanul-Qasas' kuhusiana na tafsiri ya Surat Yusuf (as) na kitabu cha 'Guhare Shab Cheragh.'
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita David Ben-Gurion mmoja wa waasisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Waziri Mkuu wa kwanza wa utawala huo ghasibu aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 87. Ben-Gurion alizaliwa tarehe 16 Oktoba 1886 katika mji wa Plonsk huko Uholanzi ambayo katika zama hizo ilikuwa sehemu ya ardhi ya ufalme wa Russia. Alielekea katika ardhi za Palestina mwaka 1906 akiwa na umri wa miaka 20 na kuasisisi harakati ya Kiyahudi. Mwaka 1907 aliasisi chama cha wafanyakazi wa Kizayuni ambacho taarifa yake ilikuwa inasema: "Malengo ya chama cha wafanyakazi wa Kizayuni ni kufanya juhudi za kujitegemea kisiasa kwa ajili ya Wayahudi katika ardhi hizi tukufu." Aidha katika Vita vya Kwanza vya Dunia David Ben-Gurion alikuwa na nafasi kubwa katika kuwahamisha taratibu Mayahudi kwenda ardhi za Palestina. Katika kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia harakati hiyo ilishika kasi chini ya uungaji mkono wa madola makubwa hususan Uingereza, kiasi kwamba mwaka 1948 Miladia sawa na tarehe 5 Mei na baada ya kupitishwa azimio na Umoja wa Mataifa la kuigawa Palestina katika pande mbili za Kiyahudi na Palestina, kulitangazwa rasmi kuanzishwa utawala haramu wa Kizayuni na wa kibaguzi wa Israel. Masaa machache baadaye, Marekani na Urusi ya zamani zikatangaza kuutambua utawala huo khabithi.
Na katika siku kama ya leo ya tarehe Mosi Disemba nchi mbalimbali duniani huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ukimwi. Kuweko Siku ya kimataifa ya Ukimwi kulifikiriwa kwa mara ya kwanza mwezi Agosti mwaka 1987 na James W. Bunn na Thomas Netter, maafisa wawili wa habari wa Kitengo cha Kimataifa cha Kupambana na Ukimwi cha Shirika la Afya Duniani (WHO) huko Geneva Uswisi. Maafisa hao wawili waliwasilisha wazo hilo kwa Dakta Jonathan Mann, Mkurugenzi wa Shirika la UNAIDS na baadaye akakubali pendekezo hilo, na kuliidhinisha. Na hatimaye akaafiki siku ya kwanza ya kimataifa ya Ukimwi iadhimishwe duniani kote tarehe Mosi Disemba mwaka 1988. Kuanzia wakati huo kila mwaka siku ya kimataifa ya Ukimwi huadhimishwa duniani kote tarehe Mosi Disemba.