Dec 03, 2019 21:10 UTC
  • Jumatano tarehe 4 Disemba 2019

Leo ni Juumatano tarehe 7 Rabiuthani 1441 hijria saw ana Disemba 4 mwaka 2019

Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita jeshi la Iran lilitangaza kwamba limefanikiwa kuidhibiti ndege ya kijasusi isiyokuwa na rubani (drone) ya Marekani aina ya RQ-170. Ndege hiyo iliyoingia katika anga ya mashariki mwa Iran kutokea Afghanistan, ilitumbukia katika mtego wa kikosi cha vita vya elektroniki cha Iran na kushushwa chini ikiwa nzima. Ndege hiyo ya RQ-170 ni miongoni mwa drone za kisasa kabisa za jeshi la Marekani na inatumiwa na shirika la ujasusi la nchi hiyo CIA kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufanya ujasusi. Baada ya kudhibitiwa na jeshi la Iran wataalamu wa Jamhuri ya Kiislamu walichunguza na kuvumbua namba za siri za ndege hiyo ya kijasusi ya Marekani na kupata ripoti muhimu za kipelelezi na teknolojia ya utengenezaji wake. Miaka mitatu baada ya ndege hiyo kushikwa na jeshi la Iran, wataalamu hapa nchini wamefanikiwa kuzalisha na kutengeneza ndege hiyo ya kisasa kabisa na kijasusi.

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, mkutano wa kwanza wa Kiislamu kuhusiana na Palestina ulifanyika hapa mjini Tehran. Mkutano huo ulifanyika katika fremu ya mfungamano wa walimwengu na mapambano ya Intifadha ya Palestina na kukabiliana na wimbi la kuhajiri Mayahudi kuelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa kuchunguza chanzo cha mapambano ya Intifadha ya wananchi Waislamu wa Palestina, Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi hao pamoja na taathira ya matukio ya Mashariki ya Kati kwa taifa la Palestina.

Miaka 67 iliyopita katika siku kama ya leo, mkutano wa pande tatu yaani Marekani, Uingereza na Ufaransa ulifanyika katika kisiwa cha Bermuda kaskazini mwa Amerika Kusini. Mbali na nchi hizo tatu kujadili uhusiano baina yao, zilichukua maamuzi muhimu na kuratibu namna ya kukabiliana na siasa za Shirikisho la Umoja wa Sovieti huko Berlin. Katika zama hizo sehemu ya magharibi ya mji wa Berlin, Ujerumani ilikuwa chini ya udhibiti wa Marekani, Uingereza na Ufaransa na sehemu ya mashariki ilikuwa chini ya udhibiti wa Umoja wa Sovieti. Kupamba moto hitilafu za namna ya kuuendesha mji huo, ndiko kulikopelekea kujengwa ukuta maarufu wa Berlin mnamo mwaka 1961.

Ujenzi wa ukuta wa Berlin

Na miaka 120 iliyopita, kwa mara ya kwanza chanjo ya homa ya matumbo au Typhoid ilitumiwa kwa mwanadamu ili kukabiliana na maradhi hayo ambayo husababisha kuhara damu. Awali chanjo hiyo ilivumbuliwa na mtafiti mmoja wa Kifaransa na baadaye ilikamilishwa na tabibu wa Kiingereza kwa jina la Almroth Edward Wright.