Dec 05, 2019 23:16 UTC
  • Ijumaa, Disemba 6, 2019

Leo ni Ijumaa tarehe 9 Mfunguo Saba Rabiuthani 1441 Hijria sawa na Disemba 6 mwaka 2019 Milaadia.

Miaka 23 iliyopita katika siku kama ya leo, mtayarishaji filamu mashuhuri wa Iran, Ali Hatami aliaga dunia. Baada ya kuhitimu masomo katika Chuo cha Sanaa hapa nchini, Hatami alijiunga na televisheni ya taifa na kujishughulisha na masuala ya filamu. Filamu zake nyingi ziliakisi mapenzi yake kwa utamaduni wa Iran. Miongoni mwa filamu hizo ni Sattarkhan, Sutedelan, Kamalul Mulk na Maadar.

Ali Hatami

Tarehe 6 Disemba miaka 27 iliyopita, Wahindu wenye misimamo mikali waliubomoa Msikiti wa Babri katika mji wa Faizabad kwenye jimbo la Uttar Pradesh nchini India. Msikiti huo ulijengwa mwaka 1528 na Zahiruddin Muhammad Babur juu ya kilima na tangu wakati huo ulijulikana kwa jina la Msikiti wa Babri. Baada ya kupita karne tatu tangu ujengwe yaani mwaka 1855, mtawala mmoja Muingereza alipotosha ukweli kwa makusudi na kuandika kuwa msikiti huo umejengwa kwenye magofu ya jumba la ibada ya masanamu la Wahindu. Suala hilo lilikuwa chanzo cha fitina na ugomvi mkubwa kati ya Waislamu na Wahindu. Mwaka 1992 Wahindu wenye misimamo ya kufurutu mipaka walivamia Msikiti wa Babri na kuubomoa kikamilifu, suala ambalo lilizusha vita baina ya Waislamu na Wahindu.

Msikiti wa Babri

Miaka 39 iliyopita katika siku kama hii ya leo alikufa shahidi rubani Ahmad Keshvari. Brigedia Ahmad Keshvari aliingia katika Jeshi la Anga la Iran mwaka 1351 Hijria Shamsia na kuhitimu mafunzo ya kuendesha helikopta. Baada ya ushindi wa Mapindizi ya Kiislamu nchini mwaka 1979 alitoa mchango mkubwa katika kupambana na makundi yaliyokuwa dhidi ya Mapinduzi katika maeneo ya magharibi mwa Iran na baadaye kidogo aliteuliwa kuwa kamanda wa Jeshi la Anga katika eneo la Ilam. Baada ya jeshi la Saddam Hussein kuvamia ardhi ya Iran, Brigedia Keshvari alikuwa mstari wa mbele kupambana na jeshi la adui na kulisababishia hasara kubwa ya nafsi na mali. Ahmad Keshvari aliuawa shahidi baada ya kukamilisha operesheni iliyokuwa na mafanikio akiwa njiani kurejea nchini.

Ahmad Keshvari

Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Manouchehr Jahan Beglu, profesa wa miziki ya kiasili ya Kiirani akiwa na umri wa mia 62. Profesa Jahan Beglu alizaliwa mwaka 1307 Hijria Shamsia Mwanamuziki huyo wa miziki ya kiasili alijifunza sanaa ya muziki kutoka kwa wasomi wakubwa wa tasnia hiyo na kisha akaelekea Austria na kupata shahada ya juu zaidi katika fani hiyo. Alirudi nchini na kuwasaidia wanafunzi wengi kufanya utafiti na kukuza tasnia hiyo.

Manouchehr Jahan Beglu

Miaka 102 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Finland iliyokuwa chini ya utawala wa Russia ilijipatia uhuru wake. Kuwa jirani Finland na Russia kuliwatia wasi wasi mno viongozi wa Finland, kiasi kwamba, katika karne ya 12 Miladia, waliiomba Sweden iwahami dhidi ya Moscow. Hata hivyo, Wasweden wakaikalia kwa mabavu Finland. Mwaka 1721 Russia iliivamia Finland na kudhibiti sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1917 vikosi vamizi vya Russia vililazimika kuondoka nchini Finland na nchi hiyo ikajitangazia uhuru.

Bendera ya Finland

Na siku kama ya leo miaka 241 iliyopita yaani tarehe 6 Disemba mwaka 1778, alizaliwa Joseph Louis Gay-Lussac mwanafizikia na mwanakemia wa Ufaransa. Gay-Lussac alifanya tafiti nyingi na kugundua vitu mbalimbali katika kipindi cha maisha yake. Miongoni mwa mambo yaliyogunduliwa na mwanakemia huyo ni gesi ya sumu ya halogen, kipimio cha ulevi, hydromita au chombo cha kupimia uzito wa maji na viowevu na kuitambua Chloride na Iodine kama elementi mpya. Miongoni mwa kazi zake muhimu za kisayansi alizofanya mwanakemia huyo ni kuweka kanuni ya kupanuka kwa gesi. Kanuni hiyo iliyopewa jina lake pamoja na la mshirika wake ilijulikana kama Law of Charles and Lussac. Gay-Lussac alifariki dunia mwaka 1850.

Joseph Louis Gay-Lussac