Dec 06, 2019 23:20 UTC
  • Jumamosi, 7 Disemba, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 10 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1441 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 7 Desemba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1240 iliyopita, alifariki dunia Bibi Fatima Maasuma A.S, binti wa Imam Mussa bin Jaafar al-Kadhim (as). Bibi Fatima Maasuma alizaliwa mwaka 173 Hijria katika mji wa Madina. Alikuwa mwanamke mwenye fasaha katika uzungumzaji, alimu, hodari na zahidi na mcha- Mungu. Mwaka mmoja baada ya kaka yake yaani Imam Ali bin Mussa Ridha (as) kuwasili Khorasan nchini Iran, Bibi Maasuma aliondoka Madina kwa lengo la kumfuata kaka yake, lakini akiwa njiani alisimama katika mji wa Qum na kufariki dunia mjini humo kutokana na maradhi au kwa mujibu wa kauli nyingine, kutokana na sumu aliyopewa. ***

      السلام علیک یا فاطمه المعصومه

 

Miaka 130  iliyopita gari la kwanza la kisasa duniani lilitengenezwa. Gari hilo lililokuwa na uwezo wa kutembea kilomita 12 kwa saa lilitengenezwa na msomi wa Kijerumani aliyejulikana kwa jina la Karl Friedrich Benz. Gari hilo lilitumia nishati ya petroli au alkoholi. Karl Benz alifariki dunia mwaka 1929. ***

Karl Friedrich Benz

 

Katika siku kama ya leo miaka 111 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Haram tukufu ya Imam Ali bin Mussa Ridha, mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Mash'had huko kaskazini mwa Iran ilishambuliwa kwa mizinga na wavamizi wa Kirusi. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Mmarekani, Morgan Shuster kuanzisha kikosi maalumu cha polisi ya Hazina Kuu ya Iran. Urusi iliitambua hatua hiyo kuwa ni kinyume na maslahi yake haramu nchini. Mashambulizi hayo yalisababisha hasara kubwa kwa haramu ya mjukuu huyo wa Mtume (saw) na mali za thamani za eneo hilo tukufu ziliporwa na wavamizi hao. ***

 

Siku kama ya leo mika 78 iliyopita, wakati Vita vya Pili vya Dunia vilipokuwa vimeshadidi barani Ulaya, ndege mia mbili za kivita za Japan zilishambulia kituo cha jeshi la Marekani katika bandari ya Pearl (Pearl Harbor). Shambulizi hilo lilifanyika wakati Japan ilipokuwa katika mazungumzo na Marekani kuhusu masuala ya mashariki mwa Asia. Sambamba na mashambulizi hayo ambayo yaliharibu meli 19 za kivita za Marekani, jeshi la Japan pia lilifanya mashambulizi makubwa katika nchi za kusini mwa Asia. Baada ya mashambulizi hayo Marekani ilitangaza vita dhidi ya Japan na Vita vya Pili vya Dunia vikapanuka zaidi hadi mashariki mwa Asia. ***

 

Miaka 66 iliyopita katika siku kama ya leo ya  inayosadifiana na 16 Azar 1332 Hijria Shamsia, upinzani wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tehran dhidi ya safari ya Richard Nixon, Makamu wa Rais wa Marekani katika kipindi hicho hapa nchini, ulipelekea wanachuo watatu kuuawa na askari vibaraka wa utawala dhalimu wa Shah. Safari hiyo ilifanyika miezi mitatu na nusu tu baada ya mapinduzi ya Marekani dhidi ya serikali ya Dakta Musaddiq. Siku ya pili baada ya mauaji hayo, Richard Nixon alitunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu wa sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran. Kwa mnasaba huo, tarehe 16 Azar kila mwaka huadhimishwa nchini Iran kama "Siku ya Mwanachuo". ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, Abdul-Wahhab Kayyali mmoja wa wanamapambano wa Palestina aliuawa na magaidi wa Kizayuni mjini Beirut, Lebanon. Aliingia katika masuala ya kisiasa akiwa mwanafunzi na risala yake ya shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha London pia ilihusu masuala ya Palestina na mapambano ya Waarabu dhidi ya ukoloni na Uzayuni. ***

Abdul -Wahhab Kayyali