Dec 08, 2019 01:18 UTC
  • Jumapili 8 Disemba

Leo ni Jumapili tarehe 11 Mfunguo Saba, Rabiuth-Thani 1441 Hijria, mwafaka na tarehe 8 Disemba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1221 iliyopita, alifariki dunia Abu Ali Khayyat, mnajimu na mtaalamu wa hesabati wa Kiislamu. Abu Ali ni alikuwa na nafasi kubwa wakati wake huku jina lake likiwekwa mstari wa mbele katika kitabu cha majina ya wasomi wakubwa na mashuhuri wa dunia. Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha 'Mawaalid' na 'Siyarul-A'amaal.' Vitabu vingi vya Abu Ali Khayyat vimetarjumiwa kwa lugha ya Kilatini.

Abu Ali Khayyat

Siku kama ya leo miaka 833 iliyopita, alizawa mjini Mosul, moja ya miji mashuhuri ya Iraq ya leo, Ebn-e Xallakan (Ibn Khalkan), kadhi, mwanahistoria na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu. Akiwa kijana alisoma elimu za awali katika mji alikozaliwa na kisha kufanya safari mbalimbali na kukutana na wanasheria wa Kiislamu na wanahistoria wakubwa sanjari na kustafidi na elimu kutoka kwao. Kwa muda mrefu Ebn-e Xallakan alikuwa kadhi mjini Damascus Syria,  huku akiwa mtaalamu pia katika elimu za historia, fasihi ya Kiarabu na mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwezi wa Rajab mwaka 681 Hijiria baada ya kuugua na kuzikwa chini ya mlima Qasioun ulio Damascus ambako pia wamezikwa wasomi wengi.

Ebn-e Xallakan (Ibn Khalkan), kadhi, mwanahistoria na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 151 iliyopita, yaani tarehe 8 Disemba 1868 Miladia ulianguka utawala wa Washugani au kwa jina jingine watawala wa kijeshi huko Japan. Kuanguka kwa utawala huo kulipelekea kuanza marekebisho ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni nchini humo. Washugani walikuwa moja kati ya makumi ya silsila zenye nguvu huko Japan, walioanzisha utawala wao wa kidikteta tangu karne ya 12 Miladia. Kwa kutegemea uwezo na upenyaji wao, Washugan walizuia serikali ya Japan kuwa na mahusiano na nchi nyingine. Hata hivyo mwaka mmoja baadaye na baada ya kuingia madarakani mfalme mwenye nguvu wa Japan Mutsuhito, mwaka 1867 utawala wa Washugan ukaanguka.

Mutsuhito

Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, alifariki dunia Herbert Spencer mwanafikra na mwanafilosofia wa Kiingereza. Spencer alizaliwa mwaka 1820 Miladia na kujifunza elimu mbalimbali kutoka kwa baba yake. Aidha alijiongezea ujuzi wa kielimu kutokana na juhudi zake za kupenda kutalii mambo. Herbert Spencer aliamini kuwa, mtu anaweza kujipatia elimu kwa kushuhudia na kupata uzoefu. Aidha msomi huyo alisisitizia sana juu ya udharura wa tabia njema, uadilifu na urafiki. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu cha 'Misingi ya Saikolojia' 'Misingi ya Elimu ya Kijamii' chenye juzuu tatu na 'Misingi ya Utambuzi wa Tabianchi.'

Herbert Spencer mwanafikra na mwanafilosofia wa Uingereza.

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, yalijiri mapigano ya baharini ya Falklands pambizoni mwa visiwa vya Falklands katika Bahari ya Atlantiki kati ya Uingereza na Ujerumani. Vikosi vya wanamaji vya Ujerumani vilipigwa vibaya na vile vya Uingereza na kupelekea visiwa hivyo kwa mara nyingine tena kuwa chini ya himaya ya Waingereza. Ni vyema kuashiria kuwa, visiwa vya Falklands viligunduliwa mwishoni mwa karne ya 16 Miladia na kukaliwa na jeshi la Ufaransa mwaka 1764 Miladia. Hata hivyo baadaye vilifahamika kuwa na utajiri wa mafuta, na hivyo kukodolewa macho na Uingereza ambapo hatimaye London ilituma jeshi lake na kuvikalia kwa mabavu visiwa hivyo. Visiwa hivyo vya Falklands au kwa jina lingine 'Malvinas' vipo katika Bahari ya Atlantiki na kusini mashariki mwa nchi ya Argentina.

Ramani ya visiwa vya Falklands

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, Chian Kai-shek kiongozi wa wapigania uhuru wa China alikimbilia Taiwan akiwa na wafuasi wake wengi baada ya kushindwa na wapiganaji wa chama cha Kikomonisti chini ya uongozi wa Mao Tse Tung na kuunda serikali ya kitaifa ya Uchina. Uungaji mkono wa Marekani kwa kiongozi huyo wakati huo ulipelekea Taiwan kujitenga na Uchina na kiti cha nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kikapatiwa Taiwan. Hata hivyo mwaka 1971 Miladia na kufuatia kujiri mazungumzo kati ya China na Marekani, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililipigia wingi wa kura, suala la kutambuliwa rasmi Jamhuri ya Watu wa China sambamba na kuwa mmoja wa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la umoja huo. Kwa msingi huo Taiwan ikawa imevuliwa uanachama katika jumuiya hiyo kubwa zaidi ya kimataifa.

Chian Kai-shek kiongozi wa wapigania uhuru wa China aliyekimbilia Taiwan

Na siku kama ya leo miaka 19  iliyopita sawa na tarehe 17 Azar 1378 Hijria Shamsia aliaga dunia Husseini Makki mwanasiasa, mwanahistoria na mwandishi wa zama hizi wa Iran. Hussein Makki alizaliwa mwaka 1290 Hijria Shamsia. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi alielekea katika mji wa Tehran na kuanza kufanya kazi serikalini. Baada ya kupatikana anga ya wazi ya kisiasa mwaka 1320 Hijria Shamsia alianza rasmi harakati zake katika magazeti. Maandishi ya Husseini Makki ya kihistoria, kiutafiti na kifasihi yalikuwa sehemu muhimu ya makala katika magezeti mashuhuri ya Tehran zama hizo. Kujiunga kwake na Chama cha Iran na Chama cha Demokrasi cha Iran ndio uliokuwa mwanzo wa safari yake ya kuelekea katika harakati za kisiasa ambapo aliwahi kushika wadhifa wa Bunge katika duru tatu mtawalia.

Husseini Makki mwanasiasa, mwanahistoria na mwandishi wa zama hizi wa Iran