Jumatano tarehe 11 Disemba 2019
Leo ni Jumatano tarehe 14 Rabiuthani 1441 Hijria sawa na 11 Disemba 2019.
Siku kama ya leo miaka 1375 iliyopita Mukhtar bin Abi Ubaida al Thaqafi alianza mapambano ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein bin Ali AS, mjukuu wa Mtume Muhammad SAW. Mwaka 61 Hijria Imam Hussein AS akiwa pamoja na wafuasi na watu wa familia yake, aliuawa shahidi na jeshi la Yazid akiwa katika harakati za kuilinda dini tukufu ya Uislamu. Mukhtar alianzisha harakati zake za mapambano katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la 'Tawwabiin' ambalo lilipigana na utawala wa Bani Umayyah, kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS. Mukhtar Thaqafi alitawala Kufa kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja na mwishowe alishindwa na jeshi la Mus'ab bin Zubair na kuuawa shahidi.

Katika siku kama ya leo miaka 209 iliyopita Alfred Louis Charles de Musset-Pathay malenga na mwandishi mwashuhuri wa Ufaransa alizaliwa katika familia ya wasomi mjini Paris, Ufaransa. Musset aliandika diwani yake ya kwanza ya mashairi kwa jina la Simulizi za Uhispania na Italia akiwa na umri wa miaka 19 na hivyo kupata umashuhuri mkubwa kutokana na mbinu yake mpya ya uandishi. Akiwa na umri wa miaka 22 aliandika tamthilia yake ya kwanza iliyoibua utata kutokana na masuala ya kiroho na kimaadili. Fikra zake huru zilimfa awe miongoni mwa waandishi waatajika katika nusu ya kwanza ya karen ya 19. Alfred de Musset aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 47 mwaka hapo mwaka 1857.

Tarehe 11 Disemba miaka 176 iliyopita alizaliwa daktari na mtaalamu wa vividudu maradhi wa Kijerumani aliyevumbua ugonjwa wa kifua kikuu, Robert Koch. Baada ya kukamilisha masomo katika taaluma ya tiba, Robert Koch alijishughulisha na kutibu wagonjwa katika miji mbalimbali ya Ujerumani sambamba na kufanya uhakiki kuhusu maradhi tofauti. Tarehe 24 Machi mwaka 1882 alifanikiwa kuvumbua ugonjwa wa kifua kikuu (TB). Katika safari zake nyingi barani Afrika, tabibu huyo wa Kijerumani pia alibaini kuwa ugonjwa wa malale uliokuwa ukisababisha vifo vya Waafrika wengi ulikuwa ukisababishwa na mdudu anayeitwa mbung'o.

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) uliasisiwa baada ya kupasishwa suala hilo kwa wingi wa kura. Kwa utaratibu huo, taasisi hiyo ikaanza rasmi shughuli zake chini ya Baraza la Masuala ya Kijamii la Umoja wa Mataifa. Awali Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), ulikuwa na jukumu la kuwahudumia watoto waliojeruhiwa katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Hata hivyo baadaye asasi hiyo muhimu ikapanua zaidi shughuli zake na kuanza kuandaa mahitaji ya kimsingi maishani kama chakula, elimu na malezi kwa watoto waliokosa haki hizo za kimsingi. Makao makuu ya UNICEF yapo mjini New York, Marekani.

Na miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, aliuawa shahidi Ayatullah Sayyid Abdulhussein Dastgheib, alimu mkubwa na mwalimu wa akhlaq wa Kiislamu. Ayatullah Dastgheib aliuawa shahidi na kundi la munafiqin alipokuwa akielekea kwenye Swala ya Ijumaa. Alizaliwa katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran na alipata elimu yake ya kidini hadi daraja ya ijtihadi katika chuo cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Dastgheib pia alishirikiana na maulamaa wengine waliokuwa na mwamko na wanaharakati wa Iran katika kufundisha elimu ya Kiislamu, kupambana na utawala wa Shah na mara kadhaa alikamatwa na kufungwa jela. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni "Madhambi Makubwa", "Maad" pamoja na tafsiri ya sura kadhaa za Qur'ani Tukufu.'

Tarehe 11 Disemba mwaka 1958 Burkina Faso ilitangazwa kuwa Jamhuri. Tangu mwanzoni mwa karne ya 19 nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala na ukoloni wa Ufaransa. Burkina Faso ambayo hapo kabla ilikuwa ikiitwa Upper Volta, mnamo mwaka 1958 ilijitangazia utawala wa ndani wa jamhuri. Hata hivyo iliendelea kuwa sehemu ya Ufaransa. Miaka miwili baadaye yaani tarehe 5 Agosti 1960, Burkina Faso ilijipatia uhuru kamili sambamba na kukubaliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Mwaka 1984 jina la nchi hiyo lilibadilishwa rasmi kutoka Upper Volta na kuitwa Burkina Faso. Nchi ya Burkina Faso ina ukubwa wa karibu kilomita mraba 274,000 na inapatikana Magharibi mwa Afrika ikipakana na nchi za Mali, Ivory Coast, Ghana, Togo, Benin na Niger.
