Dec 13, 2019 23:30 UTC
  • Jumamosi, Disemba 14, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 17 Mfunguo Saba Rabiuthani 1441 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 14 Disemba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 214 iliyopita, sawa na 14 Disemba 1805, iligunduliwa nishati ya joto ya makaa ya mawe na George Branclon, mhunzi kutoka Uingereza. Kabla ya hapo, makaa ya mawe yalikuwa yakitumiwa kama mojawapo ya vifaa vya kujengea nyumba. Shehena ya kwanza ya madini ya makaa ya mawe yaliyotumiwa katika nishati ya joto, ilipatikana katika bandari Plymouth nchini Uingereza. ***

Makaa ya mawe

 

Katika siku kama ya leo ya tarehe 23 Azar miaka 116 iliyopita, Daktari Mahmoud Najmabadi, mmoja wa matabibu na wahakiki mahiri wa Iran alizaliwa. Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi, Najmabadi alijiunga na shule ya tiba na kufanikiwa kuhitimu. Daktari Najmabadi mbali na kutibu wagonjwa alikuwa akifundisha Chuo Kikuu na alikuwa na mapenzi makubwa na tiba ya Kiislamu-Kiirani. Ni kwa msingi huo ndio maana akatarjumu vitabu kadhaa vya kuwatambulisha matabibu wa Kiirani ambao ni mashuhuri katika Ulimwengu wa Kiislamu kama Zakaria Razi na wengineo. Baadhi ya vitabu vyake ni: Mukhtasari ya Tiba ya Kiislamu, Historia ya Tiba ya Iran na MuhammadZakaria Razi; Tabibu, Mwanafalsafa na Mkemia wa Kiirani. ***

Daktari Mahmoud Najmabadi

 

Miaka 108 iliyopita katika siku kama ya leo, baada ya juhudi na jitihada za miaka mingi, hatimaye Ncha ya Kusini yaani South Pole ilivumbuliwa na kwa mara ya kwanza na wavumbuzi kadhaa waliwasili katika eneo hilo. Katika siku hii, Roald Amundsen baharia mashuhuri wa Kinorway aliyekuwa akishindana na Robert Falcon Scott wa Uingereza ili kuifikia ncha hiyo ya kusini, aliibuka mshindi na kuitundika bendera ya Norway katika ncha hiyo. Robert Falcon Scott akiwa na wenzake walikumbana na theluji kali wakati wanarejea na kupoteza maisha yao. ***

Roald Amundsen

 

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia msomi mkubwa wa hadithi Mullah Muhammad Nakhjawani. Mullah Nakhjawani alibobea sana katika elimu za fiqhi na hadithi na lifuatwa zaidi na Waislamu wa eneo la Kaukazia. Ayatullah Nakhjawani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 66 katika mji mtakatifu wa Karbala na kuzikwa katika Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika mji wa Najaf. Msomi huyo ameandika vitabu kadhaa. ***

Mullah Muhammad Nakhjawani.

 

Miaka 87 iliyopita sawa na siku kama ya leo ya tarehe 23 Azar aliaga dunia Ayatullah Abdallah Mamqani msomi na mwanazuoni mkubwa aliyekuwa amebobea katika elimu ya fikihi. Abdallah Mamqani alizaliwa mwaka 1252 katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq katika familia ya elimu. Baba yake ambaye ni Ayatullah Muhammad Hassan Mamqani alikuwa mmoja wa Maulamaa na wanazuoni wakubwa na watajika katika zama zake. Bidii kubwa ya masomo aliyokuwa nayo Abdallah Mamqani pamoja na kipaji kikubwa cha masomo vilimfanya akwee kwa haraka daraja za kielimu na kuondokea kuwa mmoja wa Marajii Taklidi muhimu wa Kishia katika zama zake. Mwanazuoni huyo hakuwa nyuma pia katika uandishi wa vitabu. Baadhi ya vitabu vyake mashuhuri ni Miqyas al-Hidayah Fi Elm al-Dirayah, Manasik Hajj na al-Qaid al-Tibiyah. ***

Ayatullah Abdallah Mamqani

 

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Disemba 1981 Bunge la utawala haramu wa Israel 'Knesset' liliiunganisha rasmi miinuko ya Golan ya huko Syria na ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu. Hatua hiyo ilikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa nchi za Kiislamu, Kiarabu pamoja na jamii ya kimataifa. Utawala dhalimu wa Israel uliikalia kwa mabavu miinuko hiyo ya Golan ya Syria katika vita baina yake na Waarabu mwaka 1967. ***

Bunge la utawala haramu wa Israel 'Knesset'

 

Na siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, makubaliano ya amani ya Bosnia yaliyojulikana kwa jina la "Dayton Peace Agreement" yaani Makubaliano ya Amani ya Dayton" yalithibitishwa kwa mara ya mwisho katika kikao kilichofanyika mjini Paris, Ufaransa. Makubaliano hayo ambayo yalifanyika kwa mashinikizo ya viongozi wa Marekani tarehe 21 Novemba 1995, yalitiwa saini na Marais wa wakati huo wa Bosnia Herzegovina, Serbia na Croatia. Mafanikio pekee ya makubaliano hayo kwa upande wa Waislamu, yalikuwa ni kuhitimishwa mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa dhidi yao na  Waserbia. ***

Utiaji saini wa makubaliano ya "Dayton Peace Agreement"