Alkhamisi tarehe 19 Disemba 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 22 rabiuthani 1441 hujria sawa na Disemba 219 mwaka 2019
Katika siku kama ya leo miaka 232 iliyopita mwafaka na tarehe 19 Disemba 1787, nchi ya Kiafrika ya Sierra Leone iliunganishwa na Uingereza, baada ya kupita miaka 327 tangu ardhi ya nchi hiyo igunduliwe na wazungu. Sierra Leone iligunduliwa na mtalii wa Uhispania na kukoloniwa. Katika miaka ya kukoloniwa kwake na Uhispania, maelfu ya wanaume na wanawake wa Sierra Leone walichukuliwa watumwa na kwenda kuuzwa katika masoko ya Ulaya. Mwenendo huo uliendelea pia baada ya Waingereza kuishinda Uhispania na kuanza ukoloni wa Uingereza nchini humo. Mwaka 1961 Sierra Leone ilianza kujitawala na kuwa na utawala unaosimamiwa na jeshi na mwaka 1971 ikawa na utawala wa Jamhuri.
Siku kama ya leo miaka 179 iliyopita alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Seikh Muhammad Taqi Razi katika mji wa Isfahan nchini Iran. Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku. Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid".

Siku kama hii ya leo miaka 113 iliyopita alizaliwa kiongozi wa Urusi ya zamani, Leonid Brezhnev katika familia maskini nchini Ukraine. Mwaka 1931, Brezhnev alijiunga na kuwa mwanachama wa chama hicho cha Kikomonisti. Brezhnev alitwaa uwaziri mkuu Russia na uongozi wa Chama cha Kikomonisti cha Urusi ya zamani mwaka 1964 wakati Nikita Khrushchev alipokuwa sfarini nje ya nchi. Mashambulizi dhidi ya Czechoslovakia na kukaliwa kijeshi Afghanistan yalifanyika katika zama zake.
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, inayosadifiana na 19 Disemba 1972, kiongozi wa wakati huo wa Uganda Jenerali Idi Amin Dada aliwapatia wafanyakazi wa Kiingereza waliokuwa wakifanya kazi nchini humo makataa ya siku 12 wakubali kupunguziwa mishahara yao kwa asilimia 40 au waondoke nchini humo. Zoezi hilo liliwajumuisha karibu wafanyakazi 780 wa Kiingereza waliokuwa wakifanya kazi kwenye mashirika mbalimbali nchini Uganda.
Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo, Sadeq Ganji mwambata wa Kituo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Lahore Pakistan alishambuliwa kwa risasi na vibaraka wa ubeberu wa kimataifa na kuuawa shahidi. Kwa karibu miaka minne Ganji alikuwa akitekeleza jukumu lake la kutangaza na kuziarifisha thamani aali za Kiislamu na kupanua uhusiano wa kiutamaduni baina ya wananchi wa Iran na Pakistan. Sadeq Ganjia aliuawa shahidi akiwa amekaribia kurejea hapa nchini baada ya hafla ya kumuaga iliyoandaliwa na wana utamaduni na shakhsia wa kielimu na kifasihi wa Lahore Pakistan.