Dec 27, 2019 20:56 UTC
  • Jumamosi, 28 Disemba,2019

Leo ni Jumamosi tarehe Mosi Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1441 Hijria mwafaka na tarehe 28 Disemba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 230 iliyopita yaani tarehe Mosi Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1211,  alifariki dunia mshairi mkubwa wa Kiislamu Sheikh Kadhim Tamimi Baghdadi, maarufu kwa jina la Uzri akiwa na umri wa miaka 80. Alikuwa msomi na mwanafasihi mkubwa na ameacha diwani ya mashairi. Miongoni mwa mashairi ya malenga huyu maarufu wa Kiislamu ni shairi maarufu la "Al Uzriya" ambalo linamsifu Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kizazi chake kitukufu na kubainisha misingi ya dini ya Uislamu. Shairi hilo lina zaidi ya beti 1000. ***

Sheikh Kadhim Tamimi Baghdadi

 

Katika siku kama ya leo miaka 245 iliyopita yaani mwaka 1774, Joseph Priestley, mwanakemia na mwanafizikia wa Uingereza alifanikiwa kugundua gesi ya oksijeni. Msomi huyo aliishi katika kipindi kilichokuwa maarufu kama zama za dhahabu za kemia. Gesi ya oksijeni ina mchango na nafasi muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu na viumbe vingine hai na huingia katika mwili wa mwanadamu wakati wa kupumua na kuchanganyika na chakula. Matokeo ya kazi hiyo ni kuzalishwa nishati ambayo hutumika katika kubakia hai mwanadamu. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.***

Joseph Priestley,

 

Miaka 132 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Ayatullah Mirza Muhammad Hassan Husseini Shirazi alitoa fatuwa maarufu ya kuharamisha tumbaku ili kuzuia uporaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni wa Kiingereza katika nchi za Kiislamu. Fatuwa hiyo ilitolewa baada ya mfalme Nasiruddin Shah wa Iran kutia saini mkataba wa kuipa kampuni moja ya utawala wa kikoloni wa Uingereza mamlaka ya kuuza na kununua tumbaku ya Iran kwa kipindi cha miaka 50. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa hiyo ya kuharamisha tumbaku. Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fatua hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni. ***

Mirza Muhammad Hassan Shirazi

 

Siku kama ya leo miaka 124 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Disemba 1895, kwa mara ya kwanza katika historia ya sanaa ya filamu, filamu ya kwanza ya kisa ilioneshwa kwenye mkusanyiko wa watu wengi. Filamu hiyo ilitayarishwa na kuandaliwa na ndugu wawili waliojulikana kwa majina ya Auguste na Louis Lumiere. Miaka iliyofuata ilitengenezwa mitambo bora zaidi ya kurekodi na kuonesha filamu na hatua kwa hatua filamu zenye ubora wa juu na za aina mbalimbali zikaanza kuonyeshwa katika nchi mbalimbali duniani. ***

Ndugu wawili Auguste na Louis Lumiere

 

Miaka 94 iliyopita,  inayosadifiana na tarehe 28 Disemba 1925 alizaliwa Apollo Milton Obote Rais wa zamani wa Uganda. Obote aliiongoza Uganda kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza mwaka 1962. Aliiongoza Uganda akiwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1962 hadi 1966. Milton Obote alikuwa Rais wa Uganda kuanzia mwaka 1966 hadi 1971 alpoondolewa madarakani na Idi Amin Dada. Hata hivyo mwaka 1980 alirejea madarakani baada ya Idi Amin kuondolewa uongozini na kuiongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 wakati alipoondolewa madarakani na kulazimika kukimbilia Tanzania na baadaye Zambia. Obote alifariki dunia mwaka 2005 huko Johannesburg, Afrika Kusini kutokana na matatizo ya figo***

Apollo Milton Obote Rais wa zamani wa Uganda

 

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita inayosadifiana na tarehe 7 Dei 1353 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Ayatullah Hussein Ghaffari mmoja wa wanazuoni na mwanamapambano wa Kiislamu. Ayatullah Ghaffari aliuawa shahidi akiwa katika jela ya utawala wa wakati huo wa Kifalme hapa Iran. Ayatullah Ghaffari aliendesha harakati za kupambana na utawala wa kidikteta wa Mfalme Shah kwa kuandika vitabu na majarida mbalimbali. Baadaye alitiwa mbaroni na kutiwa jela na kufa shahidi katika siku kama ya leo, baada ya kuvumilia mateso mengi gerezani humo. ***

Ayatullah Hussein Ghaffari

 

Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 7 Dei mwaka 1357, wananchi wa mji wa Qazwin Iran walifanya maandamano makubwa wakitangaza upinzani wao dhidi ya utawala wa kifalme wa Shah. Maandamano hayo yalifanyika sambamba na kushika kasi mapinduzi ya wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa kidikteta wa Kipahlavi. Vyombo vya usalama vya utawala wa Shah viliyakandamiza maandamano hayo na kupelekea umwagaji damu mkubwa ambapo watu 20 waliuawa shahidi. ***

Maandamano ya wananchi wa Qazwin

 

Na miaka 40 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Dey mwaka 1358 Hijria Shamsia, Imam Khomeini (MA)  mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alitoa amri ya kuanzishwa harakati ya kupambana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika. Imam Khomeini alitoa amri kwa wananchi wote wa Iran kushirikiana bega kwa bega kwa shabaha ya kumtokomeza adui ujinga. Hivi sasa kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika nchini Iran kimeongezeka sana, na kufikia hatua kwa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO kuiweka Iran kwenye kundi la nchi zenye idadi kubwa ya watu wanaojua kusoma na kuandika. ***

Harakati ya kupambana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika.