Dec 28, 2019 23:21 UTC
  • Jumapili, Disemba 29, 2019

Leo ni Jumapili tarehe Pili Mfungo Nane Jamadul-Awwal 1441 Hijria, mwafaka na tarehe 29 Desemba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1050 iliyopita alifariki dunia Abu Is'haq Kisai Marvazi, malenga mashuhuri wa Iran. Marvazi alizaliwa mwaka 341 Hijiria mjini Marv, moja ya miji ya zamani ya Iran ambao hii leo unapatikana nchini Turkmenistan. Kipindi cha ujana wake kilienda sambamba kumalizika kwa utawala wa Samanid na kuanza utawala wa Ghaznavid. Ni kwa ajili hiyo ndio maana beti zake za mashairi zilihusu tawala hizo mbili. Aidha Abu Is'haq Kisai Marvazi alijulikana kwa kuwasifu sana katika mashairi yake Ahlu Bayti wa Mtume (saw) hususan Imam Ali Bin Abi Twalib. Kadhalika alikuwa akitoa mawaidha na hekima kupitia mashairi ya lugha ya Kifarsi. Abu Is'haq Kisai Marvazi ameacha athari nyingi katika uwanja huo ambazo zimehifadhiwa katika maktaba mbalimbali nchini Iran.

Abu Is'haq Kisai Marvazi

Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita, yaani tarehe nane Dei 1285 Hijiria Shamsia, katiba ya Iran iliyokuwa imeandikwa na kuandaliwa na Bunge la kwanza la taifa ilitiwa saini na kupasishwa na mfalme wa wakati huo wa Iran Mozaffar ad-Din Shah Qajar. Katiba hiyo ilikuwa na vipengee 51 ambapo baadaye viliongezwa vipengee 107 kama vikamilisho. Katika kipindi cha miaka iliyofuata na katika zama za tawala mbalimbali hususan katika kipindi cha utawala wa kidikteta wa Kipahlavi, katiba hiyo ilifanyiwa marekebisho ya kimsingi. Akthari ya marekebisho hayo yalikuwa kwa madhara ya mamlaka ya wananchi na Uislamu.

Katiba yenyewe

Siku kama ya leo miaka 89 iliyopita alifariki dunia Theodor Nöldeke msomi wa Kijerumani na mtaalamu wa mambo ya nchi za mashariki. Alihitimu masomo yake katika taaluma ya theolojia, falsafa pamoja na lugha mbalimbali ambapo katika risala yake ya kuhitimu masomo aliandika historia ya Qur'ani Tukuufu kwa kutumia vyanzo vya dini ya Kiislamu na uchunguzi kutoka kwa wasomi wa Ulaya waliobobea katika masuala ya mashariki ambapo alitunukiwa shahada ya uzamivu. Theodor Nöldeke alianza kufundisha katika Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 25 na kuifanya kazi hiyo kwa miaka mingi. Aidha Theodor Nöldeke alibobea katika lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kituruki, Kigiriki, Kihispania na Kitaliano. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 94.

Theodor Nöldeke

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, mkataba wa kupata uhuru Jamhuri ya Ireland ulitiwa saini baina ya viongozi wa wapigania jamhuri wa Ireland na utawala wa wakati huo wa Uingereza. Hata hivyo kutokana na kuanza Vita vya Pili vya Dunia, serikali ya Uingereza ilikataa kutekeleza mkataba huo. Baada ya vita hivyo, mnamo mwaka 1949, Jamhuri ya Ireland ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa mkoloni Muingereza. Uhuru wa Ireland ilikuwa natija ya mapambano ya karne nane ya wapigania Jamhuri wa Ireland dhidi ya Uingereza.

Bendera ya Ireland

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita alifariki dunia Ayatuullah Sheikh Ali Akbar Nahavandi, msomi mkubwa mwenye zuhdi. Ayatullah Ali Akbar Ibn Mula Muhammad Hussein Nahavandi, ni mwenye asili ya mji wa Nahavand katika mkoa wa Hamadan nchini Iran ingawa alizaliwa mjini Mash'had. Awali alijifunza masomo ya Kiislamu mjini Tehran kwa Allamah Haj Mirza Hassan Ashtiyani kisha akaelekea mjini Najaf Iraq na kupata kusoma kwa Allamah Haj Mirza Habibullah Rashti na Shariat Isfahani. Mwaka 1328 Hijiria Ayatullah Sheikh Ali Akbar Nahavandi alielekea mjini Mash'had na kuweka huko makazi yake. Vitabu vya 'Al Bayaanur Rafii fii Ahwaali Khawaajah Rabii' 'Golzaar Akbari' na 'Lole Zaar' ni miongoni mwa athari za msomi huyo. Ayatuullah Sheikh Ali Akbar Nahavandi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 90 na kuzikwa katika mji wa Mash'had.

Ayatuullah Sheikh Ali Akbar Nahavandi