Juamanne tarehe 31 Disemba 2019
Leo ni Jumanne tarehe 4 Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na Disemba 31 mwaka 2019.
Katika siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, Rais Boris Yeltsin wa Russia aliondoka madarakani na nafasi yake ikachukuliwa na Vladimir Putin. Kipindi fulani Yeltsin alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti. Boris Yeltsin alichaguliwa kuwa Rais wa Russia Januari mwaka 1991 na alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi. Hata baada ya kusambaratika Umoja wa Sovieti mwishoni mwa mwaka 1991, aliendelea kuwa Rais wa Russia akitumai kwamba, kwa kutumia misaada ya kifedha ya Magharibi angeweza kuiokoa nchi hiyo kutokana na matatizo ya kiuchumi yake ya kiuchumi. Kinyume na matarajio yake, viongozi wa madola ya Magharibi hawakutekeleza ahadi zao, hali iliyopelekea siasa za Rais Boris Yeltsin kushindwa. Kushambuliwa kijeshi eneo lililotangaza kujitawala la Chechnia na kukaliwa kwa mabavu ardhi hiyo na majeshi ya Russia, ni miongoni mwa matukio yaliyojiri katika kipindi cha utawala wa Boris Yeltsin nchini Russia.
Tarehe 10 Dei miaka 25 iliyopita yaani tarehe 31 Disemba mwaka 1994 Idhaa ya Kiswahili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kazi kwa shabaha ya kufikisha sauti na ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wazungumzaji wa lugha hiyo. Matangazo ya Idhaa hii yalianza sambamba na sherehe ya kubaathiwa na kupewa utume Nabii Muhammad (saw). Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran yanahusu masuala ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kadhalika.
Kwa sasa unaweza kuyasikiliza matangazo yetu kwa njia ya moja kwa moja na kupitia hifadhi ya matangazo wakati wowote. Unaweza pia kuyapata matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran kupitia simu ya mkononi bila ya kutoa malipo yoyote isipokuwa gharama zako za kawaida za Intaneti kupitia njia ya kupakua aplikesheni ya matangazo yetu ya IRIB World Service.

Miaka 144 iliyopita katika siku kama ya leo Arthur Christensen mtaalamu wa masuala ya Mashariki alizaliwa huko Copenhagen mji mkuu wa Denmark. Christensen alionyesha hamu kubwa ya kujifunza masuala ya Mashariki hususan historia ya Iran na mwishoni mwa masomo yake, alifanya utafiti kuhusu historia ya fasihi ya Irani. Arthur Christensen aliweza kujifunza vyema lugha ya Kifarsi. Mojawapo ya vitabu vyake muhimu ni kile alichokipa jina la "Iran katika Zama za Wasasani." Christensen aliaga dunia mwaka 1945 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 192 iliyopita, yaani tarehe 31 Disemba mwaka 1827 kibiriti kilivumbuliwa na John Walker mtaalamu wa madawa wa Uingereza. Hata hivyo awali, mbali na kibiriti cha Walker kuwaka kwa taabu na mashaka kilikuwa pia na hatari kwa watumiaji wake. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana wataalamu wengine wakafanya jitihada za kukikamilisha kibiriti hicho. Hatimaye mwaka 1855 mtaalamu mmoja wa Kiswedeni alifanikiwa kutengeneza kibiriti kama hiki kinachotumiwa leo hii baada ya kufanya majaribio na utafiti wa muda mrefu.
Siku kama ya leo miaka 886 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alizaliwa huko nchini Iraq Ibn Athir Jazari mwanahistoria na mwanafasihi mahiri wa Kiislamu. Ibn Athir alisoma mjini Mosul, Sham na Baghdad kwa maulama watajika kama Khatib Tusi. Alikuwa na mapenzi makubwa na kutwalii na kufanya uhakiki kuhusiana na historia na ni kutokana na sababu hiyo athari zake nyingi zilizoko hii leo zinahusiana na historia. Kitabu mashuhuri zaidi cha Ibn Athir ni kile kinachojulikana kwa jina la "al-Kamil Fil Taarikh." Msomi na mwanahistoria huyo wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 630 Hijria katika mji wa Mosul huko Iraq.
