Jan 01, 2020 02:42 UTC
  • Jumatano, tarehe Mosi Januari, mwaka mpya wa 2020

leo ni Jumatano tarehe 5 Jamadil Awwal mwaka 1441 Hijria sawa na Januari Mosi mwaka 2020

Leo ni tarehe Mosi Januari inayosadifiana na kuanza mwaka mpya wa 2020 Miladia. Mpangilio wa miezi ya mwaka wa Kirumi unaoanza Januari hadi Disemba ulianza kutumiwa katika kipindi cha Mfalme Numa Pompilius yapata miaka 700 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih (as). Kwa msingi huo tarehe 31 Disemba huwa siku ya mwisho ya mwaka wa Miladia na usiku wa kuamkia tarehe Mosi Januari huanza sherehe za kupokea mwaka mpya katika jamii za Wakristo na nchi nyingi za Afrika, America, Ulaya, Australia na hata Asia.

Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita alizaliwa Bibi Zainab (s.a) binti mtukufu wa Imam Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatimatu Zahraa (as). Bibi Zainab alikuwa mashuhuri miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo. Katika tukio la Karbala, Bibi Zainab (s.a) alisimama kidete na kukabiliana na dhulma za watawala dhalimu na ujahili watu wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (a.s). Bibi Zainab alipelekwa Sham pamoja na mateka wengine wa Nyumba Tukufu ya Mtume (saw) baada ya mapambano ya Imam Hussein (a.s) huko Karbala. Hotuba za Bibi Zainab mbele ya majlisi ya Ibn Ziyad mtawala wa Kufa na katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko Sham zilikuwa na taathira kubwa katika kufichua dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya na kuonesha jinsi Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume walivyodhulumiwa.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa nchini Iran siku ya kuzaliwa Bibi Zainab (a.s) husherehekewa kama 'Siku ya Wauguzi'.

Siku kama ya leo, miaka 1433 iliyopita kulijiri vita vya Mu'utah, baina ya jeshi la Waislamu na jeshi la Roma na waitifaki wake. Vita hivyo vilitokea baada ya mjumbe aliyekuwa ametumwa na Mtume (saw) huko Sham kwa ajili ya kulingania dini ya Kiislamu, kuuawa shahidi na askari wa kulinda mpaka wa eneo hilo. Baadhi ya wanahistoria wanasema kuwa, miongoni mwa sababu zilizomfanya Mtume (saw) kutuma jeshi la wapiganaji 3,000 kukabiliana na utawala wa Roma katika eneo hilo ni kuuawa shahidi walimu 14 wa Qur'an Tukufu waliokuwa wametumwa na Mtukufu Mtume katika maeneo ya mpakani ya Sham. Katika vita hivyo Mtume alimteua Jaafar bin Abi Twalib, mtoto wa ami yake, kwa ajili ya kuongoza jeshi la Kiislamu, na akawateua Zaid bin Haritha na Abdullah bin Rawaaha kwa ajili ya kukaimu nafasi hiyo. Jeshi la Kiislamu ambalo lilikuwa limechoka kutokana na kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwenda safari ndefu kama hiyo, lilipambana na jeshi la Roma na wapiganaji wa kikabila katika eneo la Mu'utah, magharibi mwa Jordan ya leo ambapo liliwapoteza viongozi wote watatu wa jeshi hilo la Kiislamu. Hatimaye Waislamu walimpa jukumu la kuongoza jeshi hilo Khalid Bin Walid ambaye ndiye kwanza alikuwa amesilimu, ambapo naye alitoa amri ya kuwataka Waislamu kurudi nyuma. Hata kama jeshi la Kiislamu halikushinda vita hivyo, lakini liliweza kusoma mbinu za jeshi la adui hatua ambayo ilikuwa utangulizi wa ushindi dhidi ya jeshi hilo la adui katika vita vya baadaye.

جنگ مؤته

Siku kama ya leo miaka 459 iliyopita, alifariki dunia, Muhammad Mustafa Imadi, maarufu kwa jina la 'Abus-Suud', faqihi na mfasiri wa Qur'an Tukufu. Abus-Suud alizaliwa karibu na mji wa Istanbul, magharibi mwa Uturuki na kuanza kujifunza masomo ya dini ya Kiislamu ambapo alipanda daraja na kuanza kufundisha. Mbali na msomi huyo wa Kiislamu kufahamu lugha ya Kituruki, alikuwa hodari pia katika lugha ya Kifarsi na Kiarabu ambapo aliweza hata kusoma mashairi kwa lugha hizo. Miongoni mwa athari za Abus-Suud ni pamoja na 'Tafsir Abis-Suud' 'Dua Nameh' 'Qanun Nameh' na 'Mafruudhaat.'

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Januari 1956, nchi ya Sudan ilipata uhuru kutoka kwa Misri na Uingereza. Mwaka 1899 Uingereza na Misri zilitiliana saini mkataba wa kuitawala kwa pamoja Sudan. Katikati mwa karne ya 20 lilianza vuguvugu la kutaka kujipatia uhuru nchini Sudan na mwaka 1956 Misri na Uingereza zikalazimika kuutambua uhuru wa nchi hiyo.

Bendera ya Sudan

Tarehe Mosi Januari mwaka 1959 mapinduzi ya Cuba yalipata ushindi na dikteta Fulgencio Batista akaikimbia nchi hiyo. Ushindi wa mapinduzi hayo yaliyoongozwa na Fidel Castro uliiweka Marekani katika mazingira magumu baada ya kushindwa vibaraka wake nchini Cuba.

Cuba

Na siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Mosi Januari 1993, yalianza kutekelezwa makubaliano ya Maastricht, eneo lililoko kusini mwa Uholanzi yaliyokuwa na lengo la kuondoa mipaka ya kiuchumi kati ya nchi 12 za Ulaya. Mkataba wa muungano wa Ulaya ulitiwa saini tarehe 10 Disemba mwaka 1991 na viongozi wa nchi 12 wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya katika mji mashuhuri wa Maastricht. Baadaye Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya ilibadilishwa na kuwa Umoja wa Ulaya. Utekelezwaji wa makubaliano ya Maastricht ulikuwa hatua kubwa katika mchakato wa kuungana zaidi wanachama wa Umoja wa Ulaya japo kuwa umoja huo ulikabiliwa na matatizo mengi katika miaka iliyofuatia.

Makubaliano ya Maastricht