Ijumaa tarehe 3 Januari 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 7 Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na tarehe 3 Januari 2020.
Katika siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, inayosadifiana na Januari 3, 1993 kulitiwa saini makubaliano ya Start-2 kati ya Marais wa zamani wa Russia na Marekani, Boris Yeltsin na Bill Clinton. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi hizo mbili zinapaswa kupunguza theluthi mbili za silaha zao za nyuklia. Makubaliano ya Start-1 yenye lengo hilohilo yalitiwa saini mwaka 1987 kati ya Marais Mikhael Gorbachev wa Russia na Ronald Reagan wa Marekani. Hata hivyo badala ya kuanza kuharibu silaha zake za nyuklia, Marekani ilijilimbikizia sialaha zaidi za aina hiyo suala ambalo liliilazimisha pia Russia kusitisha mpango wa kuanza kuharibu silaha zake za atomiki.
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Dei 1367 Hijria Shamsia, ujumbe wa Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliwasilishwa kwa Mikhail Gorbachev kiongozi wa mwisho wa Umoja wa Kisovieti akimlingania dini ya Kiislamu na kumtaka aachane na fikra za Kimaksi. Katika sehemu moja ya ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tatizo kuu la nchi yako si suala la umiliki, uchumi wala uhuru, bali ni kutokuwa na imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu; na tatizo hilo ndilo lililoitumbukiza au litakaloitumbukiza Magharibi katika mporomoko wa kimaadili na kuifanya igonge ukuta. Tatizo lenu kubwa ni kupigana vita visivyokuwa na faida dhidi ya Mwenyezi Mungu." Mwishoni mwa ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tokea sasa Ukomonisti unapaswa kutafutwa kwenye majumba ya makumbusho ya kisiasa duniani; kwani hauwezi kukidhi mahitaji halisi ya mwanadamu." Imam Khomeini alimuusia Gorbachev akisema: "Nakutaka ufanye uchunguzi wa kina kuhusu Uislamu, sio kwa sababu Uislamu na Waislamu wanakuhitajia wewe, hapana, bali kutokana na thamani za hali ya juu na za ulimwengu mzima za dini hiyo ambayo inaweza kuwa wenzo wa ufanisi na uokovu wa mataifa mbalimbali na kukidhi matatizo makubwa ya mwanadamu."
Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo kulifanyika mkutano wa Guadeloupe kati ya viongozi wa serikali za marekani, Uingereza, Ujerumani ya Magharibi na Ufaransa kwa ajili ya kuchunguza masuala kadhaa muhimu ya kimataifa hususan Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Mkutano huo ulifanyika katika kisiwa cha Guadeloupe kilichoko magharibi mwa Bahari ya Atlantic ambacho ni koloni la Ufaransa. Katika mkutano huo uliofanyika siku 40 kabla ya ushindi kamili wa harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran washiriki wote walikiri kwamba, Mfalme wa wakati huo wa Iran Shah Pahlavi ataondolewa madarakani isipokuwa Jimmy Carter rais wa wakati huo wa Marekani ndiye pekee aliyekwua na matumaini ya kubakia madarakani utawala wa Shah kwa msaada wa jeshi. Haya hivyo mkutano huo wa Guadeloupe haukuwa na mbinu ya kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu ya wanancdhi wa iran na iliishia kukiri nguvu kubwa ya mapinduzi hayo na mustakbali wake mwema.
Miaka 55 iliyopita katika siku kama ya leo tarehe 7 Jamadil Awwal Sayyid Qutb msomi na mwanamapambano wa Misri alinyongwa pamoja na wenzake wawili huko Cairo mji mkuu wa nchi hiyo. Msomi huyo alihifadhi Qur'ani Tukufu katika ujana wake. Sayyid Qutb alifahamiana na Hassan al Bana na kujiunga na harakati ya Ikhwanul Muslimin ya nchi hiyo wakati alipokuwa katika harakati za kisiasa nchini Misri. Sayyid Qutb alitiwa nguvuni na baadaye kunyongwa baada ya kuzuka hitilafu kati ya Gamal Abdel Nasser Rais wa wakati huo wa Misri na Ikhwanul Muslimin. Sayyid Qutb alikuwa akiiamini kwamba "kambi za Mashariki na Magharibi zinapigana na Waislamu na kwamba kambi mbili hizo zimeungana ili kupora maliasili za nchi za Kiislamu". Miongoni mwa vitabu vya msomi na mwanamapamban huyo wa Kiislamu ni kile alichokipa jina la" Uislamu na Amani ya Kimataifa".
Na katika siku kama hii ya leo tarehe 7 Jamadil Awwal miaka 1052 aliaga dunia qari na mtaalamu maarufu wa Hadithi Ibn Ghalbun. Msomi huyo wa Kiislamu alizaliwa mwaka 309 Hijria katika mji wa Halab (Aleppo) nchini Syria lakini akachaga maskani nchini Misri. Ibn Ghalbun alijifunza qira ya Qur'ani na Hadithi kwa wanazuoni wa zama zake na kuwa mwalimu mahiri katika taaluma hizo. Mtaalamu huyo wa Hadithi wa Kiislamu alikuwa ya mitazamo mipya kuhusiana na elimu ya qiraa ya Qur'ani tukufu ambayo imeelezwa na mwanafunzi wake, Makki bin Abu Twalib katika kitabu cha al Kashf. Vilevile alikuwa hodari na gwiji katika fasihi na mashairi ya lugha ya Kiarabu. Kitabu muhimu zaidi ya Ibn Ghalbun ni al Irshad kinachohusiana na visomo saba vya Qur'ani tukufu.
