Alkhamisi tarehe 2 Januari 2010
Leo ni Alkhamisi tarehe 6 Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na Januari Pili mwaka 2010.
Siku kama ya leo miaka 176 iliyopita ilianzishwa huduma ya posta ya kisasa na kuwekwa sanduku la kwanza la posta huko Vienna mji mkuu wa Austria. Kabla ya kufikia hatua ya kuboreshwa huduma za uchukuzi wa barua na vifurushi, vipando kama vile farasi, ngamia au hata mashua maalumu zilitumika kusafirishia barua na vifurushi.
Miaka 154 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Gilbert Murray, mshairi na malenga wa Australia. Akiwa na umri wa miaka 11 Murray alielekea nchini Uingereza na baada ya kumaliza masomo ya juu katika Vyuo Vikuu nchini humo, alifundisha taaluma ya utamaduni na fasihi ya Kigiriki katika Chuo Kikuu cha Oxford. Murray alifariki dunia mwaka 1957 na kuacha athari za vitabu kadhaa kama vile, 'Historia ya Fasihi ya Ugiriki ya Kale' na 'Imani, Vita na Siasa'.

Katika siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, alizaliwa Isaac Asimov, mwandishi na mkemia maarufu wa Kimarekani aliyekuwa na asili ya Russia. Asimov alivutiwa mno na elimu ya kemia na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika taaluma hiyo. Msomi huyo alifanya utafiti na uhakiki mkubwa wa elimu ya kemia na taaluma nyingine. Hata hivyo jambo lililomtofautisha na wasomi wengine ni uwezo wake wa kuarifisha sayansi mbalimbali kwa lugha nyepesi kwa watu hususan tabaka la vijana. Isaac Asimov ameandika karibu vitabu 270 katika nyanja mbalimbali za sayansi, hisabati na sayansi za jamii.
Miaka 78 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Ayatullah Fayyaz Zanjani fakihi na msomi mahiri wa elimu ya Usuul. Awali alisoma kwa baba yake na baadaye akahudhuria masomo kwa walimu mahiri wa zama hizo mjini Tehran kama Mirza Muhammad Hassan Ashtiyani na kuwa hodari katika taaluma za fikihi, usuul, mantiki na tafsiri ya Qur'ani. Mwanazuoni huyo alikuwa Marjaa Taqlidi wa Zanjani. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 30 alikuwa mmoja wa walinganiaji wakubwa wa mafundisho ya Ahlul Bayt (sa).
Katika siku kama ya leo miaka 4 iliyopita yaani tarehe Pili Januari 2016 utawala wa Saudi Arabia ulimuua mwanazuoni wa Kiislamu Sheikh Nimr Baqir al Nimr. Baqir al Nimr aliyekuwa mwanazuoni wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia alizaliwa tarehe 21 Juni mwaka 1959 katika mji wa Awwamiyya huko mashariki mwa Saudi Arabia. Alipata elimu ya msingi katika mji huo na mwaka 1400 Hijria yaani mwaka 1989 alielekea Tehran nchini Iran na kupata elimu katika chuo cha kidini cha Qaim kilichoasisiwa na Ayatullah Sayyid Muhammad Taqi Mudarrisi. Baada ya kupata elimu katika chuo hicho kwa kipindi cha miaka 10 Sheikh Nimr alikwenda Syria na kuendelea kutafuta elimu zaidi katika Chuo cha Kidini cha Bibi Zainab (as). Aliporejea Saudi Arabia, Sheikh Nimr aliasisi kituo cha kidini cha al Imam al Qaim katika mji wa Awwamiyya ambacho kiliweka jiwe la msingi la kuanzishwa Kitiuo cha Kiislamu hapo mwaka 2011.
Mwanazuoni huyo wa Kiislamu daima alikuwa akikosoa siasa za ukandamizaji na kibaguzi za utawala wa kifalme wa Saudia na alifungwa jela mara kadhaa kutokana na kusema haki na kweli. Mara ya mwisho Sheikh Baqir Nimr alikamatwa tarehe 8 Julai mwaka 2012 katika maandamano makubwa ya Waislamu wa Kishia ya kupinga ubaguzi na ukandamizaji wa utawala wa Aal Saud na tarehe 15 Oktoba msomi huyo wa Kiislamu alihukumiwa kifo cha kukatwa kichwa kwa panga na kusulubiwa kadamnasi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kula njama dhidi ya utawala wa nchi hiyo. Hukumu hiyo ilitekelezwa tarehe Pili Januari mwaka 2016. Kuuawa kwa msomi na mwanaharakati huo kulipingwa vikali na jumuiya za kikanda na kimataifa za kutetea haki za binadamu.