Jumamosi, Januari 4, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 8 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1441 Hijria, sawa na tarehe 4 Januari mwaka 2020 Miladia.
Siku kama yya leo miaka 447 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 4 Januari 1573, Papa Gregory VII, kiongozi wa Wakristo katika karne ya 16, aliitisha mkutano maarufu kwa jina la mkutano wa 'upokonyaji'. Mkutano huo uliohudhuriwa na wawakilishi wa kidini kutoka nchi za Kikristo, ulichukua uamuzi wa kuwapokonya wafalme wa nchi hizo mamlaka ya kuchagua viongozi wa kidini wa Kikristo. Uamuzi huo uliwakasirisha watawala hao na kusababisha vita vya umwagikaji damu vilivyodumu kwa miaka kadhaa, kati ya Mapapa na Wafalme wa Ulaya. ***
Katika siku kama ya leo ya tarehe 8 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal miaka 1313 iliyopita, alifariki dunia mwanazuoni wa Kiislamu, Muhammad Baqir Zainul Abidin Khansari katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi na hadithi na alipewa ijaza ya kunukuu hadithi na wanazuoni wakubwa katika taaluma hiyo. Baada ya muda msomi huyo mkubwa ambaye alikuwa gwiji wa wasifu na shajara za maulamaa na wataalamu wa fiqhi ya Kiislamu, alishika hatamu za kuongoza Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Isfahan. Mirza Muhammad Baqir Khansari ameandika vitabu vingi na miongoni mwa vitabu vyake ni Raudhaatul Jannat na Hashiyatu Sharhil Lum'ah. ***
Miaka 118 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria aliaga dunia Sheikh Muhammad Abduh ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika mji wa Alexandria nchini Misri. Alipata elimu katika Chuo Kikuu cha al Azhar na kisha akahudhuria darsa za Jamaluddin Asadabadi, mwanazuoni aliyepigania uhuru wa nchi za Kiislamu. Baada ya Sayyid Jamaluddin kupelekwa uhamishoni, Sheikh Muhammad Abduh alichukua nafasi yake ya kufundisha na kutoa elimu kwa wanazuoni na wanafikra za Kiislamu. Hata hivyo Sheikh Abduh alibaidishiwa nchini Syria baada ya satuwa ya wakoloni wa Kiingereza kuenea nchini Misri. Baada ya kufunza kwa kipindi cha miaka sita nchini Syria alihamia Paris na kusaidiana na Sayyid Jamaluddin Asadabadi katika kuchapisha gazeti la al Uruwatul Wuthqaa. ***
Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 4 Januari 1961, ulifanyika mkutano wa kisiasa huko Casablanca nchini Morocco kwa shabaha ya kubuni msimamo mmoja wa kisiasa wa Kiafrika. Mkutano huo ulihudhuriwa na nchi za Algeria, Ghana, Guinea, Mali, Misri na Morocco. Lengo la mkutano huo lilikuwa kuanzisha kundi moja la kijeshi na soko la pamoja la nchi za Afrika. ***
Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo, wakati wa kilele cha harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa kifalme wa Shah, Jenerali Robert E. Huyser aliyekuwa mshauri mkuu wa kijeshi na Naibu Kamanda wa Jeshi la Anga la Marekani aliwasiri kwa siri mjini Tehran. Jenerali Huyser alikuwa na jukumu maalumu la kuisaidia serikali ya Marekani katika kuchukua maamuzi ya baadaye na kupata habari za ndani za Iran katika kipindi cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Katika kipindi chote cha zaidi ya siku 30 za kuwepo kwake mjini Tehran Jenerali Huyser alikutana mara moja tu na Shah na katika kikao hicho iliainishwa saa na siku ya kuondoka Shah nchini Iran. ***
Na siku kama ya leo miaka 9 iliyopita, alifariki dunia Mohamed Bouazizi, kijana muuza mboga wa Tunisia, siku 18 baada ya kujichoma kwa moto katika mji wa Sidi Bouzid akilalamikia ukandamizaji na dhulma ya serikali ya nchi hiyo. Kujichoma moto kijana huyo muuza mboga kuliibua harakati ya wananchi wa Tunisia dhidi ya utawala wa kiufisadi wa nchi hiyo na kuwa sababu ya kupinduliwa dikteta Zainul Abidin bin Ali. Kitendo hicho cha Bouazizi pia kilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi. ***