Jan 05, 2020 00:56 UTC
  • Jumapili, Januari 5, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 9 Mfunguo Nane, Jamadul-Awwal 1441 Hijria, mwafaka na tarehe 5 Januari 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1417 iliyopita vilianza vita vya miaka 24 kati ya falme za Iran na Roma. Vita hivyo viliibuka kufuatia kuuawa Maurice, aliyekuwa mfalme wa Roma na ambaye pia alikuwa muungaji mkono na rafiki wa karibu wa Mfalme Khosrow Parviz wa Iran. Kufuatia mauaji hayo ya Maurice, mtoto wake alikuja Iran na kumuomba msaada Mfalme Khosrow. Mfalme huyo wa Iran na kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Maurince, alituma jeshi lililojizatiti kwa silaha kwenda kuishambulia Roma ambapo kwa kipindi kifupi liliweza kuteka miji mingi ya nchi hiyo. Baada ya ushindi huo, mfalme mpya wa Roma alimtuma mjumbe wake kuja Iran kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya amani na mfalme wa Iran, hata hivyo Mfalme Khosrow Parviz ambaye alikuwa tayari ameingiwa na kiburi cha kupata ushindi mkubwa katika vita hivyo, alikataa mpango wa amani na hivyo akawa ameendeleza vita hivyo. Vita hivyo ambapo pande mbili zilipata ushindi katika vipindi tofauti, viliendelea kwa muda wa miaka 24.

Wigo wa tawala za wafalme wa Iran na Roma

Siku kama ya leo miaka 655 iliyopita yaani sawa na tarehe 9 Jamadil Awwal mwaka 786 Hijria, aliuawa shahidi faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi Muhammad bin Jamaluddin Makki Amili, mashuhuri kwa jina la "Shahidi wa Kwanza." Alizaliwa mwaka 734 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Jabal Amil nchini Lebanon. Alijifunza elimu mbalimbali kutoka kwa walimu wakubwa wa zama zake kama vile Allama Hilli. Mbali na elimu ya dini, Muhammad bin Jamaluddin pia alikuwa hodari katika taaluma za mashairi na fasihi. Katika miaka 52 ya umri wake uliojaa baraka, Shahidi wa Kwanza aliandika vitabu vingi, ikiwa ni pamoja na "Albaqiyatus-Swalihat" na "Allumuatu Dimashqiyya." Aliuawa na wapinzani wake wenye taasubi katika siku kama ya leo.

Muhammad bin Jamaluddin Makki Amili

Siku kama ya leo miaka 329 iliyopita,  inayosadifiana na tarehe 5 Januari 1691, ilichapishwa na kusambazwa noti ya kwanza huko Ulaya. Noti hiyo ilichapishwa na Benki ya Stockholm na kutumiwa kama fedha. Kabla ya kuchapishwa noti hiyo nchini Sweden, miamala ya kibiashara ilikuwa ikifanyika kwa kutumia sarafu za dhahabu zenye pembe nne. Moja ya noti za awali kabisa kuchapishwa nchini Sweden, imehifadhiwa kwenye jumba la makumbusho la Benki ya Stockholm.

Noti ya kwanza kuwahi kuchapishwa barani Ulaya

Siku kama ya leo miaka 211 iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa Dardanelles (Treaty of the Dardanelles) baina ya utawala wa Othmania na Uingereza. Kwa mujibu wa mkataba huo, Uingereza iliahidi kuondoka katika ardhi zote zilizokuwa chini ya utawala wa Othmania ikiwemo Misri na kuhitimisha ukaliaji mabavu wa ardhi hizo. Mkabala wake, utawala wa Othmania uliahidi kutambua rasmi haki za kibalozi za Uingereza katika ardhi za utawala wa Othmania.

Mwonekano wa eneo tajwa

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran waligoma kwenda madarasani wakionesha upinzani wao dhidi ya safari ya rais wa wakati huo wa Marekani, Jimmy Carter hapa nchini na uungaji mkono wake kwa utawala wa Shah. Wakati huo Carter alikuwa akidai kuwa ni mtetezi wa haki za binadamu na mpinzani wa suala la kuziuzia silaha tawala za kidikteta. Hata hivyo serikali ya Washington ilichukua uamuzi wa kufunga mikataba ya kuuzia silaha nzito utawala wa kidikteta wa Shah na kupuuza ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliokuwa ukifanywa nchini Iran. Jimmy Cater alifikia kiwango cha kumwita Shah kuwa ni kiongozi anayependwa na wananchi na kwamba, Iran ni kisiwa cha amani. Hata hivyo muda mfupi baadaye wananchi walianza harakati za kupigania uhuru na kujitawala na miezi 13 baada ya safari ya Carter mjini Tehran, Shah aliondolewa madarakani na ikaanzishwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais wa wakati huo wa Marekani, Jimmy Carter alipotia mguu nchini Iran kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, sawa na tarehe 5 Januari 1985, utawala wa Kizayuni wa Israel uliwachukua maelfu ya Mayahudi wa Ethiopia "Mafalasha' kupitia ardhi ya Sudan. Mafalasha hao ambao idadi yao ilikuwa watu 8,000 walihamishiwa huko Israel. Nchi za Kiarabu ziliikasirikia Sudan kwa kushirikiana na Israel katika kuwahamisha Mayahudi wa Kiethiopia na kuwapeleka Israel.

Waethiopia ndani ya Israel ambao hata hivyo wanaishi kwa tabu na kukandamizwa

Na siku kama ya leo miaka 5 iliyopita, alifariki dunia Eusébio da Silva Ferreira, nyota wa mpira wa miguu nchini Ureno. Alizaliwa Januari 25 mwaka 1942, huko Maputo Msumbiji. Alionyesha hamu na kipaji cha hali ya juu cha kusakata kabumbu akiwa shuleni. Alikuwa nyota katika timu ya taifa ya soka ya Ureno katika zama zake. Alifunga jumla ya magoli 733 katika mechi za kimataifa 745 alizocheza na anahesabiwa kuwa, mmoja wa wafungaji bora duniani katika ulimwengu wa soka. Mwaka 1956 Eusébio da Silva Ferreira alishinda tuzo ya mchezaji bora barani Ulaya. Aidha katika miaka ya 1970 na 1973 alitunukiwa tuzo ya mchezaji bora wa soka nchini Ureno. Baada ya kuugua moyo kwa muda na kulazwa mara kadhaa hospitali hatimaye Eusébio da Silva Ferreira aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 71.

Eusébio da Silva Ferreira