Jumatatu tarehe 6 Januari 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 10 Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na Januari 6 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita kulitokea hamasa ya mashahidi wa Huweize iliyoongozwa na Shahidi Alamul Huda katika miezi ya mwanzoni mwa uvamizi wa Iraq dhidi ya ardhi ya Iran. Mwezi Dei mwaka 1359 Hijria Shamsia na baada ya jeshi la Iran ya Kiislamu kuvishinda vikosi zaidi ya viwili vya jeshi la Iraq huko kusini mwa eneo la Susangerd, kundi moja la Jeshi al Sepah la Ahwaz huko kusini mwa Iran lilitumwa katika mji wa Huweize kwenda kuulinda mji huo mbele ya mashambulizi ya Iraq. Hata hivyo kutokana na kuchelewa kufika zana na hujuma kubwa ya Iraq, jeshi la Iran lililazimika kurudi nyuma. Wakati huo zaidi ya wapiganaji mia moja wa Jeshi la Sepah, wapiganaji wa kujitolea na wanafunzi wa vyuo vikuu wafuasi waaminifu wa Imam Khomeini wakiongozwa na Sayyid Muhammad Hussein Alamul Huda walibakia katika mji huo wa Huweize wakipambana na adui na wakauawa shahidi. Baadaye jeshi la Iraq liliuvunja kabisa mji wa Huweize na kuusawazisha na ardhi. Pamoja na hayo ushujaa wa vijana hao shupavu wa Iran waliosabilia roho zao kulinda ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu umebakia hai katika historia ya Iran.
Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita alifariki dunia Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandiyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi na kutokuwa na wizani. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh".
Katika siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, aliaga dunia Theodore Roosevelt Rais wa zamani wa Marekani. Theodore Roosevelt Rais wa 26 wa Marekani alizaliwa Oktoba 27 mwaka 1857. Alijiunga na harakati za kisiasa akiwa katika rika la ujana. Alikuwa mwanachama wa chama cha Republican. Alikuwa Makamu wa Rais na baada ya kuuawa William McKinley aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo, Theodore Roosevelt akawa Rais wa muda wa nchi hiyo. Mwaka 1901 alichaguliwa kuwa Rais wa Marekani. Mwanzoni mwa utawala wake, Theodore Roosevelt aliimarisha uwepo wa vikosi vya Marekani nchini Cuba iliyokuwa ikikaliwa kwa mabavu na Washington na akaitangaza rasmi nchi hiyo kuwa chini ya mamlaka na himaya ya Marekani.
Na siku kama ya leo 159 iliyopita ilianzishwa nchi ya Romania. Mpango wa kuasisiwa nchi ya Romania ulibuniwa tarehe 13 Disemba 1859 kwa kuunganishwa miji miwili midogo ya Moldavia na Wallachia. Miaka miwili baadaye majimbo na miji mingine ilijiunga na umoja huo na kuundwa nchi ya Romania.