Jan 07, 2020 01:00 UTC
  • Jumanne, tarehe 7 Januari, 2020

Leo ni Jumanne tarehe 11 Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na Januari 7 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya Kiislamu na mtarjumi wa Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kijapani Toshihiko Izutsu. Alizaliwa tarehe 4 Mei 1914 katika mji wa Tokyo na mwaka 1960 alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya lugha na kuanza kufunza lugha na falsafa yake. Toshihiko Izutsu alitunukiwa nishani ya juu kabisa ya elimu kutoka kwa mfalme wa Japan na ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni "Historia ya Fikra za Kiislamu", tarjumu ya kitabu cha "al Mashair" cha Mulla Sadra na vilevile tarjumu ya kitabu cha "Fihi Maa Fiih" cha Maulawi kwa lugha ya Kijapan.

Toshihiko Izutsu

Tarehe 7 Januari miaka 41 iliyopita dikteta wa Cambodia Pol Pot alikimbia nchi kufuatia mashambulizi ya jeshi la Vietnam dhidi ya nchi hiyo. Pot alikuwa kiongozi wa kundi la Khmer Rouge lililokuwa muungaji mkono mkubwa wa fikra za kimao na serikali ya China. Sifa kuu ya serikali ya Pol Pot ilikuwa kutumia mabavu dhidi ya raia, kuwahamishia kwa nguvu vijijini na kufuta kabisa athari zote za utamaduni na ustaarabu asilia. Pol Pot na kundi lake na Khmer Rouge waliua watu wanaokadiriwa kuwa milioni moja na nusu hadi mbili hususan raia wenye asili ya Vietnam katika kipindi cha chini ya miaka mitatu ya utawala wake huko Cambodia. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana jeshi la Vietnam likachukua hatua za kuiondoa madarakani serikali ya Pol Pot.

Pol Pot

Tarehe 17 Dei miaka 42 iliyopita wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa kote nchini wakilalamikia kuchapishwa makala iliyomvunjia heshima mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Maandamano hayo yalizidisha vuguvugu na kasi za Mapinduzi ya Kiislamu kuelekea katika ushindi. Utawala wa Shah ambao ulikuwa ukifahamu vyema ushawishi na uungaji mkono mkubwa wa Imam Khomeini miongoni mwa wananchi, ulikuwa ukidhani kwamba kumvunjia heshima Imam Khomeini kungeweza kupunguza kiwango cha mapenzi na uungaji mkono mkubwa wa wananchi wa shakhsia huyo. Katika kufanikisha lengo hilo, gazeti la Ittilaat lililokuwa likitolewa mjini Tehran liliandika makala ya kumvunjia heshima Imam Khomeini katika toleo lake la mwezi Dei mwaka 1356 Hijria Shamsiya. Hata hivyo makala hiyo ilikuwa kama cheche ya moto iliyochochea zaidi harakati za mapinduzi na hatimaye tarehe 22 mwezi Bahman mwaka 1357, utawala kibaraka wa Shah ukang'olewa madarakani kwa mapambano ya wananchi wa Iran.

Imam Khomeini

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, alifariki dunia Nikola Tesla mwanafizikia mzaliwa wa Yugoslavia. Nikola alizaliwa mwaka 1857 na alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza masomo ya fizikia wakati akiwa shuleni. Msomi huyo wa Kiyugoslavia alifanya tafiti na uvumbuzi wake mwingi katika uwanja wa nishati ya umeme na kupata mafanikio makubwa. Umeme mbadala au altenative electricity unahesabiwa kuwa miongoni mwa uvumbuzi wa Nikola Tesla. Mwanafikizia huyo alikipa jina lake la Tesla, kifaa kinachotumika kupimia kiwango na mtiririko wa sumaku yaani (magnetic flux).

Nikola Tesla

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, Reza Pahlavi mfalme wa wakati huo wa Iran, alitoa amri ya kuwazuia wanawake kuvaa aina yoyote ya vazi la Kiislamu yaani hijabu hapa nchini. Amri hiyo ilitolewa baada ya utekelezwaji wa mpango wa kubadili mavazi ya kiume kwa lengo la kufuta kabisa athari za Kiislamu na kufuata kibubusa siasa za madola ya Magharibi. Kabla ya hapo mfalme huyo alikuwa amefanya safari nchini Uturuki na kukutana na Rais wa nchi hiyo Mustafa Kemal Atatürk, ambaye naye alikuwa amepiga marufuku vazi la Kiislamu la mwanamke wa Kiislamu hijabu nchini humo kwa kufuata siasa za Magharibi. Kufuatia hatua hiyo vibaraka wa mfalme huyo walianza kuwafanyia dhihaka na kuwadunisha wanawake wa Kiislamu waliokuwa wakivaa vazi hilo la heshima.

Reza Khan

Na miaka 844 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Khoja Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mwanahisabati, mnajimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiirani katika mji wa Tusi kaskazini mashariki mwa Iran. Katika maisha yake aliasisi kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kuangalilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua iliyojulikana kwa jina la Maraghe huko kaskazini magharibi mwa Iran. Aalimu huyo aligundua namna mpya za kutumia saa ya jua kwa ajili ya kituo hicho. Kituo hicho kilikuwa na suhula muhimu zaidi ambazo kwa miaka 300 baada ya hapo hazikuweza kushushudiwa katika nchi za Magharibi.

Khoja Nasiruddin Tusi