Jumatano tarehe 8 Januari 2020
Leo ni Jumatano tarehe 12 Jamadil Awwal mwaka 1441 Hijria sawa na na Januari 8 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 488 iliyopita alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu Ibn Tulun Dimashqi, aliyekuwa faqihi, mwanafasihi na mwanahistoria huko mjini Damascus, Syria. Ibn Tulun alizaliwa mwaka 880 Hijiria mjini Damascus na katika umri wake wote alifanya jitihada kubwa za utafiti, kufundisha na kuandika vitabu vya taaluma mbalimbali. Ibn Tulun Dimashqi ameandika vitabu vingi vya thamani kuhusiana na historia ya Kiislamu na katika uwanja wa tafsiri ya Qur'ani Tukufu, hadithi, lugha, tiba na irfani. Kitabu cha 'al-Safiinatu al-Tuluuniyyah' ni miongoni mwa athari za mwanazuoni huyo.

Siku kama ya leo miaka 378 iliyopita alifariki dunia msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia Galileo Galilei akiwa na umri wa miaka 78. Alizaliwa katika mji wa Pisa na alisoma fasihi hadi alipofikisha umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu, Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua. Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya msomi Mwislamu wa Iran ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, Kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa ni kafiri na akahukumiwa. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Katika siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, yaani tarehe 8 Januari mwaka 1932 ulianza utawala wa kifalme wa Abdul-Aziz Ibn Saud katika eneo la Bara Arabu kupitia msaada wa Uingereza. Abdul-Aziz Ibn Saud, aliyekuwa mmoja wa viongozi wa makabila ya Hijaz, alianzisha mapigano dhidi ya utawala wa Othmania mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 na kupata ushindi. Mwaka 1903 mtawala wa Kiothmania alitimuliwa katika eneo la ya al-Ahsa huko Hijazi na tukio hilo lilikuwa jiwe la msingi wa kuasisiwa utawala wa Aal-Saud katika maeneo hayo. Katika kipindi cga Vita vya Kwanza vya Dunia, Aal-Saud waliingia ubia wa urafiki na Uingereza. Hatimaye mwishoni mwa vita hivyo vilivyomalizika kwa kushindwa vibaya utawala wa Othomania, utawala huo ulifikia tamati kikamilifu katika eneo hilo la Bara Arabu. Katika vita vilivyopiganwa baina ya Abdul-Aziz Ibn Saud na mtawala Hussein Bin Ali Sharif aliyekuwa mtawala wa mji wa Makkah, Ibn Saud aliibuka mshindi na akatwaa kwa nguvu eneo hilo la Hijaz. Hatimaye mwaka 1926 na kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwepo kati ya Uingereza na mtawala huyo huyo wa Kiwahabi, Abdul-Aziz Ibn Saud alijitangaza kuwa kiongozi wa Hijaz. Mwaka 1927 Ibn Saud alijitangaza rasmi kuwa mtawala wa Hijaz na Najd na tarehe 8 Januari mwaka 1932 Abdul Aziz alitangazwa kuwa mfalme wa Saudi Arabia. Hadi kutwaa madaraka ya eneo lote la Hijaz, watu wa kizazi cha Aal Saudi walifanya mauaji mengi na umwagaji damu mkubwa na kuwalazimisha watu wa maeneo hayo kufuata fikra na itikadi potufu za kiwahabi.
Na Tarehe 18 Dei mwaka 1385 Hijria Shamsia yaani siku kama ya leo miaka 13 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mhakiki na mwanahistoria wa Iran Hujjatul Islam Ali Dawwani. Msomi huyu alizaliwa mwaka 1308 Hijria Shamsia karibu na mji wa Kazerun ulioko kusini mwa Iran. Alielekea Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kupata elimu za Kiislamu akiwa na umri wa miaka 14 na kurejea nchini miaka mitano baadaye. Ali Dawwani aliendelea kutafuta elimu katika mji mtakatifu wa Qum na kusoma kwa wanazuoni wakubwa kama Imam Ruhullah Khomeini na Ayatullah Borujerdi hadi alipopata daraja ya ijtihadi. Alibobea sana katika elimu ya historia na ameandika vitabu vingi katika uwanja huo. Miongoni mwa vitabu vyake ni "Fakhari za Uislamu", "Mbora wa Wanawake Duniani" na "Harakati ya Wanazuoni wa Iran".