Ijumaa tarehe 10 Januari mwaka 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 14 Jamadil Awwal mwaka 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 10 Januari 2020.
Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, wataalamu wawili wa Uswisi walifanikiwa kutengeneza saa ya elekroniki. Baada ya miaka 12 ya juhudi kubwa, hatimaye wataalamu Solvil na Titus walifanikiwa kutengeneza chombo hicho kwa kuweka vifaa kadhaa muhimu na makini. Aina hii ya saa ni makini mno na hufanya makosa machache sana ikilinganishwa na saa nyingine.

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, inayosadifiana na 10 Januari 1920, Jumuiya ya Mataifa ilianza shughuli zake rasmi huko Geneva, Uswisi. Jumuiya hiyo iliundwa baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia kwa shabaha ya kuimarisha amani na usalama duniani. Mwanzoni nchi za Kiafrika na Urusi hazikujiunga na jumuiya hiyo na badala yake nchi za Uingereza na Ufaransa ndizo zilizobeba jukumu la kuzisaidia nchi hizo. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, mnamo mwezi Aprili 1946, uliundwa Umoja wa Mataifa na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa, ingawa matatizo yaliyokuwa yakiikumba Jumuiya ya Mataifa bado yanaendelea kuukumba Umoja wa Mataifa hadi hii leo.
Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita, alifariki dunia mjini Tehran Haj Mulla Ismail Sabzevari, mpokezi wa hadithi na hatibu mkubwa wa karne ya 13 Hijria. Mulla Sabzevari alizaliwa katika eneo la Sabzevar lililoko kaskazini mashariki mwa Iran. Alijifunza falsafa kwa Mulla Hadi Sabzevari aliyekuwa mashuhuri kwa lakabu ya Mwanafalsafa wa Mashariki. Baadaye alihamia katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu zaidi na kupata daraja ya ijtihad. Msomi huyo ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha "Majmaun Nurain" na "Nawadirul Aathar".

Siku kama ya leo miaka 196 iliyopita inayosadifiana na 10 Januari 1824, Joseph Aspdin mwanakemia wa Uingereza alifanikiwa kutengeneza saruji na kwa utaratibu huo kupatikana mabadiliko makubwa katika shughuli za ujenzi. Hatua hiyo ilitambuliwa kama tukio kubwa katika shughuli za kimaendeleo na ujenzi mpya wa nyumba. Joseph Aspdin ambaye alikuwa akifanya utafiti kwa miaka kadhaa ili kutengeneza mada ambayo ingesaidia kuimarisha msingi wa nyumba, hatimaye alifanikiwa kutengeneza saruji baada ya majaribio chungu nzima.