Jan 12, 2020 21:10 UTC
  • Jumatatu 13 Januari 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 17 Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na Januari 13 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1150 iliyopita, yaani mwaka 291 Hijiria, alifariki dunia Abul-Abbas Ahmad bin Yahya, mtaalamu maarufu wa lugha na nahau. Abul-Abbas katika masomo yake alibobea katika ulingo wa fasihi ya Kiarabu na baada ya miaka kadhaa ya kufanya utafiti wa kina, akatokea kuwa mtaalamu mkubwa katika uwanja huo. Miongoni mwa athari zilizobakia kutoka kwa mtaalamu huyo, ni pamoja na kitabu maarufu kiitwacho 'I'raabul-Qur'an'. 

Siku kama ya leo miaka 991 iliyopita, alizaliwa Muhammad Ghazali msomi wa fiq'hi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiislamu wa Iran. Ghazali alisoma elimu ya fiq'hi kwa Abu Nasri Ismail na alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo akiwa na umri wa miaka 28. Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati huo Khawaja Nidham al-Mulk kumwalika msomi huyo kwenda Baghdad kwa ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na masuala ya ualimu. Imam Muhammad Ghazali aliandika kitabu chake maarufu cha "Ihyau Ulumud-Din," mwaka mmoja kabla ya kurejea Iran. Vitabu vingine mashuhuri vya msoni huyo ni "Kemia ya Saada" na "Nasaha za Wafalme." 

Imam Muhammad Ghazali

Tarehe 13 Januari miaka 570 iliyopita alizaliwa baharia na mvumbuzi wa Kireno kwa jina la Bartholomew Diaz. Baada ya kusafiri katika Bahari ya Atlantic kuelekea kusini mwaka 1488, Diaz aligundua Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) katika sehemu ya kusini zaidi ya bara la Afrika. Miaka kumi baadaye baharia mwenzake kwa jina la Vasco Da Gama naye pia alifanikiwa kugundua njia ya baharini kuelekea India kupitia eneo hilo.

Bartholomew Diaz

Miaka 79 iliyopita katika siku kama hii mkutano wa kihistoria wa nchi waitifaki za Ulaya katika Vita vya Pili vya Dunia ulifanyika mjini London, Uingereza. Mkutano huo ulifanyika kufuatia pendekezo la waziri mkuu wa wakati huo wa Uingereza Winston Churchill, lengo kuu lilikuwa kuratibu siasa za wakuu wa nchi za Ulaya katika medani za vita dhidi ya nchi mbili za Ujerumani na Italia. Vilevile nchi za Uingereza, Uholanzi, Ubelgiji, Ufaransa, Ugiriki, Norway, Luxembourg na Denmark zilishiriki katika mkutano huo.

Vita vya Pili vya Dunia

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita mapigano makali kati ya polisi wa utawala wa Shah na wananchi wa Iran yalitokea wakati yalipofanyika maandamano makubwa ya wananchi katika miji kadhaa ya Iran. Wananchi wengi wanamapambano waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika maandamano hayo. Katika siku hiyo pia wanachuo na wakazi wa mji wa Tehran ambao walikuwa wamekusanyika kwa wingi mbele ya Chuo Kikuu cha Tehran walitangaza upinzani wao dhidi ya utawala wa Shah na wakataka kurejea Tehran Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, kutoka uhamishoni huko Paris nchini Ufaransa.

Na siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, shambulio la kwanza la kemikali la jeshi la utawala wa wakati huo wa Iraq chini ya uongozi wa dikteta Saddam lilitekelezwa dhidi ya Iran ikiwa ni chini ya miezi minne tu tangu Iraq ianzishe vita vya kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Shambulio hilo la kinyama ambalo lilitekelezwa kilomita 50 magharibi mwa mji wa Ilam magharibi mwa Iran, lilipelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa raia kadhaa. Jeshi la utawala wa Baath, likipata himaya na misaada ya madola ya Magharibi na Umoja wa Kisovieti, lilitumia mara chungu nzima silaha zilizopigwa marafuku dhidi ya raia na wapiganaji wa Iran katika kipindi chote cha vita vyake vya kichokozi dhidi ya taifa hili. Takribani watu elfu kumi waliuawa shahidi na laki moja na elfu 30 walijeruhiwa kufuatia mashambuluio hayo ya silaha zilizopigwa marufuku.

Silaha za kemikali