Jumanne, tarehe 14 Januari, 2020
Leo ni Jumanne tarehe 18 Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na Januari 14 mwaka 2020.
Katika siku kama ya leo miaka 1113 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Ahmad bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Abdu Rabbuh mshairi na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Abdu Rabbuh alibobea mno katika mashairi. Athari mashuhuri zaidi ya msomi huyo ni kitabu cha al Iqdul Fariid ambacho kinahusiana na historia, lugha na mashairi.

Katika siku kama ya leo miaka 991 iliyopita, Abu al-Abbas Ahmad bin Ali maarufu kwa jina la Najjashi aliaga dunia huko Samarra, Iraq akiwa na umri wa miaka 78. Najjashi alikuwa alimu na msomi mkubwa katika karne ya tano Hijria na alibobea na kutabahari katika elimu ya hadithi na wapokezi wa hadithi. Kitabu cha Rijali ni miongoni mwa vitabu muhimu vya msomi huyo wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita ulianza mkutano wa Casablanca nchini Morroco. Mkutano huo uliofanyika wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, ulihudhuriwa na rais wa zamani wa Marekani Franklin Delano Roosevelt na Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill kama viongozi wa nchi mbili kuu za waitifaki na kujadili mpango wa kushambulia Sicily nchini Italia na nchi za washirika.
Mwishoni mwa mkutano huo wawakilishi wa nchi zilizoshiriki walitoa taarifa ya pamoja ambayo kwa mujibu wake nchi waitifaki ziliapa kuendeleza vita hadi wakati wa kusalimu amri mahasimu wao bila ya masharti.
Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita maafisa wa shirika la ujasusi la Israel Mossad walitekeleza mauaji ya kigaidi dhidi ya Salah Khalaf maarufu kwa jila la Abu Iyad akiwa pamoja na maafisa wengine wawili wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Tunisia. Salah Khalaf alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu na kiongozi nambari mbili wa Fat'h baad ya Yaser Arafat.
Mauaji ya viongozi hao wa ngazi za juu wa PLO tena baada ya kukiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi nyingine yaani Tunisia, yalionyesha kwamba utawala haramu wa Israel hauheshimu sheria yoyote ile katika suala la kuwaangamiza wapinzani wake.
Siku kama ya leo miaka 9 iliopita, sawa na tarehe 14 Januari 2011 Rais Zainul Abidin Bin Ali wa Tunisia na dikteta wa nchi hiyo alikimbilia Saudi Arabia kufuatia vuguvugu la mapinduzi ya wananchi. Kukimbia nchi Zainul Abidin, kulihitimisha utawala wa kiimla uliodumu kwa nusu karne wa Habib Bourquiba pamoja na Zainul Abidin Bin Ali na wananchi wa Tunisia wakaonja ladha ya uhuru. Zainul Abidin aliingia madarakani mwaka 1987 kupitia mapinduzi ya kijeshi bila umwagaji damu na kumwondoa madarakani Habib Bourguiba aliyekuwa amejitangaza kuwa rais wa maisha wa nchi hiyo. Bin Ali aliiongoza Tunisia kwa mkono wa chuma kwa miaka 23 huku akiendeleza siasa za kutegemea Wamagharibi na kupiga vita Uislamu. Kujichoma moto kijana mmoja muuza mboga katika kulalamikia dhulma na ukatili wa maafisa usalama wa utawala wa nchi hiyo, kuliibua harakati ya wananchi wa Tunisia dhidi ya utawala wa kiufisadi wa Bin Ali na hatimaye kupinduliwa dikteta huyo.