Jan 14, 2020 23:17 UTC
  • Jumatano, Januari 15, 2020

Leo ni Jumatano tarehe 19 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na tarehe 15 Januari 2020 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 530 iliyopita Abulfadhl Abdulrahman Suyuti, mashuhuri kwa lakabu ya Jalaluddin, faqihi, mpokezi wa hadithi na mtaalamu maarufu wa lugha wa zama hizo alifariki dunia mjini Cairo. Jalaluddin Suyuti alizaliwa mwaka 849 Hijria na alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana. Jalaluddin Suyuti kwa miaka kadhaa alijifunza masomo ya fiqih, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na lugha na kupata mafanikio makubwa. Msomi huyo wa Cairo ameandika vitabu vingi vya thamani na miongoni mwavyo ni "Al Iqtirah", "Al Kitabul Kabir" na "Tarikhul Khulafaa".

Siku kama ya leo miaka 181 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 15 Januari 1839, nchi ya El Salvador ilijitangazia rasmi uhuru wake baada ya kusambaratika Muungano wa Amerika ya Kati, amma nchi hiyo haikupata amani na utulivu hata baada ya kupita karne moja. El Salvador ambayo ilikuwa ikikoloniwa na Uhispania kwa miaka kadhaa, ilijipatia uhuru wake mwaka 1821, na ulipofika mwaka 1824 ilijiunga na Muungano wa Amerika ya Kati, na hatimaye uliposambaratika muungano huo, nchi hiyo ilijitegemea kikamilifu. El Salvador ilikabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi mwaka 1931, baada ya kuporomoka bei ya kahawa katika soko la dunia, zao lililokuwa likitegemewa nchini humo. Hali mbaya ya kiuchumi iliwakasirisha wananchi wa nchi hiyo, na kupelekea kuanza kuibuka uasi wa wananchi na wanachuo dhidi ya dikteta Jenerali Maximiliano Hernandez Martinez wa El Salvador.

Bendera ya El Salvador

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita inayosadifiana na tarehe 25 Dey 1357 Hijria Shamsia, kulitokea mapigano makali baina ya jeshi la utawala wa Shah na wananchi wa Iran kufuatia maandamano ya mara kwa mara ya wananchi dhidi utawala huo wa kidikteta. Katika mapigano hayo baadhi ya wanajeshi waliotambua sababu za mapambano ya wananchi, waliamua kuzikimbia kambi zao za kijeshi na kujiunga katika safu za wananchi. Kujiunga wanajeshi na safu za wananchi ilikuwa bishara njema ya mabadiliko makubwa katika moyo na muundo wa jeshi la utawala wa Shah. Wakati huo huo Imam Khomeini ambaye alikuwa uhamishoni nchini Ufaransa, alikuwa akituma taarifa mara kwa mara akiwahimiza wanajeshi kujiunga na mapambano ya wananchi, kuuhami na kuutetea Uislamu na sheria zake na kuwafukuza wageni waliokuwa wakidhibiti kila kitu nchini Iran.

Na tarehe 15 Januari miaka 19 iliyopita ensaiklopidia ya Wikipedia ilianza kazi katika ntandao wa intaneti. Lengo la kuanzishwa ensaiklopidia hiyo limetajwa kuwa ni kupanua maarifa na uelewa wa watu kupitia njia ya kushirikishwa watu wote katika mradi huo. Insaiklopidia hiyo kubwa ya intaneti ina taarifa na makala kuhusu mamilioni ya vitu kwa lugha mbalimbali na ndiyo inayotembelewa zaidi na watu katika mtandao huo. Hata hivyo uwezekano wa kila mtu kuingia na kuandika atakavyo katika ensaiklopidia hiyo umeshusha chini hadhi na nafasi yake ya kielimu. Zaidi ni kwamba licha ya kuwa wasimamizi wa Wikipedia wanadai hawapendelei upande wowote lakini kwa kawaida makala zinazohusiana kwa njia moja au nyingine na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel huwa za upendeleo.

Kituo kikuu cha Wikipedia kiko katika jimbo la Florida nchini Marekani na ensaiklopidia hiyo inafanya kazi kwa mujibu wa sheria za Marekani.