Jan 16, 2020 23:07 UTC
  • Ijumaa, tarehe 17 Januari, 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 21 Jamadil Awwal mwaka 1441 Hijria sawa na Januari 17 mwaka 2020.

Miaka 1121 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 21 Mfunguo 8 mwaka 320 Hijiria, alizaliwa Abu Jaafar Ahmad bin Ibrahim Qiravani, katika mji wa Shirvan ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Msomi huyo alijulikana kwa jina maarufu la Ibn Jazzar, na alikuwa tabibu, mwanafalsafa na mwanajiografia mashuhuri wa Kiislamu. Ibn Jazzar alikuwa tabibu mwenye moyo wa kujitolea na anayewatakia watu mema na aliandika kitabu kiitwacho "Twibul Fuqaraa” au Tiba ya Watu Maskini." Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu 20. Miongoni mwa vitabu vyake ni Risalatun Fii Ibdalil Adwiya na Zadul Musafir.

Ibn Jazzar

Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita yaani tarehe 27 Dey 1334 Hijria Shamsia, Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.

Navvab Safavi

Miaka 59 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliuawa Patrice Lumumba mhandisi wa uhuru wa Kongo. Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Lumumba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960. Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa. Mwanamapinduzi huyo shujaa aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokita "Kongo, Nchi Yangu."

Patrice Lumumba

Katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, Sayyid Mahdi Hakim aliyekuwa mjumbe muhimu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq na mwana wa Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu aliuawa shahidi na makachero wa utawala wa Saddam Hussein dikteta wa zamani wa Iraq, huko Khartoum mji mkuu wa Sudan. Sayyid Mahdi Hakim alikuwa mmoja wa wanafunzi wa shahidi Ayatullah Sadr na mmoja wa wapinzani wakuu wa utawala wa Saddam Hussein.

Sayyid Mahdi Hakim

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, vikosi vya majeshi ya nchi kadhaa chini ya uongozi wa Marekani vilizishambulia ngome za wanajeshi wa Iraq huko Kuwait na Iraq ili kukomesha kukaliwa kwa mabavu Kuwait na jeshi la utawala wa Saddam. Mgogoro huo ulianza tarehe Pili mwezi Agosti mwaka 1990 baada ya utawala wa zamani wa Iraq kuikalila kwa mabavu ardhi ya Kuwait. 

Askari wa Marekani katika jangwa la Saudia baada ya Saddam kuvamia Kuwait

Miaka 11 iliyopita katika siku kama ya leo, Wazayuni maghasibu walilazimika kutangaza usitishaji vita baada ya jeshi la utawala wa Israel kufanya mashambulizi ya kinyama ya siku 22 dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza. Katika mashambulizi hayo, utawala wa Kizayuni ulikusudia kuiangamiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas au kwa uchache kuilazimisha harakati hiyo ikubali mazungumzo eti ya mapatano. Hata hivyo uungaji mkono wa Wapalestina kwa harakati ya Hamas na vilevile malalamiko makali ya walimwengu dhidi ya jinai za wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza, yaliulazimisha utawala haramu wa Israel usitishe mashambulio yake.

Ukanda wa Gaza