Jumamosi, 18 Januari, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 22 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1441 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 18 Januari 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 331 iliyopita, alizaliwa mwandishi na mwanafikra maarufu wa Ufaransa Charles de Montesquieu. Charles alikuwa miongoni mwa wasomi ambao fikra na itikadi zao zilikuwa na taathira kubwa katika harakati ya mapinduzi ya Ufaransa na alikuwa mtu wa kwanza kutoa nadharia ya udharura wa kutenganishwa mihimili mikuu mitatu ya dola yaani serikali, Bunge na Mahakama. Kitabu maarufu cha Charles de Montesquieu ni "The Spirit of the Laws" (Roho ya Sheria) ambacho kilichapishwa mwaka 1748 huko Geneva, Uswis. Kitabu kingine cha mwanafalsafa huyo wa Kifaransa ni (Barua za Kiirani) au "Persian Letters". ***
Katika siku kama ya leo miaka 105 iliyopita mkataba maarufu kwa jina la 'Mkataba wa Siri' ulitiwa saini kati ya nchi tatu za Ufaransa, Uingereza na Russia wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Sababu kuu ya mkataba huo ilikuwa kadhia ya kujiunga utawala wa Othmania (Ottoman Empire) na waitifaki wa Vita vya Kwanza vya Dunia, yaani Ujerumani na Austria. Kwani kujiunga utawala huo na waitifaki hao, kungekata uhusiano wa jeshi la majini la Russia na waitifaki wake katika Bahari Nyeusi. Baada ya kutiwa saini mkataba huo, nchi waitifaki zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya Lango Bahari la Dardanelles linalounganisha Bahari Nyeusi na Bahari ya Mediterania.***
Miaka 101 iliyopita yaani tarehe 18 Januari 1919, ulifanyika mkutano wa kihistoria wa amani baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, kwa kuwashirikisha wawakilishi wa nchi 27 kutoka mabara matano duniani. Mkuu wa mkutano huo alikuwa Georges Clémenceau, Waziri Mkuu wa wakati huo wa Ufaransa. Nchi tano zilizokuwa zimeshindwa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia yaani Ujerumani, Austria, Hungary, Bulgaria na dola la Othmania, hazikushiriki kwenye mkutano huo. Kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini katika mkutano huo, Ujerumani ililazimishwa kulipa fidia kubwa na kutoa sehemu za ardhi zake kwa Austria. Mkutano huo ulikuwa utangulizi wa kuanzishwa Jumuiya ya Kimataifa. ***
Na miaka 11 iliyopita mwafaka na tarehe 22 Jamadul-Awwal 1430 Hijria, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Muhammad Taqi Bahjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kishia. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchaji Mungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya alimu na mwanazuoni huyo. ***