Jumapili, 19 Januari, 2020
Leo ni Jumapili tarehe 23 Jamadil-Awwal 1441 Hijria, sawa na tarehe 19 Januari 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 889 iliyopita alifariki dunia na kuzikwa mjini Baghdad, Iraq Ibn Swadaqah, mmoja wa mawaziri na maafisa wa utawala wa Iraq. Kabla ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo alikuwa akijishughulisha na masomo ya fasihi na elimu ya hadithi. Mwaka 542 Hijiria aliteuliwa kuwa waziri na kupewa lakabu ya Qawamud-Din, ingawa uwaziri wake haukudumu kwa muda mrefu kutokana na wapinzani kumsema vibaya. Ni kufuatia hali hiyo ndipo akauzuliwa kwenye nafasi hiyo miaka miwili baadaye.
Siku kama ya leo miaka 284 iliyopita, sawa na tarehe 19 Januari 1736, alizaliwa James Watt, mvumbuzi na mhandisi wa Kiingereza. Msomi huyo alipendelea na kuvutiwa mno na utafiti kuhusu masuala ya kisayansi. Katika utafiti wake Watt alifanikiwa kuvumbua nishati ya mvuke na kuibua mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda hususan usafiri wa nchi kavu na baharini.
Siku kama ya leo miaka 222 iliyopita, sawa na tarehe 19 Januari 1798 Miladia, alizaliwa Auguste Comte mwanafalsafa, mwanahisabati wa Kifaransa na mtaalamu wa falsafa umbile au positivism kwa kimombo. Comte alifikia daraja ya uhadhiri katika hisabati akiwa na umri wa miaka 18 tu. Vitabu mashuhuri vya mwanafalsafa huyo wa Kifaransa ni Auguste Comte and positivism na Early Political Writings. Comte alifariki dunia mwaka 1857 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita sawa na tarehe 23 Jamadil-Awwal 1307 Hijiria, alifariki dunia Sayyid Muhammad Ibrahim mashuhuri kwa lakabu ya Sayyidul Ulamaa, alimu na fakihi wa Kiislamu wa nchini India. Alikuwa mmoja wa maulama watajika na mahiri wa mwanzoni mwa karne ya 14 Hijria. Baada ya kufariki dunia baba yake, Muhammad Ibrahim alichukua jukumu la kueneza mafundisho ya dini katika baadhi ya miji ya India. Mwanazuoni huyo alifanya hima kubwa ya kueneza misingi na itikadi za Kiislamu katika ardhi ya India. Vilevile ameandika vitabu na makala nyingi.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, wananchi Waislamu, wenye imani na umoja wa Iran walifanya maandamano makubwa kupinga mabaki yaliyosalia ya utawala wa kifalme wa Shah, yaani serikali ya Shapour Bakhtiar. Wafanya maandamano hao walitaka serikali hiyo ya kifalme itangazwe kuwa isiyo halali, na pia kung'olewa madarakani utawala wa Shah na badala yale kuundwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran. Siku hiyo Imam Khomeini MA akiwa mjini Paris alitoa ujumbe wa maandishi kwa wananchi wa Iran akisema: "Kwa uwezo wake Mola hivi karibuni nitaungana nanyi ili niweze kuwatumikia na kushirikiana bega kwa bega na matabaka yote ya wananchi kuelekea katika njia ya kujitawala na kuwa huru Iran.
Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita, Mahmoud al-Mabhouh, mmoja wa makamanda waandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS aliuawa shahidi huko mjini Dubai, katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Mabhouh aliuawa na makachero wa Shirika la Ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel walioingia nchini Imarati wakitumia pasipoti bandia. Al-Mabhouh alizaliwa katika familia iliyoshikamana na dini katika kambi ya Jabalia katika Ukanda wa Gaza, Palestina. Shahidi Mahmoud al-Mabhouh ni miongoni mwa waasisi wa Brigedi ya Izzudeen al-Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Baada ya kupita miezi kadhaa, Israel ilitangaza wazi kwamba, ilihusika na jinai ya kumuua al-Mabhouh.
Na siku kama ya leo tarehe 30 Dei inajulikana nchini Iran kwa anwani ya "Siku ya Gaza". Siku hii ni kumbukumbu ya kumalizika vita vya siku 22 vya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza ambapo vita hivyo vilifikia tamati kwa ushindi wa muqawama na mapambano ya Kiislamu huko Gaza. Kutokana na vyombo vya Magharibi kuficha jinai za utawala haramu wa Israel na kwa upande mwingine kutokana na hamasa kubwa iliyooonyeshwa na wananchi madhulumu wa Gaza katika kutetea ardhi zao, siku hii imepewa jina la "Siku ya Kitaifa ya Gaza.