Jumanne tarehe 21 Januari 2020
Leo ni Jumanne tarehe 25 Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na Januari 21 mwaka 2020.
Katika siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Muawiya bin Yazid, Khalifa wa tatu wa ukoo wa Bani Umayyah aliaga dunia katika mazingira ya kutatanisha. Alichukua hatamu za uongozi baada ya kuaga dunia baba yake yaani Yazid bin Muawiya. Hakuwa na hamu ya kuendelea kuongoza kwa sababu alikuwa akitambua kwamba, Ahlul Bait wa Mtume (a.s) ndio waliostahiki jambo hilo. Muawiya bin Yazid anayejulikana kama Muawiya wa Pili alitoa hotuba na kulaani vita vya babu yake yaani Muawiya bin Abi Sufyan dhidi ya Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) na vita vya baba yake, yaani Yazid dhidi ya Imam Hussein bin Ali (a.s) na kuwasifu Ahlul Bait (a.s).

Siku kama ya leo miaka 283 iliyopita tufani kubwa ililikumba eneo la Ghuba ya Bengali mashariki mwa India na kuua watu laki tatu. Tufani hiyo ilitambuliwa kuwa kimbunga kilichosababisha maafa makubwa zaidi katika eneo hilo. Ghuba ya Bengali iko kaskazini mwa Bahari ya Hindi na kusini mwa Asia na ni miongoni mwa maeneo ambayo hukumbwa na mafuriko na vimbunga vya mara kwa mara vinavyosababisha maafa makubwa ya nafsi na mali.

Katika siku kama ya leo miaka 227 iliyopita Mfalme Louis XIV wa Ufaransa alinyongwa. Alichukua hatamu za uongozi mwaka 1774 na kuathiriwa mno na mkewe Marie-Antoinette. Mwaka 1789 wananchi wa Ufaransa walianzisha mapambano dhidi ya Mfalme Louis XIV kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii na miaka mitatu baadaye serikali ya kifalme ilifutwa rasmi nchini Ufaransa. Hata hivyo kutokana na kuwa mfalme Louis alikuwa ameomba msaada wa nchi za kigeni kwa siri alituhumiwa kuwa amefanya uhaini na kuhukumiwa kifo. Watu kadhaa wa familia ya Mfalme Louis XIV akiwemo mkewe Marie-Antoinette pia walinyongwa.
Na siku kama ya leo miaka 41 liyopita sambamba na kuanza kutetereka nguzo za utawala wa Shah nchini Iran mkabala wa wimbi kubwa la mashinikizo ya wananchi na harakati za Mapinduzi ya Kiislamu, serikali ililazimika kuwaachia huru wafungwa waliokuwa katika jela za Shah na wananchi Waislamu wa Iran wakawapokea watoto wao waliokuwa wakiteseka kwa miaka mingi katika jela hizo. Alasiri ya siku hiyo maafisa wa Jeshi la Anga la Iran walifanya maandamano na kutangaza uungaji mkono wao kwa harakati ya taifa la Kiislamu la Iran. Siku hiyo hiyo pia magazeti ya Iran yaliandika habari iliyokuwa na kichwa kilichokolezwa wino kwamba: "Imam Khomeini Kurejea Iran Siku Kadhaa Zijazo". Habari hiyo ilizusha wimbi la hamasa na furaha kubwa kati ya wananchi wanamapinduzi wa Iran na kila mtu alianza kujitayarisha kwa ajili ya kwenda kumpokea kiongozi wa kihistoria wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Ruhullah Khomeini.
