Ijumaa, Januari 24, 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 28 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na Januari 24 mwaka 2020 Milaadia.
Siku kama hii ya leo miaka 41 iliyopita sawa na tarehe 4 Bahman mwaka 1357 Hijria Shamsiya, Shapour Bakhtiar Waziri Mkuu wa utawala wa Shah ambaye alikuwa akielewa kuwa kurejea Imam Khomeini nchini kutoka uhamishoni Paris kungempokonya udhibiti wa hali ya mambo, alitoa amri ya kufungwa viwanja vyote vya ndege vya Iran ili kuzuia kurejea nchini Imam Khomeini. Shapour Bakhtiar alichukua hatua hiyo baada ya kuchapishwa habari ya kukaribia kurejea nchini Imam Khomeini kutoka uhamishoni huko Paris Ufaransa. Hatua hiyo ya serikali ya utawala wa Shah iliwakasirisha wananchi ambao walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa ujio huo wa Imam Ruhullah Khomeini nchini Iran.
Miaka 55 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Winston Churchill, mwanasiasa maarufu wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 91. Churchill alizaliwa mwaka 1874 na mwaka 1895 alijiunga na jeshi la Uingereza na kushiriki katika vita vya kikoloni. Mwaka 1900 Winston Churchil aliingia katika bunge la Uingereza akikiwakilisha chama cha Kihafidhina na mara kadhaa aliongoza wizara mbalimbali na kwa vipindi viwili alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.
Miaka 122 iliyopita na katika sikukama ya leo, Mirza Muhammad Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mamar'ja' mashuhuri wa Kiislamu aliaga dunia. Alizaliwa Shiraz kusini mwa Iran na baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kuendeleza masomo yake ya kidini ambako alisomo kwa wanazuoni mashuhuri wa mji huo kama Sheikh Murtadha Ansari. Bidii yake kwenye masomo ilimuwezesha kukwea haraka daraja za elimu na kuwa mhadhiri na mwanazuoni wa ngazi za juu katika ulimwengu mzima wa Kiislamu. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa yake ya kuharamisha tumbaku katika kipindi cha utawala wa Nasiruddin Shah kutoka ukoo wa Qajaar. Fatuwa hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa ikihodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Fatuwa hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingereza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni nchini.
Katika siku kama ya leo miaka 161 iliyopita, kisima cha kwanza kabisa cha mafuta katika historia kilichimbwa huko Pennsylvania nchini Marekani. Kisima hicho kilichimbwa na Edwin Laurentine Drake kikiwa na kina cha urefu wa mita 230. Uchimbaji wa kisima hicho uliendelea kwa kipindi cha mwaka mmoja. Vifaa vilivyotumika kuchimbia kisima hicho vimehifadhiwa hadi leo katika jumba moja la makumbusho nchini Marekani.
Siku kama ya leo miaka 353 iliyopita, Mkataba wa Breda ulitiwa saini kati ya Uingereza na Uholanzi. Kwa mujibu wa mkataba huo, Uholanzi ambayo haikuwa na uwezo wa kulinda makoloni yake katika bara lililokuwa ndio kwanza limegunduliwa la Amerika, iliyakabidhi makoaloni yake hayo kwa Uingereza. Eneo muhimu ambalo Uingereza ilikabidhiwa ni New York, ambalo leo kijiografia linapatikana mashariki mwa Marekani.