Jumamosi, 25 Januari, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 29 Mfunguo Nane Jamadul Awwal 1441 Hijria mwafaka na tarehe 25 Januari 2020 Miladia.
Miaka 564 iliyopita katika siku kama ya leo, kazi ya uchapishaji vitabu ilianza na kitabu cha kwanza kabisa kikachapishwa kwa kutumia mashine iliyogunduliwa na Mjerumani, Johannes Gutenberg. Mashine hiyo ya uchapishaji ilikuwa hatua muhimu katika njia ya uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.' Hii leo kurasa kadhaa zilizobakia za kitabu hicho zinahifadhiwa katika majumba ya makumbusho. ***
Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria alifariki dunia Abdul Baqi bin Sulaiman Farooqi anayehesabiwa kuwa miongoni mwa wataalamu na malenga wa lugha ya Kiarabu. Alikuwa na kipawa cha kutunga mashairi ya kuvutia tangu akiwa kijana. Abdul Baqi alikuwa miongoni mwa wapenzi wa kizazi cha mtukufu Mtume Muhammad (saw) na alidhihirisha mapenzi yake hayo katika mashairi yake. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na kile alichokipa jina la "Al Baqiyatus Swalihat."***
Katika siku kama ya leo miaka 167 iliyopita, alizaliwa alimu na mtaalamu wa lugha wa Kiirani Ayatullah Sheikh Muhammad Qasim Ordubadi katika mji wa Tabriz ulioko kaskazini Magharibi mwa Iran. Baada ya kumaliza masomo yake ya kati alielekea Najaf nchini Iraq ambapo alipata elimu kwa Maulamaa mashuhuri wa mji huo. Msomi huyo mkubwa baada ya kufikia daraja ya ijtihadi alirejea katika mji wa Tabriz na kuanza kufundisha. Ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha "Al Shihabul Mubin fii I'jaazil Qur'an." Alifariki dunia mwaka 1333 Hijria. ***
Siku kama ya leo miaka 149 iliyopita, vijidudu maradhi vinavyosababisha maradhi ya ukoma viligunduliwa na tabibu na mhakiki wa Norway kwa jina la Gerhard Henrik Armauer Hansen. Ugonjwa huo huambatana na vidonda vikali vinavyovuruga na kuharibu maumbo ya muathirika. Vijidudu maradhi vya ugonjwa huo wa ukoma pia hukusanyika katika mishipa ya neva na kusababisha uharibifu katika sehemu kubwa ya mishipa hiyo. Maradhi hayo hujitokeza zaidi katika maeneo yenye joto. Licha ya maendeleo makubwa ya kisayansi yaliyopatikana katika kudhibiti ugonjwa wa ukoma, lakini njia ya kutibu maradhi hayo sugu bado haijapatikana na idadi kubwa ya waathirika wake wanaendelea kuteseka katika nchi mbalimbali duniani. ***
Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, licha ya kuwa makachero wa utawala wa Shah hapa Iran ulikuwa umepiga marufuku mkusanyiko wa zaidi ya watu wawili katika miji mingi hapa nchini, lakini matabaka mbalimbali ya wananchi yalipuuza monyo ya serikali ya kijeshi dhidi ya maandamno na kuendelea kufanya maandamano. Mamluki wa utawala wa Mfalme Shah walitumia mabavu na ukandamizaji mkali, ingawa hawakufanikiwa kuwadhibiti wananchi. Ukatili na utumiaji mabavu wa maafisa usalama dhidi ya wananchi ulipelekea kuuawa shahidi idadi kubwa ya wananchi katika miji mbalimbali ya Iran. Siku hiyo hiyo maafisa wa jeshi la anga walijitokeza katika barabara za Tehran na kuandamana dhidi ya utawala wa Shah na kutangaza utiifu wao kwa Imam Khomeini (MA).
Katika siku kama ya leo ya tarehe 29 Mfunguo Nane Jamadul Awwal miaka 33 iliyopita, Ayatullah Sayyid Mahdi Hakim mjumbe mahiri wa Baraza Kuu la Kiislamu nchini Iraq na mtoto wa Ayatullah al-Udhma Sayyid Muhsin Hakim mmoja wa Marajii wakubwa wa Kiislamu aliauawa shahidi huko Khartoum Sudan na maafisa usalama wa utawala wa Saddam Hussein. Sayyid Mahdi Hakim ni mwanafunzi wa Shahidi Ayatullah Sadr na alikuwa mmoja wa wapinzani wakubwa wa dikteta Saddam. ***
Na miaka 14 iliyopita katika siku kama ya leo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge ikiwa ni mara ya kwanza kwa harakati hiyo kushiriki kwenye zoezi hilo. Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na waangalizi wa kigeni, Hamas ilifanikiwa kupata viti 76 kati ya jumla viti 132 vya Bunge la Palestina licha ya propaganda chafu zilizokuwa zikifanywa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Kwa utaratibu huo Hamas ilimuarifisha Ismail Hania kama Waziri Mkuu na kutangaza kwamba itaunda serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na muitifaki wake Israel, zilikataa kutambua rasmi serikali hiyo iliyochaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Palestina.