Jan 27, 2020 23:15 UTC
  • Jumanne, Januari 28, 2020

Leo ni Jumanne tarehe Pili Mfunguo Tisa Jamadithani 1441 Hijria sawa na Januari 28 mwaka 2020 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 7 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilituma kwa mara ya kwanza kiumbe hai katika anga za mbali kwa kutumia roketi. Kiumbe huyo alikuwa tumbili ambaye alirejea salama ardhini baada ya jaribio hilo lililofanyika kwa mafanikio. Majaribio hayo yalidhihirisha tena maendeleo makubwa ya Iran katika masuala ya anga licha ya vikwazo vikali zaidi vya Marekani na waitifaki wake. 

Siku hii ya leo, yaani tarehe 28 mwezi Januari, inaadhimishwa duniani kama Siku ya Kimataifa ya Kuwasaidia Wagonjwa Wenye Maradhi ya Ukoma. Siku hii ilipewa jina hilo na Raul Follivero, raia wa Ufaransa yapata nusu karne iliyopita. Wakati huo dunia ilikuwa na watu milioni 15 waliokuwa wakisumbuliwa na maradhi hayo. Kufuatia hali hiyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliiainisha tarehe 28 Januari kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ugonjwa wa Ukoma. Tangu yalipoanza mapambano dhidi ya ukoma  waathirika wa maradhi hayo wamepungua na kufikia watu milioni mbili. Hata hivyo licha ya juhudi hizo, ugonjwa wa ukoma bado haujatokomezwa kikamilifu.

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita Shapoor Bakhtiyar, Waziri Mkuu kibaraka wa Shah wa Iran alitangaza kwamba ataelekea Paris, Ufaransa kwa shabaha ya kukutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu Imam Ruhullah Khomeini. Katika upande wa pili, Imam Khomeini alitangaza akiwa Paris kwamba, hamtambui Bakhtiyar kuwa ni Waziri Mkuu wa Iran, tofauti na uvumi uliokuwa ukienezwa wakati huo. Imam alisisitiza kuwa hatampokea wala kuzungumza na Waziri Mkuu wa Shah kabla hajajiuzulu. Siku hiyo hiyo wananchi wa Tehran walikusanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mehrabad kwa ajili ya kujiandaa zaidi na kutayarisha mipango ya kumpokea Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini (MA).

Shapoor Bakhtiyar

Miaka 41 iliyopita katika siku kama hii ya leo, kundi kubwa la wanazuoni wa Kiislamu lilianzisha mgomo wa kuketi katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran baada ya Waziri Mkuu wa serikali ya wakati huo ya Shah, Shapoor Bakhtiyar, kumzuia Imam Khomeini kurejea nchini Iran akitokea uhamishoni. Wanazuoni hao walisema, sharti pekee la kusitisha mgomo huo ni kuruhusiwa Imam Khomeini kurejea nchini. Mgomo huo ulikuwa miongoni mwa matukio muhimu katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Kwani kwa upande mmoja, serikali ya wakati huo ya Shah iliyokuwa ikiungwa mkono na Marekani, ilifanya jitihada kubwa za kumzuia Imam Khomeini asirejee nchini, na kwa upande mwingine ilikuwa ikifanya njama za kuzusha hitilafu na migawanyiko kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi kwa kutoa ahadi na kutumia vitisho. Mgomo huo wa wanazuoni wa Kiislamu uliowashirikisha maulamaa mashuhuri kama Shahid Ayatullah Murtadha Mutahhari na Ayatullah Muhammad Beheshti, ulikifanya Chuo Kikuu cha Tehran kuwa kituo kikuu cha harakati za mapambano.

Mgomo wa wananchuo wa Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Tehran

Siku kama ya leo miaka 782 iliyopita alifariki dunia Abu Bakr Muhammad bin Ahmad maarufu kwa jina la Ibn Sayyidun-Naas, faqihi, mtaalamu wa hadithi, mwanahistoria na mtaalamu wa fasihi wa Andalusia au Hispania ya leo. Mwanazuoni huyo alifariki dunia nchini Tunisia. Ibn Sayyidun-Naas alizaliwa mwaka 597 Hijiria katika viunga vya mji wa Seville (Ishbilia) huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na masomo. Abu Bakr Muhammad bin Ahmad alifundisha kwa miaka mingi katika eneo hilo na kulea wanafunzi wengi. Msomi huyo alitabahari pia katika taaluma ya mashairi na fasihi na mashairi yake mengi yanamsifu Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni kile cha Sira na Maisha ya Mtume Muhammad (saw).