Jumatano tarehe 29 Januari 2020
Leo ni Jumatano tarehe Tatu Jamadithani 1441 Hijria sawa na 29 Januari 2020.
Siku kama ya leo, miaka 1430 iliyopita, sawa na tarehe tatu Jamadithani mwaka wa 11 Hijiria alikufa shahidi Bibi Fatimatu Zahra (as), binti wa Mtume Muhammad (saw) na mke wa Imam Ali Bin Abi Twalib (as), baada ya muda mfupi wa maisha yake. Bibi Fatimat Zahra alizaliwa miaka mitano baada ya kubaathiwa na Mwenyezi Mungu Mtume wa Allah. Mama yake Bibi Fatimatu Zahra ni Bibi Khadija Binti Khuwailid (as) mwanamke mtakatifu na aliyekuwa akipendwa sana na Nabii wa Allah (saw). Chini ya malezi ya baba yake, Bibi Fatima alifikia daraja la juu katika maarifa, elimu na uchamungu. Katika maisha yake, Bibi huyo mtukufu alifahamika sana kwa ukarimu, kujitolea, subira, uchamungu na kuwasaidia masikini na watu wasiojiweza. Bibi Fatima Zahra aliishi miezi michache baada ya kufariki dunia baba yake, Mtume Muhammad (saw). Bibi huyo alijishughulisha na kuwalea wanawe yaani Imam Hassan na Imam Hussein (as) ambao wametajwa na Bwana Mtume kuwa ni Mabwana wa Vijana wa Peponi. Wasomi wengi wamemzungumzia Bibi Fatima (as) na kumtaja kuwa kigezo bora cha jamii na shaksia ya mwanamke mkamilifu wa Kiislamu. Redio Tehran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa msiba huu mchungu wa kumpoteza mtukufu huyo.

Katika siku kama hii ya leo miaka 94 iliyopita alizaliwa mjini Punjab, mashariki mwa Pakistan, Mohammad Abdus Salam, mwanafizikia mkubwa wa nchi hiyo. Alikuwa na juhudi kubwa kwenye masomo tangu akiwa kijana mdogo na akiwa na umri wa miaka 14 alijiunga na Chuo Kikuu cha Mjini Punjab. Baada ya kupata shahada ya uzamili katika chuo kikuu hicho, Abdus Salam alijiunga na chuo kikuu cha Cambridge nchini Uingereza. Hatimaye akiwa katika chuo hicho, Abdus Salam alijiunga na taaluma ya fizikia ambapo mwaka 1951 alifanikiwa kupata tuzo ya Adams. Katika mwaka huo huo msomi huyo alirejea nchini kwake na kujishughulisha na kazi ya ukufunzi. Hata hivyo kukosekana kwa zana na vitendeakazi, kulimfanya arejee tena nchini Uingereza na baadaye kusafiri latika nchi nyingi za Ulaya ambapo aliongoza taasisi kadhaa za kielimu barani humo. Mohammad Abdus Salam, alifariki dunia mwaka 1996.
Siku kama ya leo miaka 78 baada ya vikosi vya Uingereza na Umoja wa Kisovieti kuivamia Iran tarehe 20 Shahrivar mwaka 1320 Hijria Shamsia, kukatiwa saini makubaliano ya pande tatu baina ya nchi hizo. Kwa mujibu wa mkataba na makubaliano hayo, serikali ya wakati huo ya Iran ikawa haina budi ghairi ya kukubali kuruhusu njia zake za mawasiliano za ardhini, angani na majini kwa ajili ya nchi waitifaki ili zitumie njia hizo kwa ajili kuipelekea suhula kambi ya Umoja wa Kisovieti iliyokuwa ikipigana dhidi ya Ujerumani ya Kinazi.
Tarehe 29 Januari miaka 57 iliyopita alifariki dunia mshairi wa Kimarekani Robert Frost. Malenga huyo alizaliwa mwaka 1874. Kipaji chake kikubwa katika sanaa ya mashairi kilimuwezesha kuandika diwani yake ya kwanza ya mashairi akiwa na umri wa miaka 20. Frost aliipa diwani hiyo ya mashairi jina la "A Boy's Will". Malenga huyo mara kadhaa alitunukiwa tuzo ya usanii ya Pulitzer.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita sawa na tarehe 9 Bahman mwaka 1357 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, watu wengi wa mji wa Tehran walielekea katika msikiti wa chuo Kikuu cha Tehran baada ya wanaharakati wa kidini kukusanyika katika chuo hicho wakipinga hatua ya utawala wa Shah ya kumzuia Imam Khomeini (M.A) kurejea nchini. Wananchi waliandamana katika miji mingine ya Iran kupinga hatua hiyo na kutaka kupinduliwa utawala wa kidhulma wa Shah na kurejea Imam Khomeini (M.A) nchini. Siku hiyo wanajeshi wa utawala wa Shah kwa mara nyingine waliwashambulia wananchi na kujeruhi na kuua shahidi Waislamu wengi miongoni mwao.