Alkhamisi tarehe 30 Januari 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 4 Jamadithani 1441 Hijria sawa na Januari 30 mwaka 2020.
Miaka 86 iliyopita katika siku kama ya leo, kilianza kipindi cha uongozi wa Adolph Hitler, dikteta mbaguzi wa Kinazi wa Ujerumani. Chama cha Taifa cha Kisoshalisti cha Wafanyakazi wa Ujerumani ambacho kiliasisiwa na Hitler kilishinda viti 107 vya bunge katika uchaguzi wa mwaka 1930. Adolph Hitler alijitangaza kuwa kiongozi wa Ujerumani mwaka 1934 baada ya kuwa Kansela na Rais wa nchi hiyo. Hitler aliwafanya mamilioni ya wanadamu kuwa wahanga wa malengo yake ya kibaguzi. Hatua ya Adolph Hitler ya kuivamia Poland mwezi Septemba mwaka 1939 ilichochea Vita vya Pili vya Dunia na hatimaye Ujerumani na waitifaki wake walishindwa katika vita hivyo. Hitler alijiua mwaka 1945 baada ya Ujerumani kushindwa katika vita hivyo.
Katika siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, kiongozi wa taifa la India na mpigania uhuru wa nchi hiyo Mohandas Karamchand Gandhi aliuawa na kijana mmoja wa Kihindu aliyekuwa na misimamo mikali. Gandhi alizaliwa mwaka 1869 na baada ya kukamilisha masomo alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya sheria nchini Uingereza. Mohandas Gandhi kwa muda fulani pia alikuwa kiongozi wa wanamapambano wa Kihindi huko Afrika Kusini. Gandhi pia aliwaongoza wananchi wa India dhidi ya serikali ya kikoloni ya Uingereza katika kupigania ukombozi wa nchi hiyo. India ilipata uhuru mwaka 1947 chini ya uongozi wa Gandhi.
Tarehe 4 Jumadi Thani miaka 66 iliyopita Sayyid Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi akiwa pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita yaani tarehe 10 Bahman 1357 Hijria Shamsia, wahadhiri na matabaka mengine ya wananchi walitangaza mshikamamo wao na kuamua kuungana na viongozi wa kidini waliokuwa wamekusanyika katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran nchini Iran kuupinga utawala wa Shah. Katika hali ambayo idadi ya watu katika mkusanyiko ilikuwa ikiongezeka kila dakika, Shapour Bakhtiyar, Waziri Mkuu kibaraka wa utawala wa Shah alilazimika kukubali Imam Khomeini arejee nchini Iran kutoka uhamishoni nchini Ufaransa. Sambamba na hayo ndege za kijeshi za Marekani zilianza kuwaondoa raia wa nchi hiyo nchini Iran.