Jumapili 2 Februari, 2020
Leo ni Jumapili tarehe 7 Mfungo Tisa Jamadu th-Thani 1441 Hijria, mwafaka na tarehe Pili Februari 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 916 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, yaani sawa na tarehe 7 Mfunguo Tisa Jamadu th-Thani 525 Hijria, alinyongwa na kuuliwa shahidi arifu mkubwa wa Kiislamu Ainul Qudhat Hamedani, aliyekuwa na lakabu ya Abul Fadhaail. Alikuwa fakihi, mwanafasihi, msomi, mshairi na malenga stadi. Ainul Qudhat alizaliwa mwaka 492 Hijria. Msomi huyo hakuwa na woga katika kueleza itikadi zake na alikuwa shujaa na muwazi. Kutokana na sifa hiyo mwaka 525 Hijria alikamatwa kwa amri ya waziri wa Sultani Ahmad Sanjar wa utawala wa Kiseljuqi na kufungwa jela mjini Baghdad. Baadaye alihamishiwa Hamedan nchini Iran na kunyongwa kando ya shule yake. Miongoni mwa vitabu vya Ainul Qudhat Hamedani ni "Tamhidaat" na "Haqaiqul Qur'an."
Siku kama ya leo miaka 798 iliyopita alifariki dunia mjini Cairo, Misri Bahaud-Din Abul-Abbas, maarufu kwa jina la 'Qadhi Ashraf' aalimu mkubwa wa nchini Misri. Kama alivyokuwa baba yake katika ukadhi, naye pia alijishughulisha na kazi hiyo hiyo ya ukadhi. Alikuwa na akili sana ambapo pia alimuiga baba yake hata katika hati ya uandishi. Qadhi Ashraf alinukuu na kukusanya hadithi zenye itibari kutoka kwa wataalamu wa zama zake. Miongoni mwa athari za Bahaud-Din Abul-Abbas ni pamoja na majimui ya hadithi alizozikusanya.
Siku kama ya leo miaka 228 iliyopita, mkataba wa kihistoria wa Berlin, ulitiwa saini baina ya Leopold II mfalme wa wakati huo wa Austria na Frederick William aliyekuwa mfalme wa Prussia. Mkataba huo ulikuwa natija ya maafikiano baina ya viongozi hao wawili yaliyofikiwa tarehe Pili Agosti mwaka 1791 huko Pillnitz kwa ajili ya kukabiliana na mapinduzi ya Ufaransa. Hii ilitokana na kuwa, watawala wa Ulaya walikuwa wameingiwa na woga mkubwa kutokana na baadhi ya nadharia za wapigania uhuru wa Ufaransa. Licha ya kuweko mkataba huo na hata mashambulio ya pamoja ya Austria, Prussia na Uingereza dhidi ya Ufaransa na himaya yao kwa wapigania mfumo wa utawala wa Kifalme wa nchi hiyo, lakini harakati hizo hazikuwa na natija kwani hatimaye wanamapinduzi wa Ufaransa waliibuka na ushindi.
Siku kama ya leo miaka 124 iliyopita yaani tarehe 13 Bahman 1274 Hijiria Shamsia, aliaga dunia Ayatullah Mirza Javad Mujtahid Tabrizi, alimu, msomi, mwanamapambano na mchaji-Mungu. Alizaliwa mjini Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran katika familia iliyosifika kwa kushikama na dini. Mirza Javad Tabrizi alisoma masomo ya awali kwa baba yake na kisha akaelekea katika mji wa Najaf Iraq ambapo akiwa huko alihudhuria darsa za maulama waliokuwa mahiri katika zama hizo kama Sheikh Muurtadha Ansari na Sayyid Hussein Kuh Kamari na kufanikiwa kufikia marhala ya Ijtihadi. Baada ya kurejea katika mji aliozaliwa wa Tabriz, Ayatullah Mirza Javad Tabrizi alijishughulisha na tablighi na kazi ya kufundisha. Akiwa Imam wa Swala ya Ijumaa mjini Tabiriz, msomi huuyo alikuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa wananchi. Ayatullah Mirza Javad Tabrizi alikuwa akipinga vikali uingiliaji wa Russia na Uingereza katika masuala ya ndani ya Iran.
Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita, Dmitri Ivanovich Mendeleev msomi na mwanakemia wa Kirusi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 73 huko Saint Petersburg uliokuwa mji mkuu wa Russia wakati huo. Dmitri alizaliwa mwaka 1834 na kusoma taaluma ya kemia. Msomi huyo alifanya utafiti na uhakiki mkubwa muhimu katika taaluma ya kemia ambapo baadaye uliandaa jedwali la masuala ya kemia mashuhuri kama Jedwali la Mendeleev.
Na siku kama ya leo miaka 100 iliyopita yaani tarehe 13 Bahman 1298 Hijiria Shamsia, alizaliwa Ustadh Shahidi Murtadha Mutahhari. Ustadh Mutahhari alizaliwa katika mji wa Fariman Iran na baada ya kumaliza masomo ya awali alisafiri na kuelekea katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Qum na kuhudhuria darsa za wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Ayatullah al-Udhma Buroujerdi, Allama Tabatabai na Imam Khomeini MA. Wakati wa kuanza harakati ya Kiislamu nchini Iran, Shahidi Murtadha Mutahhari naye alijunga na harakati hiyo. Mutahhari alitiwa mbaroni mara kadhaa na vyombo vya usalama vya utawala wa Shah. Mbali na harakati za kisiasa, Ayatullah Mutahhari alikuwa na nafasi muhimu pia katika harakati za kijamii na uandishi wa vitabu ambapo amevirithisha vizazi vya baada yake vitabu vingi na vyenye thamani kubwa. Hatimaye aalimu huyo mwanamapambano na asiyechoka aliuawa shahidi na watenda jinai majahili wa kundi ovu la Furqan, usiku wa tarehe 12 Ordebehesht 1358 Hijiria Shamsia.