Feb 03, 2020 02:30 UTC
  • Jumatatu tarehe 3 Februari mwaka 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 8 Jamathani 1441 Hijria sawa na Februari 3 mwaka 2020.

Tarehe 3 Februari miaka 552 iliyopita, alifariki dunia mvumbuzi wa mashine ya uchapishaji, Johannes Gutenberg. Mvumbuzi huyo alizaliwa nchini Ujerumani lakini alihamia Strasbourg, Ufaransa na akaanza kujishughulisha na kazi za kiufundi. Mwaka 1443 au 1444 Gutenberg alifanikiwa kutengeneza mashine ya uchapishaji na kupiga hatua muhimu katika uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.'

Johannes Gutenberg

Miaka 190 iliyopita katika siku kama ya leo, Ugiriki ilipata uhuru wake kutoka kwa utawala wa Othmania. Ugiriki ambayo kijiografia ipo kusini mashariki mwa Ulaya ni moja kati ya nchi zenye tamaduni kongwe duniani. Mwaka 338 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s, mfalme wa Macedonia aliivamia Ugiriki na karne moja baadaye nchi hiyo ikawa chini ya mamlaka ya utawala wa Roma na baadaye Roma ya Mashariki. Katika kipicdi chote cha karne ya 19, Ugiriki ilishuhudia mapigano vita na vurugu za ndani na nje. Hatimaye katika siku kama ya leo nchi hiyo ikajipatia uhuru. 

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, mfereji wa Suez uliokuwa ukidhibitiwa na Uingereza, ulishambuliwa na vikosi vya majeshi ya Ujerumani na utawala wa Othmaniya katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Udhibiti wa mfereji huo wa Suez ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa pande mbili zilizokuwa zikipigana katika Vita vya Kwanza vya Dunia kutokana na ukweli kwamba mfereji huo ndio unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu. Uingereza ambayo haikuwa tayari kupoteza makoloni yake ya Asia, ilipigana vikali na majeshi ya Ujerumani na utawala wa Othomaniya na kupata ushindi. Mfereji wa Suez uliendelea kudhibitiwa na Uingereza hadi ulipotaifishwa na kiongozi wa Misri Gamal Abdul Nasir hapo mwaka 1956.

Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, Woodrow Wilson Rais wa 28 wa Marekani alifariki dunia. Woodrow Wilson alizaliwa 1913 na akiwa na umri wa miaka 57 alichukua hatamu za uongozi wa Marekani. Kama walivyokuwa marais waliomtangulia wa Marekani, na yeye alikita zaidi katika kuingilia masuala ya ndani ya Amerika ya Kati. Kipindi cha urais wa Woodrow Wilson kilitawaliwa na uingiliaji na uvamizi wa kijeshi dhidi ya maeneo mbalimbali duniani. Nusu ya kipindi cha utawala wa Woodrow Wilson, kilishuhudia Marekani ikishughulishwa na vita. Nchi zilizoshambuliwa kijeshi na Marekani katika uongozi wa Rais Woodrow Wilson ni Haiti, Guatemala, Dominican na Cuba.

Woodrow Wilson

Miaka 64 iliyopita katika siku kama hii ya leo mnamo tarehe 8 Jamadu Thani mwaka 1377 Hijria, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin Aamali Aalim mkubwa wa Kiislamu. Ayatullah Sharafuddin alizaliwa mwaka 1290 Hijria huko Kadhimein moja kati ya miji ya Iraq. Aidha alielekea Jabal Amil nchini Lebanon baada ya kuhitimu masomo yake na kuanza kujishughulisha na harakati za Kiislamu. Aalim huyo mkubwa ametoa huduma za thamani kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu na daima alikuwa akisisitiza suala la umoja baina ya Waislamu duniani. Ayatullah Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin ameandika vitabu na risala nyingi pia ili kufikiwa lengo hilo.

Ayatullah Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin Aamali

Miaka 41 iliyopita katika siku kama hii ya leo, katika hali ambayo mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah yalikuwa yamefikia kileleni baada ya Imam Ruhullah Khomeini kurejea nchini akitokea uhamishoni, Waziri Mkuu wa utawala wa kifalme wa Shah, Shapur Bakhtiyar alifanya jitihada za kuwatuliza wananchi bila ya mafanikio yoyote. Bakhtiyar alifanya juhudi za kusitisha harakati za Mapinduzi kwa kujidhihirisha kuwa ni mwanademokrasia na mpigania uhuru na akasema kwamba, hatamruhusu Imam Khomeini kuunda serikali ya mpito nchini. Wakati huo uasi wa kiraia, kukimbia wanajeshi na kujiunga na safu za wananchi katika miji mbalimbali ya Iran ikiwa ni pamoja na kujiuzulu wabunge, viongozi wa ngazi za juu serikalini na kadhalika kuliifanya serikali ishindwe kudhibiti hali ya mambo nchini.

Imam Khomeini

Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilirusha kwa mafanikio kombora la kwanza la kupeleka satalaiti angani la Omid. Miaka iliyofuata Iran ilituma viumbe hai angani kwa mafanikio ikiwa ni pamoja na kobe na tumbili na hatua hiyo iliingiaza Iran katika klabu ya nchi zenye teknolojia ya anga za mbali tena katika kipindi hicho cha vikwazo vikali vya kiuchumi vya nchi za Magharibi.