Feb 07, 2020 23:31 UTC
  • Jumamosi, 08 Februari, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 13 Mfunguo Tisa Jamadi Thani 1441 Hijria mwafaka na tarehe 8 Februari 2020.

Siku kama ya leo miaka 1375 kwa mujibu wa riwaya mashuhuri, aliaga dunia Umm al-Banin mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (as) na mama wa Abul Fadhil al-Abbas (as). Baada ya kupita miaka mingi baada ya kufariki dunia Bibi Fatma Zahra (as), Imam Ali (as) alimuoa Umm al-Banin aliyejulikana kwa jina la Fatima al-Kilabiya baada ya kushauriwa na ndugu yake yaani Aqil aliyekuwa msomi wa nasaba na koo za Kiarabu. Umm al-Banin alizaa na Imam Ali watoto wanne ambao ni Abbas, Ja'afar, Abdallah na Othaman na hivyo akaondokea kuwa mashuhuri kwa lakabu ya Umm al-Banin yaani mama wa  watoto wa kiume. Watoto wote hao wa kiume wa Umm al-Banin waliuawa shahidi katika tukio la umwagaji damu la Karbala. Umm al-Banin alifariki dunia miaka mitatu baada ya tukio la Karbala na kuzikwa katika mji wa Madina.***

Umm al-Banin

 

Katika siku kama ya leo miaka 1011 iliyopita Ibn Haytham mwanafizikia na msomi mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia huko Cairo Misri. Alizaliwa mwaka 354 katika mji wa Basra kusini mwa Iraq ya leo.  Ibn Haytham baada ya kufanya hima na juhudi kubwa na utafiti wenye thamani aliibuka na kuwa mwanahisabari stadi.  Ibn Haytham alikuwa mwalimu mahiri katika masomo ya fizikia, tiba, falsafa na nujumu. Aidha  alifanya utafiki wa kuzingatiwa kuhusiana na nuru. ***

Ibn Haytham

 

Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo, Kanali Abdu Salam Arif alifanikiwa kushika hatamu za uongozi nchini Iraq, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akishirikiana na maafisa wa kijeshi wa Chama cha Baath. Akisaidiwa na majeshi ya anga ya Iraq, Kanali Abdu Salam Arif alilishambulia jengo la Wizara ya Ulinzi ya Iraq yalipokuwa makao ya Abdul-Karim Qassim, Rais wa wakati huo wa nchi hiyo. Baada ya kumtia mbaroni na kumuua Rais huyo, Abdu Salam Arif alijitangaza kuwa Rais wa nchi hiyo. Abdul-Karim Qassim alikuwa ameingia madarakani mwaka 1958, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu dhidi ya mfalme wa mwisho wa Iraq. Kanali Abdul Salam Arif alifariki dunia mwaka 1966 katika tukio la kutatanisha la ajali ya helikopta, na kaka yake yaani Abdul-Rahman Arif akawa Rais wa Iraq. ***

Abdul-Salam Arif

 

Na katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, wananchi wa Iran walifanya maandamano makubwa katika miji mbalimbali ya Iran na kusisitiza juu ya kuendelezwa mapambano hadi kuuangusha utawala wa Shah. Mamilioni ya wananchi Waislamu wa Iran waliandamana katika siku kama hii wakiitikia wito wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu aliyewataka waiunge mkono serikali ya muda ya Mapinduzi. Katika upande mwingine maafisa na vikosi vya Jeshi la Anga la Iran huku vikiwa katika sare zao za kijeshi, walielekea kwa Imam na kutangaza mshikamano wao na Mapinduzi ya Kiislamu na uongozi wa Imam Khomeini. Katika mazungumzo hayo, Imam Ruhullah Khomeini aliwaambia wanajeshi hao kwamba walikuwa watumishi wa utawala wa kitaghuti na sasa wamejiunga na Qur'ani. Hatua ya vikosi vya Jeshi la Anga la Iran ya kutangaza utiifu wao kwa Imam Khomeini iliukasirisha sana utawala wa Shah.  Siku hii inajulikana hapa Iran kama siku ya Jeshi la Anga. ***