Jumatatu tarehe 10 Februari 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 15 Jamadithani 1441 Hijria sawa na Februari 10 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1404 iliyopita yaani tarehe 15 Jumadithani mwaka 36 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, vilitokea vita vya Jamal baina ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kundi la waasi waliozusha vurugu na fitina. Katika vita hivyo, jeshi la Kiislamu lililishinda kundi hilo ambalo lilianzisha uasi baada ya kushindwa kustahamili uadilifu wa Imam Ali, na hivyo kuamua kuvunja baia na kiapo chao cha utiifu. Viongozi wa kundi hilo ambalo lilijulikana kwa jina la Nakithina yaani wavunja ahadi, walikuwa Twalha na Zubair, ambapo waliamua kukusanya jeshi kubwa na kulichochea kwa matarajio ya kufikia malengo batili ya kutaka kutwaa utawala kwa nguvu.

Tarehe 15 Jumadi Thani mwaka 771 katika siku kama ya leo miaka 669 iliyopita, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Hilli, maarufu kwa jina la 'Fakhrul Muhaqqiqiin', faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu. Mwanachuoni huyo alizaliwa mwaka 682 Hijria na kupata elimu ya kidini kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. Fakhrul Muhaqqiqiin ameacha vitabu vingi na miongoni mwavyo ni Manbaul Asrar na Tahswilul Najah.

Katika siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, tawala za waitifaki na zile zilizokuwa zikihasimiana katika Vita vya Pili vya Dunia zilisaini makubaliano ya amani. Katika siku hiyo, Marekani, Urusi ya zamani, Uingereza na Ufaransa zilisaini makubaliano ya amani na nchi zilizoshindwa katika vita hivyo yaani Italia, Finland, Poland, Hungary, Romania na Bulgaria, na kwa utaratibu huo nchi sita hizo kwa mara nyingine tena zikajipatia uhuru wake.
Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita yaani tarehe 10 Februari mwaka 1950, Joseph Mc Carthy Seneta wa chama cha Republican cha nchini Marekani aliwasilisha orodha ya majina ya wafanyakazi 205 wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo akiwatuhumu kuunga mkono ukomonisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani. Hatua hiyo ilipelekea kuanza kwa kile kilichojulikana kama "Mc Carthisim" huko nchini Marekani, ambapo kwa mujibu wake wanafikra, wataalamu na viongozi mbalimbali wa Marekani walifuatiliwa na kusakwa baada ya kutuhumiwa kuwa na mitazamo na fikra za Kikomonisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani. Kamisheni ya Mc Carthisim ambayo ilikabiliwa na upinzani mkubwa, iliwafuta kazi karibu watumishi wa serikali wapatao 2000 huku idadi kubwa ya wataalamu na wasomi wakiswekwa jela kwa tuhuma zisizokuwa na msingi.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita majenerali wa utawala wa Shah waliongeza muda wa serikali ya kijeshi katika mji wa Tehran. Majenerali hao walichukua hatua hiyo ili kuwazuia wananchi kuwaunga mkono na kuwasadia wanajeshi wa kikosi cha anga ambao walikuwa wakishambuliwa na kikosi cha gadi ya Shah, na kwa njia hiyo waweze kumtia mbaroni Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu pamoja na shakhsiya wengine muhimu waliokuwa katika harakati za Mapinduzi au kuwauwa. Lakini Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuona mbali na kusoma vyema nyakati, aliwatolea mwito wananchi kupuuza kizuizi hicho kilichowekwa na majenerali wa Shah cha kuongeza muda wa serikali ya kijeshi au sheria za kutotoka nje. Wananchi wanamapinduzi wa Iran pia waliitikia agizo hilo la Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu na kumininika katika mitaa mbalimbali na kueneza mapambano yao katika vituo vingine vya kijeshi vya utawala wa kidikteta wa Shah katika mji wa Tehran na miji mingineo.