Alkhamisi tarehe 13 Februari 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 18 Jamadithani 141 Hijria sawa na tarehe 13 Februari 2020.
Siku kama ya leo miaka 422 iliyopita aliuawa shahidi Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari, faqihi, mwanatheolojia na alimu mkubwa. Alizaliwa mwaka 956 Hijiria katika familia bora na ya kielimu mjini Shushtar, kusini magharibi mwa Iran. Sayyid Nurullah Shushtari alijifunza masomo ya awali ya kidini kwa baba yake na kisha akaelekea mjini Mash’had, kaskazini mashariki mwa Iran na kuweza kustafidi na elimu kutoka kwa maulama wakubwa wa mji huo. Yapata mwaka 993, Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari alielekea India kwa ajili ya kufanya tablighi ambapo wakati huo nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Mfalme Akbar Shah katika silsila ya Mongolia huku ikiwa na utulivu. Hadhi yake, elimu na uadilifu wa Sayyid Shushtari vilimfanya ateuliwe kuwa kadhi wa mji wa Lahore nchini humo. Baada ya kufariki dunia Mfalme Akbar Shah, wapinzani wa alimu huyo walimwendea mfalme aliyechukua uongozi kwa jina la Jahangir Shah na kumwambia maneno ya uongo na ya uchonganishi ambapo kwa kutumia kisingizio cha madhehebu ya Shia ya alimu huyo mkubwa akauawa shahidi katika siku kama ya leo. Sayyid Nurullah Shushtari aliandika vitabu kadhaa miongoni mwavyo ni ‘Majaalisu-Mu’miniina’ ‘Ihqaaqul-Haqqi’ na ‘Tuhfatul-Uquul.’

Katika siku kama ya leo miaka 331 iliyopita tangazo lililojulikana kama Tangazo la Sheria lilisomwa katika sherehe za kumvika taji Mfalme William wa Tatu na Malkia Marry wa Pili wa Uingereza na kuanzia hapo mfumo wa utawala wa nchi hiyo ukabadilika na kuwa utawala wa kifalme wa kikatiba. Kwa mujibu wa tangazo hilo, madaraka ya Mfalme wa Uingereza yalipunguzwa na kukabidhiwa bunge la nchi hiyo.
Tarehe 18 Jumadi Thani miaka 160 iliyopita aliaga dunia faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Murtadha Ansari katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq. Alizaliwa mwaka 1214 Hijria Shamsia katika mji wa Dezful nchini Iran na baada ya kupata elimu ya msingi kwa baba yake alielekea katika miji mitakatifu ya Karbala na Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Miaka kadhaa baadaye Sheikh Ansari alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni na walimu mashuhuri wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Rasail na Makasib ambavyo vingali vinatumiwa hadi sasa kufundishia katika vyuo vikuu vya kidini.
Siku kama ya leo mwaka 1945 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, ndege za kivita za Uingereza na Marekani zilianza kudondosha zaidi ya tani 3900 za mabomu katika mji wa Dresden nchini Ujerumani. Mashambulizi hayo yaliua zaidi ya watu 25,000 na kusababisha majonzi na vilio kote duniani.
Miaka 32 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Ayatullah Sheikh Salman Khaqani. Alizaliwa mwaka 1293 Hijria Shamsia katika moja ya miji ya kusini mwa Iraq ya leo. Baada ya kupitisha kipindi cha utoto, akiwa na umri wa miaka 13 alihajiri na kuelekea Najaf al-Ashraf kwa ajili ya kusoma masomo ya dini. Akiendelea na masomo yake, Sheikh Salman Khaqani hakuacha kujihusisha na harakati za kijamii, kiasiasa na kifasihi. Akiwa na umri wa miaka 43 na baada ya kufariki dunia baba yake aliyekuwa mmoja wa maulama wa Khorramshahr hapa Iran aliuchagua mji huo kuwa makazi yake. Katika kipindi cha miongo mitatu ya kuishi kwake mjini Khorramshahr, mwanazuoni huyo aliondokea kuwa chimbuko la uongofu wa watu na kufanikiwa kutoa huduma zenye thamani kubwa. Baada ya kuanza vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Baath wa Iraq, nyumba ya alimu huyo ilikuwa kimbilio la watu.